WAZIRI BITEKO ANA KWA ANA NA MRATIBU MKAZI WA UMOJA WA MATAIFA NCHINI

NA TITO MSELEM-WM

KATIKA harakati za kuvutia wawekezaji katika Sekta ya Madini nchini, Waziri wa Madini, Doto Biteko amekutana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Zlatan Milisic kujadili fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini.
Waziri Biteko amemweleza kuhusu uwepo wa viwanda vikubwa vitatu vya kusafisha madini ya dhahabu ambapo Kiwanda cha Mwanza kina uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku, Kiwanda cha Geita kina uwezo wa kusafisha kilo 400 za dhahabu kwa siku na kiwanda cha Dodoma kina uwezo wa kusafisha kilo 250 kwa siku.

Aidha, Waziri Biteko amemweleza kuhusu uwepo wa miradi mikubwa kadhaa inategemewa kuanza kazi nchini Tanzania ambapo Desemba 13, 2021 inategemea kusaini mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Black Rock Mining Ltd itakayochimba Madini ya Kinywe (Graphite), Strandline Resources Ltd itakayochimba madini ya ujenzi, Nyazaga itakayochimba Madini ya dhahabu, Petra Diamond Ltd itakayochimba Madini ya Almasi pamoja na PRNG itakayochimba Madini ya Rare Earth Element.

Pia, Waziri Biteko amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini huwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwajengea uwezo wa kuzalisha kwa tija kupitia mafunzo ya uchimbaji na uchenjuaji, kuwakopesha mitaji kwa ajili ya kuendesha shughuli zao na kuwaelimisha mbinu bora za matumizi ya teknolojia rahisi ya uchimbaji na uchenjuaji sababu ndiyo eneo linalotoa ajira kubwa kwa watanzania.
Pamoja na Mambo Mengine, Waziri Biteko amemuahidi Milisic kuwapeleka yeye na mabalozi wa Nchi mbalimbali wanaohudumu Tanzania kutembelea Kiwanda cha kusafisha Madini ya dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery Ltd pamoja na kutembelea migodi mkubwa na midogo iliopo nchini ili kujionea fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini.

Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Zlatan Milisic ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua nzuri inazozichukuwa katika kuwavutia wawekezaji hususan kwenye Sekta ya Madini na kutilia mkazo suala la uongezaji thamani madini nchini.
Milisic amesema anaunga mkono juhudi za uongezaji thamani madini kuliko kusafirishwa yakiwa ghafi pia, atahakikisha anafikisha taarifa kwa wadau wa maendeleo ili atakaye vutiwa aje Tanzania kuwekeza katika Sekta ya Madini.

“Nipo tayari kutoa ushirikiano katika kufanikisha harakati za Maendeleo katika Sekta ya Madini nchini Tanzania," amesema Milisic.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news