Mwalimu Makuru asema hotuba ya Rais Samia imewafungua macho Watanzania

NA FRESHA KINASA

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Mwalimu Makuru Lameck Joseph amesema hotuba aliyoitoa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO -19 imewafungua macho Watanzania juu ya umuhimu wa mikopo katika kukuza uchumi wa nchi. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Ameyasema hayo leo akiwa Mjini Musoma wakati akizungumza na DIRAMAKINI BLOG ambapo amebainisha kuwa,hotuba ya Rais Samia imeweka wazi Mipango ya Serikali kuhusu matumzi ya fedha za mikopo kuwa zinagusa maendeleo ya nchi na maisha ya Watanzania wote. 

Mwalimu Makuru amesema kuwa, hatua ya Serikali anayoiongoza Rais Samia kukopa fedha nje ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa na kwamba watanzania ndio wanufaika wakubwa wa mikopo hiyo kutokana na kuyagusa mahitaji ya maisha yao sambamba na kuliletea Taifa maendeleo mtambuka.

"Rais Samia amekuwa mkweli sana kwa kila jambo jema analotaka kufanya lazima Watanzania wafahamu. Huko nyuma wakati mwingine mikopo ilikuwa na kificho sana, na hata mikataba mbalimbali ilifanywa lakini Watanzania hawakufahamu. Lazima tujivunie kuwa na Rais ambaye anaeleza hatua anayotaka kufanya iwe ni chanjo, au jambo la kijamii, kisiasa na hata hizi fedha tulijulishwa, huyu ni kiongozi wa mfano na kuigwa sana.
"Ukweli na uwazi uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kutueleza Watanzania matumizi ya mkopo wa Shilingi Trilioni 1.3 na matumizi yake ni jambo la kipee sana na kila mtu ameona kwa macho madarasa yamejengwa. Kiongozi huyu amedhamiria kulifanya taifa letu liwe na maendeleo makubwa kwa hiyo mimi nampongeza sana kwa hatua hii muhimu na Watanzania wote ninaamini kabisa wapo pamoja naye kwa kumpa ushirikiano na kumuombea aweze kutekeleza mipango ya maendeleo kwa ufanisi zaidi," amesema Mwalimu Makuru.

Aidha, Mwalimu Makuru amesema kuwa, Watanzania wanapaswa kutembea kifua mbele bila kuogopa kwani wana kiongozi ambaye yupo pamoja nao wakati wote katika kuhakikisha kwamba, anawatumikia kikamilifu kuwaletea maendeleo na pia akasisitiza wasikubali kusikiliza maneno ya wapotoshaji wanaobeza hatua yake ya kukopa fedha nje kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo nchini.

Pia, amewaasa viongozi na wanasiasa waache propaganda za kuwahadaa wananchi kwa kutaka kumsema vibaya na kumkosanisha na wananchi kwa masilahi yao binafsi ili hali wanatambua fika kuwa fedha zinazokopwa ni kwa ajili ya manufaa ya Watanzania wote na pia kuwaweka wazi Watanzania kuwa awamu zote zilizopita zilikopa na hivyo kuwatoa hofu Watanzania kuwa sio Awamu ya Sita ndio imeanza kukopa fedha nje.

"Waliokuwa wanakosoa hatua ya Rais kukopa fedha nje hawataki taifa letu lipige hatua za kimaendeleo. Mfano wafanyabishara hukopa fedha katika taasisi za Kifedha kwa lengo la kukuza biashara zao na tumekuwa tukishuhudia wakiinuka na kupiga hatua kubwa. Iweje Taifa lisikope kufanikisha miradi ya kimaendeleo huku kukiwa na mataifa makubwa kiuchumi yanakopa kujiimarisha zaidi.?alihoji Mwalimu Makuru.

Amekishauri Chama Cha Mapinduzi kuzidi kuendelea na umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama na viongozi na pia kisikae kimya kuwajibu wale ambao wataonekana kumsema Rais kwa unafiki na kumnenea mabaya kwa wananchi ambao wanamwamini kama kiongozi wao Mkuu ambaye analiongoza Taifa lizidi kustawi katika nyanja mbalimbali za kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments