Rais Dkt.Mwinyi adhamiria kuboresha Sekta ya Mawasiliano nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza matumaini yake makubwa katika kuimarisha ushirikiano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kukuza sekta ya mawasiliano.

Mheshimiwa Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Moses Nnauye Ikulu jijini Zanzibar akiwa amefuatana na ujumbe wake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania ukiongozwa na Waziri wa wizara hiyo, Mhe.Nape Moses Mnauye kulia kwa Rais na kushoto kwa Rais ni Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi,Mhandisi Zena Ahmed Said. (Picha na Ikulu).

Katika mazungumzo hayo Rais Dkt. Mwinyi alimpongeza Waziri Nape kwa kupata wadhifa huo na kuahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano uliopo ili kuweza kufanikisha kuwapatia wananchi wote mawasiliano sambamba na kushirikiana katika nyanja nyingine muhimu zilizokuwemo katika wizara hiyo ili pande mbili hizo ziweze kwenda kwa pamoja katika maendeleo.

Alieleza kwamba kuwepo kwa mradi wa kusambaza minara ambao itawekwa minara ipatayo 42 katika Shehia zipatazo 38 Unguja na Pemba kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kuwapatia mawasiliano bora wananchi, mradi utakao simamiwa na Mfuko wa Mawasilano kwa wote (UCSAF) ulioanzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Moses Nnauye kwa upande wake aliahidi kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kueleza kwamba ushirikiano uliopo kati ya Mfuko wa Mawasiliano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mzuri. 

Alisema kwamba, mradi huo utafanyika kwa kiasi ya Shilingi Bilioni 6.9, ambao pia, umezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na maelekezo aliyoyatoa katika ziara zake alizozifanya katika mikoa ya Zanzibar ambapo iligundulika kwamba kuna baadhi ya maeneo katika visiwa vya Unguja na Pemba hawapati mawasiliano bora ya simu.

Sambamba na hayo, Waziri Nape alimuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kwamba Wizara anayoiongoza itatoa ushirikiano ya kutosha hasa kwa kutambua kwamba ni Wizara ya Muungano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news