THRDC yapendekeza njia bora za suluhu ya migogoro ya ardhi wilayani Ngorongoro

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umesema unaendelea kufuatilia kwa karibu mgogoro wa ardhi wilayani Ngorongoro mkoani Arusha na ushiriki wa wanachama wa THRDC na Watetezi wa Haki za Binadamu katika kutatua mgogoro huo.
Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),Onesmo Olengurumwa (kushoto) pamoja na Afisa Uchechemuzi kutoka THRDC, Bi. Nuru Maro. (Picha na THRDC).

Hayo yamebainishwa leo Januari 25, 2022 kupitia taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),Onesmo Olengurumwa.

Olengurumwa amesema kuwa, "kwa mujibu wa taarifa tulizozipokea kuanzia tarehe 21 Januari 2022, Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Arusha ilionyesha nia ya kuchukua kilomita za mraba 1,500 kutoka ardhi za vijiji vya Loliondo wilayani Ngorongoro kwa ajili ya matumizi pekee ya uhifadhi na uwekezaji. 

"Mpango huo wa Serikali uliwekwa wazi tarehe 11 Januari 2022 kupitia hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha,ndugu John Mongela alipokuwa akiongea na viongozi wa vijiji, kata, wahifadhi kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na wawekezaji. 

"Katika mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Arusha alitamka wazi nia ya kutwaa eneo la kilomita za mraba 1,500 na kutengwa kwa ajili ya alichoeleza ‘maslahi ya taifa’.

"Mpango huu wa Serikali umeleta taharuki kubwa kwa wananchi wa Ngorongoro hasa kwa kuzingatia kuwa maisha ya jamii hizi yanategemea raslimali hii kwa ajili ya makazi na malisho ya mifugo yao. Wakati huo huo wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro, eneo linalosimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) wameonyesha hofu ya kuona mikakati ya kutaka kuwaondoka katika maeneo yao ikiendelea huku wakidai kutokushirikishwa kikamilifu katika mipango hii,"amefafanua Olengurumwa.

Pia amefafanua kuwa, itakumbukwa kwamba mgogoro wa ardhi wa Ngorongoro ni wa muda mrefu. Kabla ya kupata uhuru, jamii za kifugaji zilipoteza ardhi yao huko Serengeti na kuhamishiwa maeneo ya Tarafa ya Ngorongoro na Loliondo na kuahidiwa hawataondolewa tena katika maeneo yao.

Amesema, Wilaya ya Ngorongoro ina jumla za kilomita za mraba zaidi ya 14,000. Zaidi ya asilimia 75 ya eneo la Ngorongoro kwa sasa hutumika kwa shughuli za utalii na uhifadhi. 

"Kilomita za mraba 4,000 kwa sasa ndio zimebaki kwa matumizi ya makazi ya watu na shughuli za kijamii, taharuki imekuwa ikiibuka mara kwa mara katika kipindi cha miaka kadhaa toka mwaka 1992. Matukio ya kutaka kuhamisha watu yamekuwa yakifanyika mara kwa mara na huku ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ukishuhudiwa. 

"Katika mikakati hiyo baadhi ya nyumba za wananchi zilichomwa moto, watu kupoteza maisha, mifugo kufa na mali za raia kuharibika. Jambo la kushukuru na kutia faraja ni kuwa miaka yote hii viongozi wa juu wa Serikali kuanzia marais wastaafu na Mawaziri Wakuu wamekuwa wakiingilia kati migogoro hii na kuondoa hofu kwa wananchi,"amesema Olengurumwa. 

Amesema kwa sasa, "tunaamini Mheshimiwa Rais Samia akitoa nafasi ya kuwasikiliza wananchi wa Ngorongoro huenda akawa ni Rais wa kwanza kupatia ufumbuzi wa kudumu migogoro ya ardhi na uhifadhi wilayani Ngorongoro,"amesema.

