Rais Dkt.Mwinyi ajumuika na wananchi katika sala ya kumuombea marehemu Mzee Machano Mwadini Omar

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo amejumuika pamoja na wanafamilia, wananchi pamoja na viongozi mbalimbali katika sala na dua ya kumuombea marehemu Mzee Machano Mwadini Omar, Sheha wa Shehia ya Kwahani, huko kijijini kwao Chaani Masingini, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ya kumuombea marehemu Machano Mwadini Omar baada ya kutoa mkono wa pole kwa familia ya marehemu alipofika kijiji kwao Chaani Masingini Mkoa wa Kaskazini Unguja.(Picha na Ikulu).

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipa pole familia ya marehemu Mzee Machano Mwadini Omar mara baada ya kufika kijijini hapo, na kuisihi familia kuwa na subira katika kipindi hiki cha msiba pamoja na kuendelea kumuombea dua marehemu.

Alhaj Dkt. Mwinyi alimuelezea marehemu jinsi alivyomfahamu na jinsi alivyokuwa nae karibu katika kazi wakati akiwa Mbunge wa Jimbo la Kwahani tokea marehemu nae akiwa Diwani na hatimaye kuwa Sheha wa Shehia ya Kwahani, nafasi ambayo alikuwa nayo hadi mauti yanamfika.

Akitoa pole, Alhaj Dkt. Mwinyi alimuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Mzee Mwadini Omar mahali pema peponi, Amin.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kutoa mkono wa pole kwa Familia ya Marehemu Machano Mwadini Omar aliyekuwa Sheha wa Kwahani, alipofika Kijiji kwao Chaani Masingini Mkoa wa Kaskazini Unguja.(Picha na Ikulu).

Mapema Alhaj Dkt. Mwinyi aliungana na waumini wa dini ya Kiislamu katika sala ya Ijumaa katika msikiti wa Mwembenjugu (Masjid Iman), ambapo mara baada ya sala hiyo alitoa salamu kwa waumini na kuwasihi kuitumia misikiti kwa masuala mbalimbali ya kijamii.

Alhaj Dkt. Mwinyi alisema kuwa, misikiti isitumiwe kwa kusali pekee bali itumike pia kwa masuala ya kijamii ikiwa ni pamoja na kuwasaidia yatima, wajane, wasiojiweza na kutoa elimu juu ya matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kupambana na udhalilishaji.

Aliwasihi waumini kujikinga na mambo mbalimbali katika jamii pamoja na kujikinga katika afya zao ikiwa ni pamoja na kuwa na mfumo mzuri wa kula kama alivyofundisha Mtume Muhammad (S.A.W), kufanya mazoezi huku akisisitiza haja ya kujikinga na maradhi ya UVIKO-19, majanga ambayo mbali ya kuathiri afya pia yameathiri uchumi kwa kiasi kikubwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt.Hussein Akli Mwinyi akijumuika na wananchi katika kusoma dua na kumuombea Marehemu Mchano Mawadi Omar aliyekuwa Sheha wa Kwahani, maziko yaliofanyika Kijiji kwao Chaani Masingini Mkoa wa Kaskazini Unguja.(Picha na Ikulu).

Sambamba na hayo, Alhaj Dkt. Mwinyi alikubali ombi la uongozi wa msikiti huo la kusaidia ujenzi wa msikiti wao ambao hivi sasa haukidhi haja kutokana na kuwa mdogo, ombi ambalo Alhaj Dkt. Mwinyi amelipokea na kuahidi kulifanyia kazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news