Madereva bodaboda washukuru uwepo wa wasaidizi wa kisheria

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MADEREVA bodaboda katika Manispaa ya Morogoro wamesema uwepo wa Wasaidizi wa Kisheria katika maeneo wanayoishi imewasadia wengi wao kuwa na uelewa katika masuala mbalimbali yanayohusu haki. 
Msaidizi wa Kisheria,Tuasi Nitu akitoa elimu ya mkataba kwa kikundi cha bodaboda cha Barabara ya Mazimbu Kata ya Kihonda Manispaa ya Morogoro.

Wamesema, wamekuwa wakipewa pikipiki na mabosi wao bila kuwa na mkataba wowote kimaandishi na pindi inapotokea tatizo mmiliki wa pikipiki anatumia nguvu kuchukua chombo hicho cha usafiri bila dereva huyo kufaidika chochote. 

“Niliingia mkataba na bosi wangu,alinipa pikipiki kwa kipindi cha miezi 12,kwa siku nimpe shilingi 10,000, ilipofika miezi nane mmiliki huyo alichukua pikipiki wakati tulikubaliana nikimaliza miezi 12 pikipiki inakuwa yangu,nimeshindwa kumshtaki kutokana na hatukuwa na makubaliano ya kimaandishi,”amesema Andrew Antony. 

Andrew anasema, madereva wa bodaboda wengi wamepata shuluhisho la kudhulumiwa na kuonewa na wamiliki wa pikipiki,hivi baada ya kupewa elimu na Msadizi wa Kisheria Phisoo wamejua njia sahihi ya kudai haki zao bila kuvunja sheria. 

Anasema, elimu waliyoipata wanaitumia na pia kuwa elimisha bodaboda wengine pamoja na wamiliki namna ya kuingia mkataba kwa pande zote mbili kwa lengo la kuweza kufaidika na mkataba walioingia bila kuvunja sheria huku kila mtu akitimiza wajibu wake. 

Msaidizi wa Kisheria,Phisoo anasema wanapokutana na bodaboda huwa yanaibuka maswali mengi juu ya haki,ndipo wanapojipanga kutoa elimu kutokana hitaji husika,pia anasema wengi wanabadilika baada ya kupatiwa elimu na mara nyingi huwa wanafika ofisi za wasaidizi wa kisheria kuomba ushauri. 

Phisoo anasema, sekta ya bodaboda imekuwa ikilaumiwa sana kwa kushiriki katika vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuwalaghai wanafunzi na uvunjivu wa amani ndani ya jamii. 

“Lengo letu ni kuhakikisha boda boda hawa wanakuwa salama,na wanaaminika katika jamii wanazoishi kwani kuna wengine hata abiria wanaogopa kupanda pikipiki zao kutokana na matendo yao,tunawarudisha kwenye njia sahihi na wao wanapokea elimu na kubadilika,”anasema Phisoo. 

Msaidizi wa Kisheria,Tausi Nitu kutoka Kata ya Kihonda anasema, madereva bodaboda wengi wameonekana ndio wavunjivu wa sheria mbalimbali na wanapokamatwa hawajui njia sahihi ya kudai haki bila kuvunja sheria. 

Anasema, baada ya boda boda hao kupewa elimu walikubali kubadilika na kuwa mabalozi wa kusimamia haki katika kituo chao cha Mazimbu,na pia kutokubali kuingia mkataba bila ya kuwa na maandishi yanayoonyesha uhalali wa pande zote mbili. 

“Niwashukuru wasaidizi wa kisheria kwa kutupatia elimu juu ya mkataba,pia ukatilia wa Kijinsia,hivyo naomba wawe wanatembelea vijiwe vya bodaboda mara kwa mara kutujenga kwani wengi wetu hatuna elimu na tunaishia kila siku polisi na magereza,”anasema Raphael Augustino. 

Raphaeli anasema kuwa, bodaboda wengi lazima wakubali kubadilika ili kuweza kuendesha maisha yao,kwani wao wanategemea wateja ila wateja wakikosekana maisha yao yanakuwa magumu,hivyo wanapaswa kuwa waadilifu katika kazi na kujenga imani kwa jamii. 

Post a Comment

0 Comments