Rais Dkt.Mwinyi aelezea UVIKO-19 ulivyosababisha maumivu katika uchumi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, ugonjwa wa UVIKO-19 ulioikumba Dunia mbali ya kuathiri kiafya, lakini umesababisha matatizo makubwa ya kiuchumi.

Alhaj Dkt.Mwinyi amesema hayo Desemba 3, 2021 wakati alipozungumza na waumini wa dini ya Kiislamu wa Kijiji cha Uzini pamoja na vitiongoji vyake, mara baada ya kukamilisha Ibada ya Sala ya Ijumaa, iliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa Uzini, Wilaya ya Kati Mkoa Kusini Unguja.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na viongozi alipowasili katika Msikiti wa Ijumaa katika Kijiji cha Uzini Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja Desemba 3,2021. (Picha na Ikulu).

Amesema, ugonjwa wa UVIKO-19 umesababisha baadhi ya nchi kufunga mipaka yao pamoja na kusimamisha shughuli za uzalishaji katika sekta mbalimbali za viwanda na hivyo kusababisha kupanda kwa gharama za bidhaa pamoja na gharama za usafirishaji.

Katika salamu zake kwa waumini wa kijiji hicho, Alhaj Dkt.Mwinyi alisema kuwa ugonjwa huo umeathiri jamii kiafya na kiuchumi, hivyo akawataka waumini kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili kuliondoa janga hilo.

Alhaj Dkt. Mwinyi aligusia kuwepo kwa matukio mbalimbali yanayoiathiri jamii hapa nchini, ikiwemo vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na kubainisha hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na vitendo hivyo ikiwemo kutunga sheria kali kwa washtakiwa.

Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi alikubali ombi la wananchi wa Kijiji cha Uzini la kuifanyia matengenezo barabara yao inayoingia ndani kuelekea msikiti mkuu wa Ijumaa Uzini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi alipokuwa akizungumza na kuwasalimia wananchi wa Kijiji cha cha Uzini Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja,baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema barabara hiyo itaingizwa katika mpango wa matengenezo ya barabara za ndani zenye jumla ya urefu wa kilomita 270 zitakazojengwa kwa kiwango cha lami na hivyo, akawataka waumini hao kuielimisha jamii juu ya muhimu wa kujenga nyumba zao masafa marefu kando ya barabara, ili kuiepusha Serikali na gharama za ulipaji wa fidia.

Naye Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Mwinyi kwa utaratibu aliojiwekea wa kuungana na waumini kupitia Ibada za sala za Ijumaa katika misikiti mbalimbali Mjini na Vijijini.

Alisema, utaratibu huo unampa fursa ya kuonana na wananchi na kusikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Mapema, Khatibu wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa Uzini, Maalim Ali Vuai alisisitiza wajibu wa waumini kutekeleza Ibada ya sala tano, kuambatana na masharti yake, ikiwemo wakati.

Alisema, sala ni miongoni mwa ibada kubwa na akabainisha kauli ya Mtume Muhammad (SAW) juu ya utekelezaji wa ibada hiyo kuwa ndio nguzo kubwa ya Dini ya Kiislamu na kusema kwa yule atayeiacha atakuwa amevunja dini hiyo.

Aidha, Maalim Vuai alimuomba Mwenyezi Mungu kuijaalia Zanzibar kuwa nchi ya amani pamoja na kuondokana na matatizo mbalimbali, ikiwemo ya udhalilishaji wa kijinsia, rushwa pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi (wa tatu kushoto) pamoja na viongozi na Mashekhe walifika katika kaburi la Marehemu Ramadhan Abdalla Shaaban kumuombea dua, wakati wa uhai wake aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika Serikali ya Mapinduzi na Chama cha Mapinduzi ambapo alizikwa kijijini kwao Uzini Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja. (Picha na Ikulu).

Wakati huo huo, Alhaj Dk. Mwinyi mara baada ya salamu zake hizo aliungana na viongozi wengine wakiwemo wa msikiti huo katika dua maalum ya kuwaombea marehemu waliozikwa pembezoni mwa msikiti huo akiwemo mwanasiasa maarufu Marehemu Ramadhan Abdalla Shaaban.

Post a Comment

0 Comments