Rais Dkt.Mwinyi atoa maagizo kwa Mabalozi kuhusu Sera ya Diplomasia ya Uchumi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameeleza haja kwa Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nje ya nchi walioteuliwa hivi karibuni kuipa kipaumbele Sera ya Diplomasia ya Uchumi katika nchi wanazokwenda kufanya kazi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyeiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akisisitiza jambo alipozungumza na Mabalozi walioteuliwa kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa kuagana nao na kupata maagizo katika utekelezaji wa kazi zao. (Picha na Ikulu).

Rais Dkt.Mwinyi alieleza hayo leo Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walioteuliwa hivi karibuni kwenda kuiwakilisha Tanzania nje ya nchi.

Miongoni mwa Mabalozi hao ni Balozi Perera Ame Silima anayekwenda Jamhuri ya visiwa vya Comoro, Balozi Said Shaib Mussa, anayekwenda nchini Kuwait, Balozi Fredrick Ibrahim Kibuta anayekwenda nchini Urusi, Balozi Profesa Adelardus Kilangi anayekwenda nchini Brazil, Balozi Alex Gabriel Kalua anayekwenda nchini Israel na Balozi Said Juma Mshana anayekwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi aliwaeleza Mabalozi hao kwamba Sera ya Diplomasia ya Uchumi ndiyo iliyopewa kipaumbe hivi sasa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo, ni vyema Mabalozi hao wakaenda kuifanyia kazi Sera hiyo ili uchumi wa Tanzania uzidi kuimarika.

Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwaeleza Mabalozi hao namna Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ilivyoweka mikakati yake katika kuimarisha uchumi wake ambao Dira ya uchumi huo ni Uchumi wa Buluu.

Ameongeza kuwa, kwa upande wa Zanzibar sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta iliyopewa kipaumbele kupitia uchumi huo wa Buluu na kuwasisitiza Mabalozi hao katika kuhakikisha wanaitumia fursa hiyo kuitangaza Zanzibar kiutalii katika nchi wanazokwenda kuiwakilisha Tanzania.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwamba mbali ya sekta ya utalii pia, ni vyema kuitangaza Zanzibar katika sekta za uchumi wa Buluu ikiwemo uvuvi, mafuta na gesi asilia, uvuvi, kilimo cha mwani na bandari huku akisisitiza kwamba iwapo bahari itatumiwa vizuri maendeleo makubwa yatapatikana.

Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwamba Dira ya Uchumi wa Buluu inaweza kufanya kazi kwa nchi zote wanazokwenda kuiwakilisha Tanzania Mabalozi hao hivyo, alisisitiza haja ya kuwakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika maeneo kadhaa ya viwanda hapa nchini.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Miwnyi alisisitiza kwamba kwa upande wa nchi ya Comoro ni vyema hatua za kurejesha uhusiano na ushirikiano wa kibiashara ukafufuliwa kati ya nchi hiyo na Zanzibar.

Pia, alieleza haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano na nchi ya Brazil hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika sekta ya teknolojia hivyo, ni vyema wakawakarisha wawekezaji kutoka nchi hiyo kuja kuekeza nchini badala ya kuagiza bidhaa kadhaa kutoka nchini humo.

Pamoja na hayo, Rais Dkt.Mwinyi alieleza haja ya kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano ili kuimarisha sekta ya biashara na nchi ya Kuwait sambamba na kutafuta namna ya kuweza kupeleka bidhaa mbalimbali nchini humo zinazotoka Tanzania.

Kwa upande wa sekta ya utalii, Rais Dkt. Mwinyi alisema kwamba, Urusi ni mdau mkubwa wa utalii hapa nchini hivyo, ni vyema juhudi za makusudi zikaendelezwa kuhakikisha watalii wanakuja nchini sanjari na kuwakaribisha wawekezaji kuja kuekeza katika maeneo ya utalii.

Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa kumekuwa na biashara kubwa ya dagaa kati ya Zanzibar na wafanyabiashara kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hivyo, ni vyema taratibu na mazingira mazuri yakawekwa ili kuhakikisha wafanyabiashara hao wanapata maslahi mazuri.

Kutokana na nchi ya Israel kupata mafanikio kwenye sekta ya kilimo, Rais Dkt. Mwinyi alisisitiza haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika sekta hiyo pamoja na sekta ya ufugaji hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo imepiga hatua kiteknolojia hatua ambayo pia, itapunguza kuagiza bidhaa nyingi kutoka nje.

Nao Mabalozi hao kwa upande wao walimuhakikikishia Rais Dkt.Mwinyi kwamba maelekezo na nasaha alizowapa watazifanyia kazi na kueleza kuwa itakuwa ni Dira yao katika utekelezaji wa kazi zao wakiwa katika vituo vyao vya kazi nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Mapema, Rais Dkt. Mwinyi alikutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), ukiongozwa na Mwakilishi Mkaazi Christine Musisi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyeiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP hapa Tanzania Bibi Christin Musisi alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kujitambulisha. (Picha na Ikulu).

Katika mazungumzo hayo UNDP imekubali kutuma timu ya Wataalamu ili kushirikiana na wataalamu waliopo Serikalini, ikiwa ni hatua ya kupata njia bora ya utekelezaji wa mipango ya Maendeleo kupitia sekta mbali mbali, ikiwemo uchumi wa Buluu, kwa lengo la kupata mafanikio .
Rais wa Zanzibar na Mwenyeiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP hapa Tanzania wakati wa mazungumzo yao leo alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kujitambulish.(Picha na Ikulu). 

Aidha, wataalamu hao watapata fursa ya kupanga mikakati ya maendeleo katika kipindi cha muda mfupi na muda mrefu kitaifa na Kimataifa, sambamba na kufuatilia utekelezaji katika maeneo ya kipaumbele.

Post a Comment

0 Comments