Dkt.Magere:Jamii iendelee kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO-19

NA DOREEN ALOYCE

JAMII imetakiwa kuendelea kujikinga na magonjwa ya UVIKO-19 kwa kuchukua tahadhari sambamba na kutambua tofauti iliyopo kati ya ugonjwa wa Mapafu TB na UVIKO-19.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la STEPS Tanzania,Dkt.Cyprian Magere wakati alipokuwa kwenye mafunzo kwa Asasi zisizo za Kiserikali ambazo zinatekeleza Afua za kifua kikuu, Ukimwi na Kuzuia maambukizi ya UVIKO-19 kwa mikoa ya Dodoma na Simiyu.

Amesema kuwa, mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo viongozi na wafanyakazi wa asasi hizo ili waweze kuibua wagonjwa wa kifua kikuu na wale walioacha kuendelea na matibabu kwa kipindi hiki cha mlipuko wa UViKO-19.

"Katika mafunzo haya tuna malengo mahususi kwa viongozi kupata uelewa wa kutosha wa kufanya kazi zao za kutoa huduma ya kuzuia maambukizi ya kifua kikuu, Ukimwi kwa kipindi hiki cha korona na kupata stadi za kutosha, hivyo kupitia mafunzo hayo ongezeko la idadi ya watu kupata chanjo litakuwepo,"amesema Magere.
Nae Ally Chionda ambaye ni Meneja Programu kutoka Taasisi ya STEPS Tanzania amesema, mafunzo hayo yamewezeshwa na Shirika la Amref chini ya ufadhili wa Mfuko wa Dunia kupitia Fedha za UVIKO-19 na kupitia mafunzo hayo yatasaidia watendaji kuwa na uelewa zaidi kuhusu tofauti iliyopo kati ya ugonjwa wa UViKO-19 pamoja na kifua kikuu TB.

Ally amesema kuwa, hapo awali waligundua changamoto kwa watoa huduma ngazi ya jamii namna ya kuifikia jamii kutokana na wasiwasi hivyo kuwepo mafunzo hayo utawafanya warudi kwenye mstari na kuendelea kuhamasisha watu kupata chanjo na kuendelea kutoa huduma bila kupata maambukizi.
"Kulikuwa na uhitaji wa hii elimu kujua mahusiano ya ugonjwa huo, tunatambua mtu mwenye kifua kikuu mtu akikohoa na yale maji maji yakimfikia mtu ambaye hana kifua kikuu kuna uwezekano wa kupata ugonjwa huo na pia mtu mwenye UVIKO-19 akikohoa na maji kumfikia ambayo yanaweza kumfikia haraka, hivyo vyote vinashabihiana na hata dalili zinafanana,"amesema Ally.

Akitoa elimu kwenye mafunzo hayo Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Dodoma, Dkt.Francis Bujiku amesema jamii inapaswa kutambua kuwa virusi waliowengi hawana tiba ila wana kinga huku akibainisha asili ya Virusi vya UVIKO-19 vimetokana na wanyama wakiwemo paka, ngamia na popo na kuenezwa kwa binadamu.
"Naomba niwaeleze kwamba ugonjwa wa UVIKO-19 hauenezwi kwa njia ya hewa bali inaenezwa kwa njia ya tone isipokuwa hewa inatusaidia kusambaza matone hivyo tuendelee kujikinga ili tusiambukizwe," amesema Dkt.Bujiku.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo hayo wamesema wataenda kuibua changamoto zinazosababisha watu wasichanje na watatumia fursa hiyo kuwapa elimu wananchi kutambua tofauti iliyopo kati ya Ugonjwa wa Mapafu TB pamoja na UVIKO-19 jambo ambalo litasaidia kupunguza vifo vinavyoweza kujitokeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news