Rais Samia amlilia mwanasiasa mkongwe, John Nchimbi aliyefariki leo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema chama kimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha mwanasiasa mkongwe nchini, John Nchimbi kilichotokea leo Januari 23, 2022.
Nchimbi amefariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.

Rais  Samia amemtaja marehemu Nchimbi kuwa enzi ya uhai wake akiwa kada ws TANU na baadaye CCM, alikuwa mstari wa mbele kukitumikia chama.

Rais Samia amesema, Nchimbi alikuwa mwanachama shupavu aliyetumia muda na maisha yake yote kukitumikia chama na Taifa kwa uaminifu na uzalendo mkubwa.

"Siku chache zijazo CCM kitatimiza miaka 45 tangu kizaliwe, Nchimbi amekuwa na mchango mkubwa, tutamkumbuka kwa uongozi wake uliotukuka, ujasiri, utiifu na aliyekitumikia chama kwa uadilifu na mapenzi makubwa. Hakuwa mtu anayekata tamaa hasa katika kufanikisha masuala muhimu yanayogusa maslahi mapana ya chama na Taifa," amesema Samia.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka amesema enzi ya uhai wake, Nchimbi amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM na miongoni mwazo ni pamoja na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) na Katibu wa CCM wa mikoa ya Kigoma, Singida na Dar es Salaam kwa nyakati tofauti na aliwahi kuwa mkufunzi wa vyuo vya chama vya Ilonga na Kivukoni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news