Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar atoa maelekezo kwa wakandarasi kuepuka kasoro ambazo zinaweza kudhibitiwa mapema

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah, amesema ipo haja kwa wakandarasi wanapopewa kazi za ujenzi na Serikali kushirikiana na taasisi zilizopitisha miundombinu yao katika maeneo waliyokabidhiwa kazi.
Mhe. Hemed ameyasema hayo alipotembelea bomba la maji safi na salama lililopasuliwa na mkandarasi ambaye alikuwa akisafisha eneo linalotarajiwa kuanza kujengwa Hospitali Lumumba. 

Mhe. Hemed amesema, endapo kutakuwepo ushirikiano baina ya wakandarasi wanaojenga miradi na taasisi zilizopitisha miundombinu mbalimbali katika maeneo yanayotekelezwa miradi, kutasaidia kuondoa athari zinazoweza kujitokeza katika miundombinu iliyopita katika maeneo hayo.

Mhe. Hemed, amemtaka mkandarasi aliyepasua bomba hilo kulipa fidia ya gharama zote zilizosababishwa na uharibifu huo ili wananchi waendelee kupata huduma. 
Aidha, ameipongeza Mamlaka ya ZAWA kwa kuchukua hatua za haraka kulifanyia matengenezo bomba hilo ili huduma ipate kurejea kwa wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Maji Zanzibar, Mhandisi Dkt.Salha Mohammed Kassim amesema,baada ya kupokea taarifa za kupasuka kwa bomba hilo, hatua zilizochukuliwa na ZAWA ni kuyafunga maji hayo ili yasiendelee kuleta athari kwa wananchi pamoja na kuanza hatua za matengenezo.
Bomba la maji lililopasuka Lumumba ni la aina ya asbestos inchi 12 na linatoa maji kutoka matenki ya Saateni na kupeleka Michenzani na Kikwajuni

Matengenezo ya bomba hilo yamekamilika na huduma imesharejeshwa kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news