RC Kunenge azindua gari la kubebea wagonjwa Kata ya Kibindu

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani,Abubakar Kunenge amezindua gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) kwa ajili ya Kata Kibindu lililonunuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kwa gharama ya shilingi milioni 120.
Kunenge amezindua gari hilo hivi karibuni katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze,hafla ambayo imeshuhudiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Mwanasha Tumbo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Abdallh,madiwani na wananchi.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo Kunenge ameipongeza Halmashauri ya Chalinze kwa kazi kubwa iliyofanya ya kununua gari hilo kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wa Kata ya Kibindu na maeneo mengine.

Kunenge amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kubwa na maelekezo anayotoa yanalenga kuboresha huduma za jamii.

Amesema,Rais anafanya mambo mengi kuhakikisha ustawi wa jamii unapatikana kupitia vipaumbele vyake vya kutoa huduma kwa jamii hasa katika afya,elimu,barabara na masuala mengine huku akisema kuna kila sababu ya kumuunga mkono.
Kunenge,amesema Halmashauri ya Chalinze imeonyesha mfano mzuri wa kununua gari hilo lakini hatahivyo imekuwa ikifanya vizuri kutokana na uongozi bora huku akitaka Halmashauri nyingine ziige mfano huo.

Aidha, Kunenge ameziagiza Halmashauri zote zilizopo Mkoani Pwani kuhakikisha zinaweka utaratibu wa kupata magari ya wagonjwa sambamba na kujenga miundombinu ya madaktari,wauguzi na wataalamu wengine wa afya ili kusudi wafanyekazi katika mazingira bora zaidi.

Amesema,Mkoa wa Pwani unamahitaji ya magari ya wagonjwa 38 lakini yaliyopo hivi sasa ni 22 na kusema bado Halmashauri inatakiwa kufanyakazi ya kuhakikisha kila Halmashauri inapata magari ya kutosha .

"Naipongeza Halmashauri hii ya Chalinze kwa kufanya jambo jema la kununua gari hili lakini Chalinze inafanya vizuri hata katika ukusanyaji mapato , kwahiyo naomba muendelee kufanyakazi zaidi lakini ili mfikie malengo ni lazima ushirikiano kati yenu huwe mzuri," amesema Kunenge.
Hata hivyo,Kunenge ametaka gari hilo litumike vizuri kwa kufanyakazi iliyokusudiwa na waache kutumia gari hilo kubebea mkaa na kufanya shughuli za harusi na kwamba ikibainika hatua kali zitachukuliwa.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Allen Mlekwa,amesema kuwa Halmashauri ya Chalinze imenunua gari hilo kwa ajili ya kubeba wagonjwa wa Kata ya Kibindu na kupeleka katika hospitali za Wilaya,Mkoa na Rufaa.

Amesema kuwa, Chalinze kuna changamoto kubwa ya hupatikanaji wa magari ya wagonjwa kwani kwasasa Kuna magari matatu pekee huku mahitaji yake ni magari Saba huku akisema gari hilo mpya litahudumia maeneo ya Kibindu,Mbwewe na Mkange.

Mlekwa amesema tayari Wilaya imeweka utaratibu wa kuhakikisha wanapata gari mpya kila mwaka ili kusudi waweze kufikia malengo ya kupata magari saba yanayotakiwa Chalinze.

Diwani wa Kata ya Kibindu,Ramadhani Mkufya, ameshukuru kupatikana kwa gari hilo kwakuwa litasaidia kuokoa wajawazito ambao wamekuwa wamekuwa wakipata adha wakati wa kujifungua.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Hassan Mwinyikondo amesema kuwa, atahakikisha atafuatilia matumizi ya gari hilo pamoja na kusimamia hupatikanaji wa magari manne ya wagonjwa yanayotakiwa katika halmashauri yake.

Post a Comment

0 Comments