Ni KMC FC dhidi ya Geita Gold FC ndani ya Chamanzi Complex kesho

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

KIKOSI cha Timu ya KMC kesho kitashuka katika dimba la Chamanzi Complex lililopo Kata ya Chamanzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania Bara dhidi ya Geita Gold, mchezo utakaopigwa saa 16:00 jioni.
Mchezo huo wa mzunguko wa nane utapigwa kesho huku KMC FC ikiwa mwenyeji na ambapo hadi sasa maandalizi yameshafanyika kwa asilimia kubwa na kikosi kipo tayari kwa mtanange huo.

Hayo yamebainishwa leo Desemba 4,2021 na Christina Mwagala ambaye ni Afisa Habari na Mawasiliano KMC FC.

Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni chini ya Kocha Mkuu  John Simkoko na wasaidizi wake Habibu Kondo pamoja na Hamad Ally imefanya maandalizi ya kutosha huku malengo makubwa kwenye mchezo huo ni kuhakikisha kwamba kama timu inapata ushindi.

Licha ya ushindani uliopo kwa timu pinzani Geita Gold, amesema bado kikosi kina matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa kesho na hivyo kuondoka na alama tatu muhimu ambazo kila mmoja anazihitaji.

"Kwa ujumla kikosi kipo vizuri, wachezaji wana afya njema, wana morali nzuri na kikubwa maandalizi yamekamilika kwa asilimia kubwa, hivyo tutakwenda kupabambania alama tatu.

"Maandalizi yetu kwa kiasi kikubwa yamefanyika vizuri, kwa sababu tunajua mchezo utakuwa na ushindani mkubwa sana, na sisi tunahitaji matokeo hivyo tutakwenda kupambana ukizingatia KMC ni timu bora ni lazima tuendelee kuonyesha ubora wetu,"amesema.

Hadi Sasa KMC FC imecheza michezo Saba ambapo kati ya michezo hiyo imeshinda mmoja na kupoteza michezo mitatu huku ikitoka sare kwenye michezo mitatu na kujikusanyia jumla ya alama sita na magoli manne hadi sasa na kuwa kweye nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news