Rais Samia atumia hekima kutuma ujumbe kwa IGP Sirro kuhusu askari wake

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameshangazwa na kitendo cha mmoja wa askari Polisi aliyevalia sare ya jeshi hilo akiisifu pombe haramu ya moshi (gongo).
Mheshimiwa Rais Samia ameyabainisha hayo Desemba 12,2021 wakati wa ufungaji wa Mafunzo ya Uofisa (Gazetted Officers) katika hafla ya ufungaji mafunzo iliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam.

“Kiukweli nilishangazwa na ile video yani askari kwenye sare za kazi anaisifia pombe haramu na pale kuna raia sasa sijui alikuwa ana maana gani?Clip kama hizi wengine tukiziona tunabaki tunasisimuka, mmh! haya bana sijui IGP na wewe uliiona na kama uliiona sijui yule bwana yuko wapi,”amesema Mheshimiwa Rais Samia huku akionekana kukerwa na kitendo hicho.

Mheshimiwa Rais Samia pia amelitaka Jeshi la Polisi kujipanga kikamilifu kuhakikisha usalama unatawala katika kipindi cha mwisho wa mwaka.

“Furaha ya kumaliza mwaka isije kuleta misiba ndani ya nchi yetu, Jeshi la Polisi likasimame vyema na doria zifanyike kila mara kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarika.Tumefanya kazi kubwa kupunguza makosa ya uhalifu mkubwa ambao ulitaka kuanza kuota mizizi, lakini tumefanikiwa kuondoa.

”Yaliyobaki ni haya makosa madogo nayo tuyafanyie kazi kuyapunguza, hatuwezi kusema tutamaliza ila tuhakikishe yanapungua kadiri ya uwezo wetu,”amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Samia amewataka askari wa usalama barabarani kuwa na lugha nzuri kwa raia na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Amesema hayo huku akitoa mfano kuhusu vitendo vya askari wa usalama barabarani kusimamisha magari na kuwataka madereva kuwapa fedha.

“Yaani askari anakusimamisha anaingiza kichwa ndani ya gari hajui ndani una nyundo au nondo, sasa najiuliza hivi mafunzo gani wanayopata hawa askari. Kuna siku nilikuwa natoka kwenye harusi ya kiongozi mmoja, ilikuwa saa saba usiku kumbe taa ya gari ilikuwa haiwaki nikakutana na askari wakanisimamisha.

"Wakanihoji nikawaambia sikuiona, nitairekebisha asubuhi, akakataa akasema mmezidi nyinyi Waarabu nyinyi sijui nani, akanipa makabila yote akaniambia twende kituoni ni umbali wa kilomita 15.Nikakubali tukaenda. Tulipofika nikawekwa kusubiri hatma yangu, sijui waliambizana nini akaja kuniuliza kwani wewe nani?

"Nikamwambia mie Samia, wakaniuliza nafanya kazi wapi, nikawambia nafanya kazi zangu. Naona alitonywa akaniruhusu kuondoka, nikamwambia siwezi kwenda mwenyewe akasema atanisindikiza, ona sasa akapata kazi ya kunisindikiza hadi kwangu.

"Mara nyingine nikataka kugongana na gari ya Polisi nikashika breki wakatoka wanafoka,nikapelekwa Polisi nikaandika maelezo nikawekwa huko mpaka magharibi imeingia mbu wananing'ata najipiga hivi wananiambia hawana shamba hao mbu Mama acha wale au tukufungie walio wengine? Amesema Mheshimiwa Rais Samia

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news