Serikali ya Awamu ya Nane Zanzibar yadhamiria kuboresha miundombinu, kuinua viwango na ubora wa elimu nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema ufunguzi wa madarasa katika Shule (Skuli) ya Msingi Sebleni ni kielelezo cha dhamira ya Serikali katika kukabiliana na changamoto ya miundombinu inayozikabili shule mbalimbali hapa nchini.

Dkt. Mwinyi amesema hayo katika hafla ya ufunguzi wa madarasa sita ya Shule ya Msingi Sebleni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Kwahani, Mhe.Ahmada Yahya Abdulwakil akitoa maelezo ya moja kati ya madarasa sita mapya ya shule hiyo yaliojengwa na Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani, baada ya kuyafungua leo Januari 7, 2022, ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Amesema, ujenzi wa madarasa hayo uliofanyika kwa ushirikiano kati ya Serikali, viongozi wa jimbo na wananchi ni miongoni mwa juhudi za kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazokabili shule hapa nchini.

Amesema, lengo la Serikali ni kuhakikisha watoto wote nchini kuanzia mjini na vijijini wanatumia haki yao ya kupata elimu katika mazingira bora.

Pia ametumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi na walezi kusimamia na kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao ili kuhakikisha wanatumia vyema fursa ya kupata elimu.

Dkt. Mwinyi amesema, ana imani ujenzi wa madarasa hayo utapunguza tatizo la msongamano wa wananfunzi katika madarasa na kuwapatia mazingira bora ya kujifunzia.

Ameeleza kuwa, ongezeko la idadi ya watu nchini sambamba na kukuwa kwa makaazi, kumeongeza mahitaji ya majengo ya shule pamoja na mahitaji zaidi ya madarasa, hivyo kuilazimu Serikali kwa kushirikiana na wananchi na viongozi wa Jimbo la Kwahani kujenga shule za Amani na Sebleni ambazo kabla hazikuwepo.

Amesema, katika kipindi cha miaka 58, Serikali imefanya juhudi kubwa ya kuongeza idadi ya shule ili kutoa fursa kwa wanafunzi wengi zaidi mjini na vijijini ili kupata haki yao ya msingi ya elimu.

Akizungumzia historia ya Sekta ya Elimu hapa nchini, Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa,kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Zanzibar ilikuwa na jumla ya shule 69 pekee katika ngazi mbalimbali na kubainisha kuwa shule mbili zilikuwa za ngazi ya maandalizi zilizoandikisha wanafunzi 60, shule 62 za msingi pamoja na shule tano za sekondari au za wananchi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiondoa kitamba kuashiria kuweka jiwe la msingi la ufunguzi wa madarasa sita ya Shule ya Msingi ya Sebleni Wilaya ya Mjini Unguja akiwa na Mbunge wa Jimbo la Kwahani Zanzibar, Mhe. Ahmada Yahya Abdulwakil,Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kingozi, Mhandisi Zena Ahmed Said na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mhe. Idrisa Mustafa Kitwana na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe.Simai Mohammed Said, ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiondoa kitamba kuashiria kuweka Jiwe la Msingi la Ufunguzi wa Madarasa Sita ya Shule ya Msingi ya Sebleni Wilaya ya Mjini Unguja akiwa na Mbunge wa Jimbo la Kwahani Zanzibar, Mhe. Ahmada Yahya Abdulwakil, ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na kulia kwa Mbunge  ni Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi,Mhandisi Zena Ahmed Said.(Picha na Ikulu).

Amesema hadi kufikia Desemba mwaka 2021, Zanzibar ilikuwa na shule za maandalizi 774, shule za msingi 545 pamoja na shule  za sekondari 302 zikiwa na jumla ya wanafunzi 552,328; ikilinganishwa na wanafunzi 25,432 waliokuwepo kabla ya Mapinduzi ya 1964. 

Amesema, katika mazingira ya namna hiyo, ni dhahiri kuwa mahitaji katika utoaji wa elimu yataongezeka, na hivyo akabainisha dhamira ya serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya miundombinu, uhaba wa walimu, vitabu na ukosefu wa madawati.

Ameeleza kuwa, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) pamoja na Taasisi ya Education Above All ya kutoka nchini Qatar imesaini mkataba wa mradi unaogharimu Dola za Kimarekani Milioni tatu, ukiwa na lengo la kusaidia kuwarejesha shule watoto wenye umri kati ya miaka 7-14 walio nje ya shule rasmi.

Aidha, amesema Serikali itaendeleza kuunga mkono juhudi zinazoanzishwa na viongozi na wananchi za ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya elimu ili kufikia dhamira hiyo ya Serikali.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikata utepe kuashiria kuyafungua madarasa sita mapya ya Shule ya Msingi ya Sebleni Wilaya ya Mjini Unguja na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,Mhe.Simai Mohammed Said, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sebleni na Mwakilishi ya Jimbo la Kwahani,  Mhe.Yahaya Rashid Abdalla na kulia kwa Rais ni Mbunge wa Jimbo la Kwahani, Mhe. Ahmada Yahya Abdulwakil,Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe.Idrisa Mistafa Kitwana na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said.(Picha na Ikulu).

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali kupitia Fedha za Mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) imedhamiria kutumia sehemu ya fedha hizo kwa ajili kupunguza changamoto za upungufu wa madarasa, kwa kujenga madarasa mapya 1,131, yakiwemo yale yalioanzishwa kwa nguvu za wananchi pamoja na kujenga madarasa mengine mapya.

Amesema Serikali itazifanyia ukarabati shule za msingi na sekondari na kujenga vyoo 1963 katika shule mbalimbali Unguja na Pemba, sambamba na kujenga nyumba kumi za walimu katika visiwa vidogo vidogo, pamoja na kununua madawati 8,000 kwa ajili ya wanafunzi 24,000 wa shule za msingi.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali,Simai Mohamed Said, ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kusema pamoja na kupitia changamoto ya Kilimwengu ya kuwepo kwa ugonjwa wa Uviko-19, Serikali ilifanikiwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wote wa sekta ya elimu, ambapo asilimia 20 ya fedha za bajeti huelekezwa katika sekta hiyo.

Amesema, maendeleo makubwa yanayoonekana kupitia sekta hiyo yanatokana na umoja na amani iliyopo hapa nchini.

Aidha, Mbunge wa Jimbo la Kwahani kupitia CCM, Ahmada Yahya Abdul-wakil (Shaa) amesema, madarasa yaliofunguliwa ni juhudi na maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambapo alikuwa Mbunge wa jimbo hilo katika kipindi cha mwaka 2015-2020.

Alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha jengo la ghorofa shuleni hapo ikiwa ni hatua ya kupanua wigo kwa wanafunzi wengi zaidi kusoma na kuondokana na changamoto ya uhaba wa madarasa unaoikabili Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwapungua mkono wananchi wa Jimbo la Kwahani Zanzibar alipowasili katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Sebleni.(Picha na Ikulu) .

Vile vile, Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani, Yahya Rashid Abdalla aliishukuru Serikali, viongozi na wananchi wote waliochangia na kufanikisha ujenzi huo, akibainisha hatua hiyo inadhihirisha matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964.

Rashid amewataka wananchi wa jimbo hilo kujiandaa na kushiriki kikamilifu katika uandikishaji wa zoezi la Sensa, pale wakati utakapowadia ili kupata takwimu sahihi na kuchochea maendeleo.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Mwinyi kwa juhudi zake za kuendelea n ujenzi wa majengo ya madarasa.

Aidha, risala ya uongozi wa jimbo hilo ilibainisha ujenzi wa madarasa hayo sita katika Shule ya Msingi Sebleni, uliotokana na wazo la Rais Dkt. Mwinyi, umegharimu shilingi Milioni 158 zinatokana na michango ya Serikali, viongozi wa jimbo pamoja na nguvu za wananchi.

Post a Comment

0 Comments