Malawi, Zimbabwe, Ghana wakutana na visiki AFCON2022 nchini Cameroon

NA GODFREY NNKO

MCHEZAJI wa kulipwa wa Guinea ambaye anacheza kama beki wa kushoto katika klabu ya Toulouse FC ya Ligue 2 nchini Ufaransa, Issiaga Sylla ameiwezesha timu yake ya Taifa ya Gunea kutwaa alama tatu katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2022) inayoendelea nchini Cameroon.

Ni kupitia mtanange wa aina yake baina ya Gunea na Malawi wa Kundi B uliopigwa Janauri 10,2022 katika dimba la Kouekong kwenye mji wa Bafoussam nchini Cameroon.

Bao pekee la Sylla ambalo ndilo lilikuwa la mwanzo na mwisho katika mtanange huo lilipatikana dakika ya 35 ya kipindi cha kwanza baada ya fowadi Jose Kante kumtengenezea mazingira mazuri.

Licha ya Malawi ambao hii ni mara ya kwanza wanachuana katika michuano hiyo ya AFCON tangu mwaka 2010 nchini Angola walipata nafasi nyingi za wazi na kushindwa kuzitumia.

Udhaifu huo ulikaribia kuwaponza Malawi, baada ya Ibrahima Sory Conte na Aguibou Camara katika kipindi cha pili kutaka kuongeza mabao ingawa mlinda mlango wao Jose Keita alifanikiwa kudhibiti mashambulizi.

Senegal vs Zimbabwe

Wakati huo huo, katika mchuano wa pili ndani ya dimba hilo, winga wa Liverpool, Sadio Mane ameiwezesha timu yake ya Taifa ya Senegal kutwaa alama tatu baada ya kuiadhibu Zimbabwe kwa bao 1-0.

Bao la Mane alilifunga kipindi cha pili katika dakika za nyongeza (90+7) baada ya Wazimbabwe ambao wanatazamwa kwa jicho la karibu katika michuano hiyo kubanana na Wasenegali vilivyo.

Alifunga bao hilo kwa penalti dakika ya saba ya muda wa nyongeza baada ya beki Kelvin Madzongwe kuunawa mpira.

Aidha, kiungo Gana Gueye anayechezea Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa alipoteza nafasi nyingi za wazi katika kipindi cha kwanza licha ya fursa aliyoipata akiwa karibu na mlinda mlango wa Zimbabwe, Petros Mhari.

Kundi C

Bao la dakika ya 82 la Sofiane Boufal limeipa Morocco ushindi mwembamba dhidi ya wapinzani wao wa Kundi C Ghana katika mechi yao ya kwanza katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2022) inayoendelea nchini Cameroon.
Winga huyo wa zamani wa Southampton aliipa timu yake ya taifa ushindi huo wa alama tatu kupitia mtanange huo ambao ulipigwa katika dimba la Ahmadou Ahidjo mjini Yaoundé, Cameroon.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news