Waziri Aweso afagia vigogo wa maji Mtwara

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MHESHIMIWA Jumaa Aweso, Waziri wa Maji amefanya mabadiliko kwa kuwaondoa watumishi sita katika nyadhifa zao kwa sababu mbalimbali za kiutendaji uliosababisha kuzorota kwa hali ya utoaji wa huduma ya maji katika wilaya za Newala na Nanyamba mkoani Mtwara. 
Watumishi waliondolewa ni Mhandisi Primy Damas Shirima (Meneja wa RUWASA Mkoa), Mhandisi Rejea Ng'ondya (Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi Mtwara-MTUWASA), Mkemia Alualus Pius Mkula (Mkuu wa Maabara ya Ubora wa Maji Mkoa), 

Mhandisi Emanuel Konkomo (Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Makonde), Mhandisi Renard Baseki (Meneja wa RUWASA- Newala) na Ndugu Anza Simon Makala ( Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Makonde). 

Wataalam hao wa Sekta ya Maji watapangiwa majukumu mengine na wizara.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri amemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Maji kuharakisha mchakato wa kumpata Mkandarasi ambaye atajenga Mradi Mpya wa Makonde ambao miundombinu yake ya sasa imechakaa kutokana na kujengwa muda mrefu tangu enzi za ukoloni (Miaka ya 1950). Mapema mwezi huu Waziri alisaini Kibali cha kuanza Utekelezaji wa Mradi wa Mpya wa Makonde. 

Pia, ameelekeza Mzabuni wa pampu sita zenye thamani ya shilingi milioni 541 alete haraka pampu hizo ambazo zimenunuliwa na Serikali ikiwa ni Jitihada za kupunguza Changamoto upatikanaji wa huduma ya Maji katika Miji ya Newala Tandahimba.

Post a Comment

0 Comments