TARURA yaendelea kufungua barabara kwa kasi wilayani Mafia

NA GEOFREY A.KAZAULA-TARURA 

WAKALA wa Barabara za Viijini na Mijini (TARURA) umeendelea kufungua barabara ili kuwezesha wananchi kufika kusiko fikika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia mkoani Pwani. 

Meneja wa TARURA Wilaya ya Mafia, Mhandisi Francis Mugisha ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2021/22 Wilaya ya Mafia imetengewa bajeti ya Shilingi 765,580,000 kutoka Mfuko wa Barabara kwa ajili ya matengenezo ya barabara, fedha za miradi ya maendeleo Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja na Shilingi Bilioni 1 fedha zilizotokana na tozo mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa barabara. 
Muonekano wa sehemu ya Barabara ya Kichangachui-Hutchery yenye urefu wa kilomita moja inayojengwa kwa kiwango cha lami katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia mkoani Pwani. Kukamilika kwa ujenzi wa barabara hii kutachochea ukuaji wa uchumi kupitia watalii. (Picha na TARURA).

Mhandisi Mugisha amesema kuwa, moja ya kazi zinazoendelea katika Wlaya ya Mafia ni pamoja na kuiongezea upana barabara ya Ndagoni-Kitimondo yenye urefu wa Kilomita 10 na kuipandisha hadhi kutoka kiwango cha udongo kwenda kiwango cha changarawe ili kuwezesha wakulima kusafirisha mazao yao hadi sokoni. 

‘‘Wananchi wameridhia kuondoa mazao yao bila fidia ili kuweza kuipandisha hadhi barabara hii ambayo ni tegemeo kwao kwa ajili ya kusafirisha mazao kufika sokoni,” amesema Mhandisi Mugisha. 

Naye Mkazi wa Mafia, Bw. Khamis Habibu ameeleza kuwa, lengo la wananchi kukubali kuondoa mazao yao ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo ni kumaliza kilio cha muda mrefu cha ukosefu wa barabara huku akiipongeza Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hiyo na kuwatengea fedha.
Muonekano wa sehemu ya Barabara ya Ndagoni-Kitomondo yenye urefu wa Km 10 kwa kiwango cha changarawe katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, mkoani Pwani. Ufunguzi wa barabara hii utawasaidia wananchi katika kusafirisha mazao yao kwa urahisi. (Picha na TARURA).

‘‘Hapa ni kisiwani na kilio cha barabara kimekuwa cha muda mrefu lakini sasa serikali imelitambua hilo na hivyo tumeridhia mazao yetu yaondolewe maana maendeleo hayawezekeni bila barabara,"amesema Bw.Habibu. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mhandisi Martin Ntemo ameelezea kuwa, Wilaya ya Mafia imekuwa na changamoto ya barabara kwa muda mrefu, lakini baada ya kuanzishwa kwa TARURA tayari barabara nyingi zimeanza kufunguliwa na kwamba ujenzi wa barabara ya lami Mafia mjini umeanza ambapo kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea shughuli za kiuchumi na utalii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news