Waziri Ndumbaro: Ukiingiza mifugo Hifadhi ya Iluma utatozwa 100,000/- kila kichwa

NA LUSUNGU HELELA-WMU

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ametangaza rasmi kwa Wafugaji watakaothubutu kuingiza mifugo katika Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya ILUMA watatozwa faini ya kiasi cha shilingi 100,000 kwa kila kichwa cha ng'ombe baadala ya kiasi cha shilingi 50,000 iliyokuwa ikitozwa mwanzo.

Uamuzi huo unakuja baada ya malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wafugaji wakidai kuwa mifugo yao inapoingia katika Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya ILUMA ambako faini ni shilingi 50,000 imekuwa ikitolewa na Askari wa TANAPA na kisha huingizwa katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambako tozo yake ni shilingi 100,000 kwa kila kichwa cha ng'ombe.

Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro, Dkt. Ndumbaro amesema amefikia uamuzi huo ili kuwapa nafasi wafugaji wataokamatwa wakiwa wameingiza mifugo yao kati ya Hifadhi hizo kuamua kulipa kiasi hicho cha pesa kwa Uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere au kwa Uongozi wa Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya ILUMA kwa vile kote faini ni sawa.

Kwa mujibu wa taarifa, Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya ILUMA ni Hifadhi ya Wanyamapori inayomilikiwa Jamii ambayo ni muunganiko wa vijiji 14 ambavyo vilitoa ardhi kwa ajili ya shughuli ya Uhifadhi na pia ni Hifadhi ambayo inapakana na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.

''Habari ya kwamba ng'ombe wangu waliingizwa katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere itakuwa haipo kwa sasa kwa sababu faini ni sawa na ya Hifadhi ya ILUMA,'' alisisitiza Dkt. Ndumbaro.
Akizungumza na Wajumbe wa Kamati hizo, Dkt. Ndumbaro amesema kumezuka tabia ya Wafugaji kujichagulia kiasi cha faini ya kulipa pindi mifugo yao inapokamatwa ndani ya Hifadhi ya ILUMA amesisitiza kuwa jambo hilo kamwe halikubaliki.

Amesema,Mfugaji atakayekuwa na hatia hana haki ya kuchagua adhabu huku akisisitiza kuwa hali hiyo imepelekea wafugaji kusema uwongo kuwa ngombe zao pindi zinapokamatwa katika Hifadhi ya ILUMA zimekuwa zikiswaga katika Hifadhi ya Nyerere ambako faini yake ni kubwa jambo ambalo sio kweli.

''Kwa mamlaka niliyonayo kama Waziri mwenye dhamana natangaza kuanzia leo faini ni kiasi cha shilingi laki moja kwa kila kichwa cha ng'ombe,'' alisisitiza Dkt. Ndumbaro.

Akifafanua uamuzi huo wa kutoza kiasi cha shilingi 100,000 kwa kila kichwa cha ng'ombe atakayekutwa ndani ya Hifadhi ya ILUMA, Dkt, Ndumbaro amesema anaitumia faini hiyo kutoka katika kifungu cha sheria kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) pamoja na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Katika hatua nyingine, Dkt. Ndumbaro amevionya vijiji vinavyoandika barua ya kutaka kujitoa katika Hifadhi hiyo ya ILUMA huku akisisitiza kuwa kujitoa kwao hakuwapi nafasi ya kurudishiwa ardhi yao kwa sababu hakuna kijiji kinachomiliki ardhi katika Hifadhi hiyo ya ILUMA.

Amefafanua kuwa, hata wakijitoa hakuna kipande cha ardhi kitachorudishwa kwa kijiji chochote kwa vile kwa sasa ardhi hiyo ipo chini mamlaka ya Bodi ya Hifadhi hiyo pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Hata hivyo, amewasihi viongozi wa kisiasa wanachochea migogoro mbalimbali katika Hifadhi hiyo Jamii kuacha mara moja kabla hatua stahiki zikiwa bado hazijachukuliwa huku akimuagiza Mkuu wa wilaya hiyo kuwachukulia hatua watu wote watakaokutwa ndani ya hifadhi hiyo wakiwa wanalima na kuchungia mifugo katika Hifadhi ya ILUMA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news