Serikali yatenga Bilioni 5/- kuboresha miji 45, wamachinga kuneemeka

NA FRED KIBANO

SERIKALI imesema shilingi Bilioni Tano zilizozotengwa zitasidia kupanga mipango ya miji na majiji 45 ikiwemo maeneo ya biashara ambayo yanatumiwa na wamachinga hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa alipokuwa akiongea na wafanyabiashara wadogo (wamachinga) jijini Mbeya ambapo ameeleza kuwa, changamoto zinazowakabili zinatambuliwa na Serikali na hatua stahiki zinachukuliwa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema, Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa makundi yote wanapofanya kazi zao bila bugudha yoyote kama ahadi ya Serikali ya Awamu ya Sita ilivyoagiza.

Aidha, ameuagiza Wakala wa Barabara za Mijini na Vijini (TARURA) kuhakikisha wanatengeneza barabara zote zinazozunguka eneo la Uwanja wa ndege wa zamani na soko la Salanga ambalo linatumiwa na wamachinga jijini Mbeya. 

Waziri Mkuu Majaliwa ameagiza wamachinga wote ambao walitelekeleza maeneo waliyopangiwa na Mamlaka ya Jiji la Mbeya hapo awali na kurejea tena baada ya kuanza kwa maboresho, wapatiwe nafasi za vibanda ili wafanyebiashara kwa kuwa Serikali inawajali wamachinga wote.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema, Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI ilipokea maagizo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kufanya upangaji wa wamachinga nchi nzima ili kuondoa kero zao ikiwemo maboresho ya maeneo ya kufanyia biashara.

“Naomba niwahakikishie kuwa Serikali ina mpango kwa miji 45 kupatiwa fedha kutoka Benki ya Dunia, Jiji la Mbeya likiwa ni mojawapo kupatiwa fedha za kujenga barabara, stendi za kisasa na eneo hili la wafanyabiashara wadogo wadogo (Wamachinga) lipo kwenye mpango wa kupatiwa fedha za Benki ya Dunia itakayoanza mwakani kwa ajili ya kuboresha eneo hili,”amesema Dkt.Dugange. 

Aidha, amesema Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya na Mstahiki Meya wameitwa Ofisi ya Rais TAMISEMI jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda kufanya tathmini ya mradi huo mapema iwezekanavyo ambayo itatatua kero ya wafanyabiashara wadogo wadogo.
Akitoa maelezo ya awali kabla ya hotuba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa, Juma Homera amesema eneo la Uwanja wa ndege wa zamani na Soko la Salanga lilikuwa na changamoto nyingi na hivyo kupelekea wafanyabiashara ndogondogo kulikimbia, lakini baada ya kuanza kuboreshwa wafanyabiashara hao wanaohitaji vibanda vya biashara eneo hilo wamerudi tena.

Mheshimiwa Homera amesema, mradi mpya wa kiwanda cha kusindika mboga mboga unaogharimu shilingi Bilioni moja na milioni mia sita unajengwa karibu na eneo hilo lakini utahitaji wafanyabiashara ndogo ngogo wapatao 200 na hivyo kutoa ajira kwao na wananchi wengine. 

Mbunge wa Mbeya Mjini, Dkt.Tulia Ackson ametoa ombi la kujengwa kwa barabara zenye kiwango cha lami kuzunguka eneo hilo na kuliinua juu kwa kuweka kifusi kwa kuwa mazingira ya eneo hilo ni chepe chepe kwani yanajaa maji kipindi cha masika.
Masanja Matondo Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wadogo (Machinga) mkoa wa Mbeya amesema, wanaiomba Serikali kuwafanyia mpango wa kupata mikopo nafuu kutoka kwenye benki kwa ajili ya kujenga vibanda vyao vya biashara, kupata mikopo ya asilimia 10 kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa, mikopo maalum kwa ajili ya kuwakopesha wamachinga, pamoja na Serikali kuuagiza Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kujenga barabara zenye kiwango cha lami kuzunguka eneo hilo la Uwanja wa ndege wa zamani na soko la Salanga.

Post a Comment

0 Comments