Rais Samia atoa maagizo mazito kwa makatibu wakuu

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewataka makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi.
Maagizo hayo ameyatoa leo Januari 21, 2022 katika kikao kazi na watendaji hao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Pia Mheshimiwa, Rais Samia amewataka makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu kufanya kazi kwa kuzingatia mipango ya Kitaifa katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2020-2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2021/22-2025/2026 na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo inabainisha vipaumbele vya Serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali za Serikali katika Kikao Kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre leo tarehe 21 Januari, 2022 Jijini Dodoma.(Picha na Ikulu).

Rais samia amewataka viongozi hao kuwa wabunifu na kutekeleza majukumu yao kwa kufuata Sheria, Kanuni na Miongozo ya Kiserikali katika kutimiza majukumu yao.

Wakati huo huo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jaffar Haniu ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu) ameeleza kuwa, Mheshimiwa Rais Samia amewasili mkoani Kilimanjaro na kupokelewa na Mkuu wa mkoa huo, Mheshimiwa Stephern Kagaigai pamoja na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali ambapo kesho Januari 22, 2022 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kilimanjaro mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) leo tarehe 21 Januari, 2022.
 
Akiwa njiani kuelekea Moshi Mjini, Mheshimiwa Rais Samia amewasalimia wananchi wa Bomang'ombe wilayani Hai na kuwapa pole kwa ukame ulioukumba mkoa huo.

Sambamba na kuwataka kudumisha amani ili Serikali iendelee kuwaletea maendeleo ambapo amewahakikishia kuwa, Serikali itatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kero ya maji, ujenzi wa vituo vya afya kama alivyofanya katika sekta ya elimu.

 

Post a Comment

0 Comments