Uongozi DIRAMAKINI Blog wataja mambo manne kwa Watanzania 2022

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

UONGOZI wa Diramakini Blog umewatakia Watanzania heri ya mwaka mpya wa 2022 huku ukiwaomba kuendelea kudumisha amani, upendo, mshikamano na umoja katika kuliwezesha Taifa letu kusonga mbele kiuchumi na jamii kwa ujumla.
Hayo yamesemwa leo Desemba 31, 2021 na Mhariri Mkuu wa Diramakini Blog ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Diramakini Business Limited, Godfrey Nnko wakati akitoa salamu za kuuaga mwaka 2021 na kuukaribisha mwaka 2022 jijini Dar es Salaam.

Nnko amesema kuwa, mwaka 2021 unaondoka wakati ambao baadhi ya watendaji waandamizi wa Serikali wameonyesha udhaifu ambao kwa namna moja au nyingine umewapunguzia heshima katika jamii, lakini hilo halipaswi kuwakwamisha Watanzania kusonga mbele katika kuendeleza mshikamano na umoja ili kuisaidia Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya kazi ya kuwaletea maendeleo Watanzania wote.

"Hayo yamepita, tunakwenda kuanza ukurasa mpya, twendeni tukafanye kazi kwa bidii na kwa umoja ili siku kama ya leo mwakani tuweze kufanya tathimini ya mafanikio tele kwa Taifa letu na jamii, ninaamini kwa umoja wetu Watanzania tulionao tutafanikisha hayo.

"Kubwa zaidi tuzidi kumtegemea Mungu wetu, kuwa na malengo, kuziheshimu na kuzitii mamlaka zilizopo kuanzia ngazi ya chini hadi juu na hakika, Mungu atatubariki sana. Pia tuendelee kufanya kazi kwa bidii, mafanikio yetu na Taifa tumeyabeba sisi,"amesema Nnko.

Nnko amechukua nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa namna ambavyo wameshirikiana kuliongoza Taifa letu kwa amani, mshikamano na upendo.

"Mafanikio haya yanatokana na uongozi wao thabiti kwa kushirikiana na watendaji waadilifu na wazalendo ambao kwao Taifa letu ndiyo jambo la kwanza kuliko kitu chochote.Wale ambao walionyesha udhaifu, ninaamini mwaka 2022 watajisahihisha ili kwenda na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar chini ya Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi,"amefafanua Nnko.

Wakati huo huo, Nnko amesema Watanzania wamekirimiwa neema ya kipekee ya kumwamini Mungu, hivyo kwa nafasi hiyo hiyo waitumie kuyakataa mambo maovu katika jamii ikiwemo udokozi, wizi, ujambazi, matumizi na biashara ya dawa za kulevya,vitendo vya kikatili, ubadhirifu na uharibifu wa mali za umma na mengineyo ili kuwa na jamii inayojaliana na kuheshimiana ikiwemo Taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments