Rais Samia ahitimisha mbio za wasemaji wengi, asisitiza miradi yote itakamilika kwa viwango bora

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewashukia wanaodai miradi yote iliyoanzishwa na Serikali haiwezi kuendelezwa nchini.
Mheshimiwa Rais amesema, Serikali itaendelea na miradi yake ya kimkakati ikiwemo kukamilisha na kukuza biashara baina ya Tanzania na nchi jirani kwa maslahi mapana ya Taifa.

Rais Samia ameyasema hayo leo Desemba 28, 2021 katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha tatu kutoka Makutupora hadi Tabora chenye urefu wa kilomita 368.

Ujenzi utakaogharimu Shilingi trilioni 4.41ambao umesainiwa kati Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Yapi Merkez kutoka nchini Uturuki.

“Kwa sababu fedha hizi hatutazitoa kwenye tozo wala hatutazitoa kwenye kodi tunazokusanya ndani, ni lazima tutakopa kwa hiyo tutakopa ili kukamilisha mradi huu...kwa hiyo ni lazima tumalize huu mradi, tukope tumalize mradi,” amesema Rais Samia.

Amesema, mradi wa SGR ulianza kutekelezwa kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo ujenzi wa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ulianza mwaka 2017 na umegawanyika katika vipande vitano ukipita katika mikoa tisa.

Mheshimiwa Rais Samia ameongeza kuwa, ujenzi huo unaendelea katika vipande vitatu cha Dar es Salaam- Morogoro asilimia 95, Morogoro- Makutupora asilimia 77 na Mwanza-Isaka asilimia nne, ambapo ni jumla ya kilomita 1,063 za njia kuu za reli pamoja na njia za kupishana.

“Hii ni kazi kubwa yenye kuhitaji uthubutu mkubwa wa Serikali na wananchi wake. Hii inafanya uwekezaji wa ujenzi wa vipande vinne kati ya vitano vinavyoendelea kufikia kiasi cha sh trilioni 14.7 ukijumlisha na kodi,” amesema Rais Samia.

Amebainisha kuwa, tayari ameshaagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia TRC kukamilisha taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi kipande kilichobaki cha Tabora – Isaka na kipande kipya cha awamu ya pili kutoka Tabora hadi Kigoma.

Mheshimiwa Rais amesema, aliahidi kuendeleza mema yaliyopita, yaliyopo na kuanzisha mema mapya. 

Amesema,ujenzi na utekelezaji wa miradi yote iliyoanzishwa na inayoendelea Serikali itaendelea kuisimamia na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

"Sasa kuna wale ambao walipenda kuona miradi hii haiendelezwi na wanathubutu kusema kwamba miradi hii imeshindikana, haiendelezwi. Pamesemwa hapa makandarasi hawadai hata senti moja ila Serikali inadai kazi, hivyo hivyo kwa miradi mikubwa mingine. Ujenzi wa bwawa tunakwenda nao vizuri hatudaiwi na miradi mingine yote iliyoachwa tunakwenda nayo vizuri.

“Na mkipita pita huko hakuna mradi uliosimama, miradi yote inaendelea. Nataka kuwaambia Watanzania tutasimamia miradi iendelee, kwa hiyo kama walidhani kutakuwa na kusimamishwa miradi ili wapate la kusema halipo. Tutaendelea na ujenzi wa miradi, kuna jitihada za kutuvunja moyo katika mikopo, hata hizo nchi zilizoendelea zina mikopo mikubwa kuzidi ya kwetu,tutakopa tumalize miradi ya maendeleo,”amefafanua Mheshimiwa Rais Samia.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia amesema Serikali imeingia mkataba wa ununuzi wa mabehewa ya abiria 89, vichwa vya treni ya umeme 19, seti za treni za kisasa 10 zenye mabehewa 80 vikiwa na gharama ya dola za Marekani milioni 381.43.

Pia amesema, Serikali inaendelea kukamilisha ununuzi wa mabehewa ya mizigo 1430 yenye thamani dola za Marekani milioni 127.21.

“Nitumie fursa hii kuagiza wizara na TRC kuhakikisha kuwa inasimamia kwa karibu ili kasi ya ujenzi iendane na kasi ya kusimamia ununuzi wa vifaa hivyo. 

"Hii itafanya vifaa viwe vimekamilika sambamba na kukamilika kwa ujenzi wa reli. Vinginevyo miundombinu ya reli itakamilika huku tukisubiri kuwasili kwa vifaa na kuhakikisha ubora unaendana na thamani ya fedha.

“Nasema hivi kwa sababu miezi michache nimekaa katika Serikali hii nimeona kuna mambo yanataka kuanza kufanyika na mimi sitakubali yafanyike. Kwamba mradi unasimamiwa na wizara kupitia sekta husika, anatafutwa mkandarasi anapopatikana anakuwa na wasemaji wengi ndani ya nchi, na hasemewi bure watu wanajua watavuna. Sasa nasema mimi sijali mkandarasi atasemewa na watu elfu ninachotaka kusema nataka reli iwe ya viwango tulivyokubaliana,”amefafanua Rais Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news