Rais Samia atuma salamu za rambirambi kwa RC Gaguti kufuatia vifo vya watu 14 katika ajali

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti kufuatia vifo vya watu 14 waliofariki dunia katika ajali ya barabarani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Ni ajali iliyotokea Januari 2, 2022 saa 2:15 usiku katika Kijiji cha Lidumbe wilayani Newala Mkoa wa Mtwara.

Hayo ni mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jaffar Haniu ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu leo Januari 3, 2022.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara ACP Mark Njera amesema, chanzo cha ajali hiyo iliyotokea katika baranara ya Uchumi Mtwara-Tandahimba-Newala-Masasi ni mwendokasi wa dereva wa gari aina ya Scania.

Imeeleza kuwa, dereva alishindwa kulimudu gari hilo na kwenda kuwagonga watu hao, hali iliyopelekea vifo hivyo na kujeruhi watu wengine 22.

"Mheshimiwa Rais Samia amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Gaguti kufikisha salamu zake za pole kwa wafiwa wote,ndugu, jamaa, marafiki na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

"Mheshimiwa Rais pia amevitaka vyombo vyote vinavyosimamia usalama wa barabarani kuongeza juhudi za kudhibiti ajali hasa katika kipindi hiki cha mwanza wa mwaka, na pia amewaaswa madereva kufuata na kuzingatia sheria za usalama barabarani,"imefafanua taarifa hiyo ya Ikulu.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mheshimiwa Rais Samia amewaombea kwa Mwenyenzi Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema peponi. Amina 

Post a Comment

0 Comments