Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) labuni teknolojia mpya ya vitasa janja,kuanza na wadaiwa sugu Januari

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limebuni teknolojia mpya ya vitasa janja (smart lock) vitakavyofungwa katika nyumba kadhaa za mfano nchini ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa mkakati endelevu wa kuwabana walimbikizaji wa madeni sugu ya kodi katika nyumba zake.
Mfano wa vitasa janja.(Picha na Mtandao).

Teknolojia hiyo inatajwa kuwa njia rahisi na ya haraka ya kuwezesha shirika kukusanya kodi kwa wapangaji wake kwa wakati, kwani itakuwa na mfumo unaofanana na ule wa kulipia umeme kwa LUKU ambapo mpangaji kodi yake ikifikia mwisho wa mwezi mlango utajifunga na hataweza kuingia ndani hadi akalipe kodi.

Meneja wa Huduma na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Muungano Saguya ameyasema hayo leo Desemba 30,2021 wakati akizungumza na waandishi mbalimbali wa habari jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dkt.Maulidi Banyani kuelezea mafanikio mbalimbali waliyoyapata kwa mwaka 2021 na matarajio yao mwaka ujao wa 2022.

Saguya amesema kuwa, vitasa hivyo vitasaidia kuwabana walimbikizaji wa madeni sugu nchini.

"Zoezi hili litafanyika kufuatia baadhi ya wapangaji wetu kutolipa kodi kwa wakati na hivyo kulikosesha shirika mapato ambayo yangeweza kusaidia kuanzisha miradi mingine,"amebainisha Meneja huyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo.

Pia amefafanua kuwa, wameamua kubuni njia za kisasa kwa ajili ya kuhakikisha kodi ya pango inalipwa kwa wakati na kudhibiti malimbikizo ya kodi kwa wapangaji.

"Hadi sasa NHC, inadai malimbikizo ya kodi ya jumla ya shilingi bilioni 26 kutoka kwa wapangaji, hivyo kwa sasa shirika limeanza kuyafanyia mapitio madeni hayo kwa kuyahakiki. Lengo ni kubainisha kila mdaiwa na mahali alipo ili mwezi Januari (2022) shirika lianze kampeni kabambe ya kukusanya madeni hayo.

"Kupitia kampeni hiyo shirika halitakuwa na huruma kwa yeyote, kwani malimbikizo hayo yanachangia kuchelewesha utekelezaji wa miradi mingine nchini,"ameongeza.

Amesema, kwa mwaka huu wamehakiki wapangaji wote ili kujua uhalali wa upangaji wao na kubaini changamoto.

"Katika zoezi hili linaloendelea, shirika limebaini wapangaji wasio halali wanaoishi kwenye nyumba nyumba kinyume na taratibu wapatao 30 na tayari tumewachukulia hatua za kisheria kwa kuwanyang'anya upangaji na kuwapatia wanaostahili,"amesema Saguya.

Punde tutakuletea habari kwa kina kuhusu mafanikio ya NHC hapa, endelea kufuatilia DIRAMAKINI BLOG

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news