Mjadala wa Kitaifa watoa majibu kuhusu Spika ajaye

NA GODFREY NNKO

WAJUMBE katika mjadala wa Kitaifa wa saa mbili na nusu kuhusu 'Uchaguzi wa Spika wa Bunge na matarajio ya wananchi kwa Spika ajaye' wamesema kuwa, wanatarajia Watanzania watampata Spika ambaye anafahamu pamoja na kuwa mkuu wa mhimili lengo la mihimili yote mwisho wa siku ni kuwaletea maendeleo wananchi.
Kuhusu mihimili

Katiba ya nchi inatambuliwa kuwa ni sheria kuu au ya msingi inayoweka mihimili mikuu mitatu ambayo ni Dola, Bunge na Mahakama. 

Aidha, Katiba inafafanua majukumu ya kila mhimili na kutoa mgawanyo wa madaraka miongoni mwa mihimili hiyo. Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakidhi tafsiri hiyo na ina jumla ya sura 10.

Sura ya Kwanza inaeleza misingi mikuu ya Sera ya Taifa; Haki za Msingi na Wajibu wa Watanzania. Sura ya pili hadi ya sita inatoa masharti ya uanzishaji wa Serikali ambayo inajumuisha Dola, Bunge na Mahakama na kufafanua mgawanyo wa madaraka na kazi miongoni mwao.

Sura ya Saba inaeleza masharti kuhusu fedha za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sura ya Nane inaunda Mamlaka ya Serikali za mitaa, majiji, manispaa na wilaya za vijijini. 

Sura ya Tisa inatoa masharti ya kuwepo na udhibiti wa majeshi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sura ya mwisho ambayo ni Sura ya Kumi inatoa masharti mengineyo yanayohusu utaratibu wa kujiuzulu watu wanaoshika nyadhifa zilizotajwa ndani ya Katiba, pia inatoa ufafanuzi wa baadhi ya masharti yanayotumika ndani ya Katiba.
Kupitia mjadala huo wa leo Januari 22, 2022 ambao umeratibiwa na Watch Tanzania kwa kudhaminiwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kupitia mtandao wa Zoom washiriki wamesisitiza kuwa,Spika anapaswa kutambua majukumu yake na kuziweka kando hisia zake ambazo hazina tija katika maslahi ya Taifa.

Mbunge wa Jimbo la Kawe ambaye pia ni Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Dkt.Josephat Gwajima amesema, Taifa linahitaji kupata aina ya Spika ambaye anafahamu pamoja na kuwa mkuu wa mhimili, lengo la mihimili yote mwisho wa siku ni kuwaletea wananchi maendeleo.

"Hivyo, kikwazo chochote ambacho Spika atafanya akifikiria kuwa yeye ni Mkuu wa Mhimili ajue lengo ni kuwaletea Watanzania maendeleo kwa ujumla.Na Spika anatakiwa ajifunze kutofautisha hisia zake binafsi juu ya watu na kanuni,katiba na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,"amefafanua Askofu Dkt.Gwajima.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mvumi mkoani Dodoma, Mheshimiwa Livingstone Lusinde amesema kuwa,anaamini Spika ajaye anakwenda kulifanya Bunge kuwa taasisi imara zaidi.

"Aina ya Spika tunayemtarajia ataamsha morari ya Bunge katika kufanya kazi za kuisimamia Serikali na kuweza kuleta maendeleo.Tunamtarajia ni mtu mkali inapobidi, lakini mtu mwenye kueleza na kuelekeza pale inapobidi,sina mashaka kwamba Bunge linakwenda kuwa taasisi imara kabisa.Spika tunayemtarajia aliwahi kukaa kwenye kiti cha Spika bila kukosekana,"amefafanua Mheshimiwa Lusinde.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Utafiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Bernadeta Killian amesema kuwa,Spika ana kazi kubwa ikiwemo kuhakikisha jukumu la msingi la ujenzi wa demokrasia ya nchi yetu.

"Ni kwa kuimarisha kazi ya Bunge kama taasisi.Bunge ni kama daraja linalowakutanisha wananchi na Serikali kwa kupitia wawakilishi wao, kwa hiyo ili demokrasia yetu iweze kufanya kazi, hatuwezi bila Bunge,ni taasisi muhimu sana ni kama 'robot' ya demokrasia ya nchi yetu,"amefafanua Profesa Killian.

