Simba SC yaondoka na milioni 25/- , Kombe la Mapinduzi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WEKUNDU wa Msimbazi, Simba SC wametwaa Kombe la Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na kitita cha Shilingi milioni 25 baada ya kuwachapa Azam FC bao 1-0.
Mtanange huo ambao umepigwa leo Januari 13,2022 katika dimba la Amaan jijini Zanzibar, mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi. 
Azam ambao ni washindi wa pili wamevuta mkwanja wa zaidi ya milioni 10 baada ya maboresho makubwa katika kombe hilo mwaka huu.

Dakika 90 zilikamilika kwa ubao kusoma Azam FC 0-1 Simba na mfungaji ni Meddie Kagere aliyefunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti.
Aidha,Tepsi Evans wa Azam FC amepewa zawadi ya kuwa mchezaji bora muungwana huku Henock Inonga wa Simba akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo.
Hili linakuwa taji la nne kwa Simba huku Azam FC ikiwa imetwaa mataji matano na ni mabingwa wa kihistoria wa Kombe la Mapinduzi.

Mbali na Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi aliyewaongoza maelfu ya wananchi kushuhudia fainali za Kombe la Mapinduzi, pia mechi hiyo imehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo.

Post a Comment

0 Comments