Mwenyekiti CCM Mara atoa neno Spika Ndugai kumuomba radhi Rais Samia, asisitiza mjadala ufungwe watu wachape kazi



NA FRESHA KINASA

SAA chache baada ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kujitokeza hadharani na kumuomba radhi Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samwelly Kiboye (Namba Tatu) amesema wana CCM na Watanzania wote wamsamehe kutokana na uamuzi wake wa busara na hekima aliyoonyesha kwa kuomba radhi kwa yale aliyodaiwa kuyasema hivi karibuni. 

Kiboye amesema, kilichopo kwa sasa ni wana CCM na wananchi wote kumsamehe Spika Ndugai na waungane kwa pamoja katika ujenzi wa Taifa.

Sambamba na kushirikiana kikamilifu na Rais Samia Suluhu Hassan ili azidi kuendelea kuliletea maendeleo Taifa.
Kiboye ameyasema hayo leo Januari 3, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya CCM Mkoa wa Mara yaliyopo Mjini Musoma.

"Tumsamehe mwenzetu Spika Job Ndugai kwa hatua yake ya kuomba radhi kwa kauli zake za hivi karibuni. Neno la Mungu linasema samehe saba mara sabini,ametambua yale maneno yanaweza kuleta taharuki kwa watanzania na taifa letu.

"Mtu akiomba msamaha, ametambua kosa lake hivyo naomba tumsamehe, na pia sasa tuache kumsema tena, tumsamehe tuendelee kujenga chama chetu na nchi yetu kwa umoja wetu na mshikamano wetu thabiti tulionao,"amesema Kiboye.
"Niwombe wana CCM na Watanzania wote tushirikiane kujenga nchi na chama, kuna watu waliingilia kati na kupiga kelele na wengine walipiga vigelegele kwa sasa vigelegele vyao vimeisha. Watanzania tumuunge mkono Rais kwa nguvu zote na tuwe pamoja pia na spika Ndugai,"amesema Kiboye.

Katika hatua nyingine Kiboye amezungumzia maandalizi ya Sherehe za Miaka 45 ya CCM itakayofanyika kitaifa tarehe 5 mwezi Februari 2022 mkoani Mara, ambapo amesema sherehe hiyo itakuwa kubwa kwa viongozi wa kitaifa na kimataifa kuhudhuria katika sherehe hiyo na kabla ya kufanyika shughuli za kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo itafanyika.

"Sherehe hiyo itahudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye atakuwa mgeni rasmi kila wilaya imejipanga vyema katika maadhimisho hayo. Sherehe itafanyika kwa ubora kabisa chama Mkoa kimejipanga vyema ili zifanyike kwa ubora mkubwa. 

"Miradi yote ya Serikali inayotekelezwa na ilani yakiwemo madarasa, vituo vya afya vinavyojengwa kwa fedha za UVIKO-19 itatembelewa sambamba na madaraja, barabara na maeneo mengine," amesema Kiboye.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news