Pia amesema kuwa, anaona dalili kubwa kwamba Spika ajaye atakuwa mwanamke, "na tutaweka tena historia nyingine katika nchi yetu kwa kuwa na spika mwanamke kwa mara ya pili.Vivyo hivyo, kuna dalili kwamba hiki kipindi tunakipita kwa mafanikio, kwani mchakato umeshaanza na tunaelekea kumpata Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,"ameongeza.

Mwenyekiti wa Chama cha Upinzani cha ADC ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Afya Zanzibar, Mheshimiwa Hamad Rashid amesema kuwa,Watanzania wanatarajia kuwa na Spika ambaye atausimamia kwa weledi na ufanisi mhimili wa Bunge ili uweze kuwa matokeo bora kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo 

"Hivyo, Spika ajaye ni muhimu kuhakikisha anazingatia umoja wa Taifa na tunu za Taifa zinalindwa na hizo ni uwepo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,uwepo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wananchi wa Tanzania,"amesema Mheshimiwa Rashid.

Ameendelea kufafanua kuwa, kazi ya Spika ni kuhakikisha kwamba sheria inayopitishwa bungeni imeshirikisha pande zote mbili ili ikipita kusiwe na vikwazo.

"Ni kwa sheria hiyo kutumika upande wa pili, lenyewe (Bunge) likiachiwa linaweza kubomoa umoja wetu.Chochote kinachopitishwa pale Bungeni ni kwa maslahi ya watu wote Tanzania,kazi hiyo Spika anaweza kuifanya vizuri,"ameongeza.

Katika hatua nyingine, Askofu Dkt.Gwajima katika mjadala huo amesema kuwa, wabunge wanatakiwa kuwa na aina ya Spika ambaye anaachia uhuru wa kutosha kwa wabunge kujadili ripoti ya CAG ili waone kama bajeti waliyoipitisha ni sawasawa na Serikali inavyotumia fedha zao.

Mjadala huu unajiri ikiwa tayari mchakato wa kuwatafuta wagombea wa nafasi ya kiti cha uspika unaendelea kufanyika. Ni kiti kilichoachwa wazi na Mheshimiwa Job Ndugai aliyejiuluzu nafasi hiyo Januari 6, 2022.

Tayari Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imepitisha jina pekee la Dkt.Tulia Ackson kuwa mgombea wa kiti cha Spika. 

Januari 20, 2022 kwenye ukumbi wa White House jijini Dodoma, Katibu Mwenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka alisema Kamati Kuu ilipitisha jina moja la Dkt.Tulia Akson kati ya majina 70 ya makada wa CCM waliochukua na kurejesha fomu.

Miongoni mwa wana CCM walioshindana na Dkt.Tulia ni wabunge wa sasa, Mussa Azzan Zungu (Ilala), Dkt.Tulia Ackson (Mbeya Mjini), Luhaga Mpina (Kisesa), Stella Manyanya (Nyasa), Godwin Kunambi (Mlimba) na Joseph Musukuma (Geita Vijijini).

Aidha, walikuwapo wabunge wa zamani, Stephen Masele (Shinyanga Mjini), Athuman Mfutakamba (Igalula), Andrew Chenge (Bariadi Magharibi), Profesa Norman Sigalla (Makete), Dkt. Titus Kamani (Busega), Ezekiel Maige (Masalala) na Sophia Simba (Viti Maalum). Pia katika hatua hiyo walijitokeza makada, watumishi wa umma, viongozi wastaafu na wanafunzi.

ADC

Wakati huo huo, Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) siku ya Januari 21, 2022 kimemtangaza Maimuna Said Kassim kuwa mgombea wa nafasi ya uspika wa Bunge.

Miongoni mwa wanachama wa ADC walioshindana na Maimuna ni Innocent Siliwa. Hivyo, kwa hatua hiyo tayari waliotangazwa ni Dkt.Tulia Ackson wa CCM na wa ADC.

Baada ya kuteuliwa na chama hicho, Maimuna alikishukuru chama chake kwa kumuamini na kumpatia fursa ya kwenda kupambana kwenye nafasi hiyo.

"Kikubwa nitahakikisha Bunge letu linakuwa la kisasa na linaenda kutenda haki kuhakikisha linasimamia maslahi ya watanzania,”alisema Maimuna wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news