Naibu Waziri Ridhiwani Kikwete atoa maelekezo yenye tija kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)

NA MUNRI SHEMWETA-WANMM

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuwa na mipango ya muda mrefu ya miradi ya ujenzi wa nyumba zake kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kukidhi mahitaji yanayoendana na ukuaji wa miji.
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dkt.Maulid Banyani (aliyesimama) akimkaribisha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete katika kikao chake cha Bodi pamoja na Menejimenti ya NHC tarehe 24 Januari 2022. (Picha zote na Munir Shemweta-WANMM). 

Ridhiwani ametoa kauli hiyo tarehe 24 Januari 2022 jijini Dar es Salaam alipokutana na Bodi pamoja na Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa kwa lengo la kupata uelewa jinsi shirika linavyofanya kazi na kupata taarifa ya miradi ya shirika.

‘’Hapa la msingi ni kuwa na 'plan' (mipango) za mbele, lazima tuzungumzie Shirika la Nyumba la Taifa ndani ya miaka 100 ijayo,’’alisema Ridhiwani.

Akitolea mfano wa mkoa wa Morogoro, Naibu Waziri Ridhiwani alisema, Shirika la NHC lazima lifikirie mipango yake kwenye mkoa huo hasa ikizingatiwa mkoa huo ni kiunganishi cha mkoa wa Dar es Salaam na Makao Makuu ya nchi Dodoma.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili Makao Makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) alipokwenda kukutana na Bodi na Menejimenti ya Shirika hilo jijini Dar es Salaam tarehe 24 Januari 2022. Aliyesimama ni Mkurugenzi wa NHC, Dkt.Maulid Banyani.

‘’Sisi tunaiangaliaje Morogoro? Plan lazima zije maana nikitaka kupunguza safari ya kwenda Dodoma ni mkoa wa Morogoro hivyo NHC tunaingaliaje Morogoro, hata kama hatuna mpango wa leo tuangalie kesho,"alisema Ridhiwani.

‘’Suala hilo ni sanjari na maeneo mengine, nimeangalia Morogoro kama eneo linalokuwa na jambo hili ni muhimu, tuangalie ‘future’ inakuaje na tunaendaje? Alisema Naibu Waziri wa Ardhi.

Aidha, alilitaka Shirika la Nyumba la Taifa kuangalia uwekezaji kwenye miradi ya nyumba za bei nafuu sambamba na miradi ya ujenzi wa nyumba inayofanyika kuzingatia mahitaji ya kila eneo kwa lengo la kupata wateja.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete akizungumza na Wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) alipokutana nao Makao Makuu ya Shirika hilo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupata uelewa wa majukumu na miradi ya shirika tarehe 24 Januari 2022.

Hata hivyo, Ridhiwani aliipongeza NHC kwa hatua yake ya kuanza kuzifanyia ukarabati nyumba zake zilizochakaa na kusema kwamba, hatua hiyo itazifanya nyumba za shirika sasa kuwa na taswira nzuri.

Shirika la Nyumba la Taifa lina nyumba 17,115 za kupangisha katika maeneo mbalimbali nchini.

‘’Pale mtaa wa Uhuru kuna jengo limetoa na kivuli, jengo ni imara, lakini mazingira yake na nawashauri wakati wa kufanya ukarabati wa nyumba zenu basi mfikirie namna wapangaji waliopo mtawapeleka wapi wakati wa ukarabati,’’alielekeza Mheshimiwa Ridhiwani.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akifuatilia uwasilishwaji taarifa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwenye kikao chake na Bodi na Menejimenti ya Shirika hilo alipokutana nao Makao Makuu ya Shirika hilo jijini Dar es Salaam kupata uelewa wa majukumu na miradi ya shirika tarehe 24 Januari 2022.

Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Dkt.Maulid Banyani alimueleza Naibu Waziri kuwa, Shirika lake limejiwekea mpango wa miaka mitano wa kufanya ukarabati wa nyumba zake zilizochakaa na kubainisha kuwa, katika mwaka huu wa fedha 2021/2022 shirika hilo limetenga takriban shilingi bilioni 8 kwa ajili ya ukarabaiti wa nyumba hizo.

‘’Mheshimiwa Naibu Waziri baadhi ya nyumba za shirika zimechakaa na nyingi ni zile zilizotwaliwa miaka ya 1971 na plan ya matengenezo ni ya miaka mitano na kwa mwaka huu wa fedha tumetenga takribani bilioni 8. Jumla ya bilioni 52 zitatumuka kutekeleza mpango huo,"alisema.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) alipokutana nao Makao Makuu ya Shirika hilo jijini Dar es Salaam kupata uelewa wa majukumu na miradi ya shirika tarehe 24 Januari 2022.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete alitembelea mradi wa Shirika la Nyumba la Taifa wa Morocco Square unaohusisha viwanja vilivyopo barabara ya Mwai Kibaki na mtaa wa Ursino, Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete akiangalia mandhari ya jiji la Dar es Salaam akiwa kwenye moja ya jengo la miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa ya Morocco Square alipokwenda kukagua mradi huo tarehe 24 Januari 2022.

Ridhiwani ameridhishwa na maendeleo ya mradi huo alioueleza kuwa, una sifa nyingi sambamba na sura ya kipekee kwa sababu una ‘junction’ kubwa kwenye makutano. 
 
Alisisitiza kuwa, ameridhika na mazingira aliyoyakuta kwenye mradi huo wa Morocco Square na kuahidi kumpa ushirikiano Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dkt.Maulid Banyani.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete akiangalia sehemu ya bwawa la kuogelea kwenye mradi wa Shirika la Nyumba la Taifa wa Morocco Square jijini Dar es Salaam alipokwenda kukagua mradi huo tarehe 24 Januari 2022.

Kwa mujibu wa Dkt.Banyani mradi huo wa Morocco Square unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 137.5 umefikia asilimia 90 na kutarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news