Msaidizi wa Rais mstaafu Dkt.Jakaya Kikwete afariki

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

OFISI Binafsi ya Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete imethibitisha kutokea kwa kifo cha Katibu wa Rais huyo mstaafu, Adam Issara kilichotokea jana jioni Jijini Dar es Salaam.
Adam Issara alifariki akiwa katika Hospitali ya Dr. Mvungi jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ambapo taratibu za msiba na maziko zitatolewa punde.

"Wakati wa uhai wake, Ndugu Adam Issara alikuwa mtu mwaminifu, muadilifu, mchapa kazi hodari na nguzo muhimu ya Ofisi Binafsi ya Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

"Kabla ya kujiunga na Ofisi Binafsi ya Rais Mstaafu mwaka 2017, Adam Issara alifanya kazi katika iliyokuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwa Afisa Dawati katika Idara ya Asia na Australia, na baadae kuwa Katibu wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kati ya mwaka 2007 na 2017.

"Ofisi Binafsi ya Rais Mstaafu na Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, na familia yake wanaungana na mjane wa Marehemu, Bi. Happy Godfrey, familia ya Marehemu Adam Issara katika kipindi hiki cha simanzi na maombolezo, Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahala pema, peponi,"imeeleza Ofisi Binafsi ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne.

Post a Comment

0 Comments