Nyika FC kuingia kambini kujiandaa na Ligi ya RCL

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MABINGWA wa soka Mkoa wa Pwani, Nyika FC wanatarajia kuingia kambini Desemba 20, mwaka huu kwa ajili ya kujiandaa na Ligi ya Kanda na Mabingwa wa Mikoa (RCL).

Akizungumza na waandishi mjini Kibaha, ofisa habari wa timu hiyo, Boniventure Ndaka amesema kuwa, timu hiyo itaingia kambini chini ya kocha mkuu, Ally Bobea na msaidizi wake, Silvester Mgonafivi.
Ndaka amesema kuwa, makocha hao wataanza rasmi kuinoa timu hiyo ambayo itaweka kambi yake maeneo ya Msangani Kibaha kwa kuyafanyia kazi makosa madogo madogo ya wachezaji wake yaliyojitokeza wakati wa mashindano ya ligi ya mkoa yaliyomalizika hivi karibuni wilayani Mafia.

"Vile vile kwa upande wa usajili yaani dirisha dogo timu inasubiria maelekezo kutoka katika kanuni ya ligi hiyo ili iweze kutekeleza na kuyafanyia kazi mapungufu,"amesema Ndaka.

Amesema kuwa, malengo yao ni kuhakikisha timu yao inafanya vizuri kwenye ligi hiyo ambayo wanasubiri utaratibu kujua lini ligi itaanza kwa kushirikisha mikoa mbalimbali.

"Maandalizi mengine ni kuhakikisha wachezaji wenye majeraha watapatiwa matibabu ili wapone waweze kujiunga na timu watakapoanza mazoezi kabla ya mashindano ya Kanda na RCL,"amesema Ndaka.

Aidha, amesema kuwa wanamshukuru Kanali Cleophace na Kanali Kiwelu kwa kuilea vizuri timu ya Nyika na kuipa hamasa kwa kipindi chote cha mashindano ya ligi ya mkoa na kuifanya timu iweze kutwaa ubingwa.

"Tunawashukuru wadau wote wa soka waliopo Kamandi ya Jeshi Nchi Kavu na maeneo ya jirani wakiwemo viongozi wa timu hiyo Mwenyekiti Luteni Chesco Mdendemi na Katibu wake Sajenti Riziki Luo kwa ushirikiano wao waliouonyesha kuanzia mwanzo wa ligi hadi kufikia hatua waliyofikia,"amesema Ndaka.

Post a Comment

0 Comments