Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar asisitiza umuhimu wa kuyaenzi maridhiano ya kisiasa, kuyatunza Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema ili kuyafikia maendeleo ya kweli na kutimiza ndoto ya matunda ya Mapinduzi ya Januari mwaka 1964 hapa visiwani, hapana budi kuitunza amani, kuyalinda maridhiano ya kisiasa, na kuwekeza katika miradi mbalimbali inayolenga utoaji wa huduma bora kwa jamii.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo, akizindua majengo ya Ukumbi wa Kufanyia Mitihani ya Skuli ya Fujoni, Madarasa Matatu, na Jengo la Utawala katika Skuli ya Mahonda, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema,mafanikio na mustakabali mwema wa jamii ya watu wa Unguja na Pemba, ambayo ndiyo dhamira hasa ya Mapinduzi, yatafikiwa kwa kila mmoja kutekeleza wajibu, ukiwemo wa kuendelea kuiheshimu Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar iliyopo kwa mujibu wa Katiba. 

“Tutambue kuwa bila ya amani, haiwezekani kuyafikia maendeleo ya kweli, na kwamba pasi na kuyazingatia yote hayo ni vigumu mno kutimiza ndoto za matunda ya Mapinduzi,”amesema Mheshimiwa Othman.
Mheshimiwa Othman ameupongeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) kwa kazi zake nzuri zinazoendelea kufanyika nchi nzima, akisema ni dhahiri ni mkombozi mkubwa wa wanyonge, na kwamba inao wajibu wa kuendelea kuwasaidia wananchi na kuchapa kazi kwa bidii, uaminifu na kwa moyo wote, ili pia kuipa kasi Serikali katika kuhakikisha inatimiza malengo yake, yakiwemo ya utoaji wa elimu bora.

Aidha, Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika zoezi la Kitaifa la Kuhesabiwa (SENSA), ambalo litafanyika baadae mwaka huu nchini, likiwa na lengo la kujua idadi sahihi ya watu na makaazi, na hivyo kuiwezesha Serikali kuandaa mipango ya maendeleo kwa wote, na kwa ufanisi zaidi. 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TASAF, Bw. Laudislaus Mwamanga amesema taasisi yake itaendeleza harakati za utekelezaji wa miradi ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, ili kuhamasisha maendeleo ya jamii katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba na Tanzania kwa ujumla.
Akiwashukuru viongozi, Kamati za Usimamizi wa Miradi na wananchi mbali mbali wa Shehia za Fujoni, Mahonda, Mkataleni na shehia nyengine za jirani kwa mashirikiano na michango yao ya hali na mali iliyofanikisha miradi hiyo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Idarous Faina amesisitiza haja ya kuyatunza majengo hayo, ili kutatua changamoto zilizoikabili hapo kabla jamii inayoyazunguka, kama ilivyotarajiwa.

Uzinduzi wa Miradi hiyo, ambao ni mfululizo wa Ratiba ya Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar, umekuja kufuatia ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) uliogharimu takriban Shilingi za Tanzania Milioni 292, sambamba na asilimia kumi (10%) ya mchango wa fedha hizo kutoka kwa wananchi. 
Viongozi mbalimbali wa Serikali, siasa na jamii wamehudhuria katika hafla hiyo ambao ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dokta Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dokta Omar Dadi Shajak, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Maafisa na Watendaji kutoka TASAF Tanzania Bara na Zanzibar.

Post a Comment

0 Comments