Waziri Mchengerwa aelekeza Afisa Manunuzi Mkuu TARURA kuondolewa kazini, kupisha uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha za miradi

NA JAMES K.MWANAMYOTO

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amemuelekeza Katibu Mkuu-UTUMISHI, kumuondoa kwenye nafasi yake Afisa Manunuzi Mkuu wa TARURA ili kupisha uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha za miradi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi wakati wa kikao kazi cha Mhe. Mchengerwa na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kagera.

Waziri Mchengerwa ametoa maelekezo hayo mkoani Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.

Mhe. Mchengerwa amesema, uamuzi wa kumuondoa mtumishi huyo, unatokana na taarifa za uwepo wa mikataba mingi iliyosainiwa na baada ya muda ikafanyiwa mapitio na kuongezwa fedha jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
Sehemu ya Viongozi na Watumishi wa Umma wa Umma wa Mkoa wa Kagera wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kagera.

“Wakati uchunguzi unaendelea, Afisa Manunuzi Mkuu huyo aripoti Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora siku ya Jumatatu tarehe 20 Desemba, 2021 na apelekwe Afisa mwingine atakayetekeleza majukumu yake,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.

Aidha, amemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kupitia mikataba yote ya TARURA na kuchukua hatua stahiki pale itakapothibitika kuna ubadhirifu wa fedha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kagera.

“Namuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kwenda TARURA kupitia mikataba yote kwa makini ili achukue hatua stahiki kwa watendaji ambao wanashiriki vitendo vya ubadhirifu vinavyokwamisha taifa kusonga mbele,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amesema kama taifa, ni lazima kufanya maamuzi magumu pale inapobidi ili nchi iweze kupiga hatua katika maendeleo na wananchi wanufaike.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akitunuku cheti cha utambuzi wa utendaji kazi mzuri kwa mtumishi wa Mkoa wa Kagera, Bi. Maria Valentine-Msaidizi wa Kumbukumbu Daraja la II, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Kagera.

Amesema, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alipofungua fursa za kiuchumi katika utekelezaji wa miradi ya serikali, alitaka taifa lipige hatua katika maendeleo na sio watu wafanye ubadhirifu wa fedha za umma, hivyo tumuunge mkono kwa kupinga vitendo vinavyorudisha nyuma maendeleo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akifafanua hoja zilizowasilishwa na Watumishi wa Mkoa wa Kagera wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa mkoa huo kilicholenga kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.

Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa, Watumishi wa Umma hawana sababu ya kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na ubadhirifu kwasababu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anajali maslahi yao na yeye ni msikivu kwa watumishi.

Mhe. Mchengerwa amefanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Kagera ambapo amezungumzat na watumishi, walengwa wa TASAF na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa na watumishi wa Mkoa wa Kagera kilicholenga kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.

Post a Comment

0 Comments