Waziri Ummy asikitishwa na ufaulu wa darasa la saba, uandikishaji darasa la kwanza Nzega

NA NTEGHENJWA HOSSEAH,OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu amesikitishwa na kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.

Pia Mhe. Ummy ameonyesha kutoridhishwa na hali ya uandikishaji wa wanafunzi wa madarasa ya awali na wale wanaoanza darasa la kwanza katika wilaya hiyo.
Waziri Ummy ameonyesha hali hiyo wakati wa ziara yake wilayani humo na kupokea taarifa ya wilaya iliyowasilishwa kwake na Mkuu wa wilaya hiyo, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Mhe. Advera Bulimba.

Mhe. Ummy amesema kuanzia mwaka 2017 kiwango cha ufaulu wa wanafunzi waliohitimu darasa la saba kinashuka mwaka hadi mwaka.

Kwa mujibu wa taarifa, mwaka 2017 ufaulu ni asilimia 72,mwaka 2018 asilimia 63,mwaka 2019 asilimia 65, mwaka 2020 asilimia 58 na mwaka 2021 asilimia 56.

"Takwimu hizi haziridhishi kabisa, lazima mfanye uchunguzi wa kina kufahamu sababu ya kuporomoka kitaaluma namna hii,hili halivumiliki mnatakiwa kufanya kitu cha ziada kuhakikisha mnaongeza kiwango cha ufaulu,"amesema Mhe. Ummy.

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy alinyooshea kidogo idadi ndogo ya wanafunzi wanaoandikishwa kuanza shule ya awali sambamba na darasa la kwanza.

Ameweka bayana hali ya uandikishaji wa wanafunzi katika darasa la awali kwa mwaka 2021/22 ni asilimia 17 tu na kwa wanafunzi wanaotakiwa kuanza darasa la kwanza ni asilimia 14 tu.

"Kwa nini watoto wanaoandikishwa kuanza madarasa ya awali na darasa la kwanza ni wachache kiasi hiki ina maana hamhamasishi jamii kuandikisha watoto shule? Niwatake sasa kila mtu kwa nafasi yake aamke na kwenda kuhamasisha wananchi kupeleka watoto shule na takwimu zibadilike,"amesema Waziri Ummy.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani alisema kwa hali ilivyo sasa watatumia njia zote kuhakikisha watoto wanaandikishwa shule kama vile kupitisha gari la matangazo, kutumia mikutano na mikusanyiko kuhamasisha jamii na mwishoni kufanya msako nyumba kwa nyumba kubaini kama kuna mtoto mwenye umri wa kwenda shule ambaye hajaandikishwa.

Naye Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Sistaimelda Lubengona amesema,mwamko duni wa jamii sambamba na utoro wa mara kwa mara wa wanafunzi ni baadhi ya sababu zianzochangia kuporomoka kwa ufaulu katika halmashauri hiyo.

Pia ameahidi kwa sasa ataongeza jitihada katika kuhamaisha jamii kushiriki kikamilifu katika kuinua viwango vya elimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news