Pia amebainisha kuwa, migogoro ya ardhi baina ya Wananchi na Wahifadhi au Mamlaka za Hifadhi na Wizara ya Mali Asili umeendelea kukua wilayani Ngorongoro pale mipango ya kuwahamisha wananchi wanaoshi kuzunguka maeneo ya Hifadhi ya Ngorongoro na Bonde la Kreta kuanza kuibuka ena mwezi Aprili 2021. 

Amesema, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilitoa maelekezo ya kuwaondoa baadhi ya wananchi katika eneo la hifadhi kwa madai kuwa ni wahamiaji haramu, "wengine kwa mamia kutakiwa kubomoa majengo yakiwemo shule za msingi za Serikali, vituo vya afya, vituo vya polisi, makanisa, misikiti na nyumba binafsi za wananchi. 

"Baada ya malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi zoezi hilo lilisitishwa hadi mwaka huu tena ambapo mikakati mingi na isiyoshirikishi imekuwa ikionekana kuelekeza baadhi ya watu kujiandaa kuondoka katika maeneo ya Wilaya ya Ngorongoro.

"Kwa ujumla migogoro hii ya ardhi baina ya wahifadhi, Wizara ya Mali Asili na Wananchi wa Ngorongoro inaleta picha mbaya kwa Taifa na hofu kubwa kwa wananchi wa Ngorongoro.Changamoto kubwa kwa sasa tofauti na miaka mingine migogoro hii inaibuka kipindi ambacho wananchi hawana uongozi kamili wa kuwaongoza katika kutatua changamoto hizi kama ilivyokuwa miaka nyuma. 

"Wilaya kwa sasa haina Mwenyekiti wa Halmashauri na pia Mbunge mteule bado hajaapishwa rasmi. Kwa mazigira haya ni kwamba kwa sasa wananchi wa Ngorongoro wamekuwa kama yatima, hawana mtu wa kuwasemea na hawana viongozi rasmi wa kupeleka malalamiko yao rasmi kwa viongozi wa juu kwa ajili ya mazunguzo na kupatiwa ufumbuzi wa kudumu,"amefafanua Olengurumwa.

Ushiriki 

Olengurumwa amesema, katika kuhakikisha kuwa mgogoro wa ardhi wa Ngorongoro unapatiwa ufumbuzi wa kudumu, Watetezi wa Haki za Binadamu/Asasi za Kiraia wamekuwa na mchango mkubwa sana hasa katika miaka ya nyuma.

"Mchango wao umekuwa mkubwa kuanzia katika kusaidia wananchi kupata msaada wa kisheria katika mgogoro huu, kuanzisha mazungumzo kati ya idara za Serikali, Bunge na wananchi wa Ngorongoro na hata kuhabarisha jamii na vyombo husika kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa kwa wananchi, wakati mwingine kutokana na shughuli za mwekezaji katika maeneo ya wananchi.

"THRDC inawapongeza baadhi ya wanachama wake ambao hadi sasa bado wako karibu na wananchi na kuwasaidia zaidi kujua njia sahihi za kulinda haki zao na pia njia za kutumia kuwasilisha malalamiko yao kwa viongozi wa nchi.  

"Pia tunawapongeza viongozi wa vyama ikiwemo CCM Wilaya ya Ngorongoro kwa kuwa karibu na wananchi kipindi hiki, kwa kuwa kiunganishi kati ya wananchi na Serikali. Pamoja na hayo THRDC inasikitishwa na ushiriki mdogo wa mashirika ya haki za binadamu hapa nchini pamoja na mashirika yanayotetea haki za wafugaji katika mgogoro huu wa sasa tofauti na miaka ya nyuma. 

Amesema, kwa ujumla hali ya utetezi wa haki za binadamu wilayani Ngorogooro kwa sasa inazidi kurudi nyuma na kufanya haki za wananchi kuwa katika hatari ya kupotea na kukiukwa zaidi.

Hali ya Watetezi wa Haki za Binadamu/AZAKI

Amesema kuwa, ni ukweli usiopingika kuwa watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wanasheria ambao wamekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wananchi wa Ngororngoro wamekuwa katika wakati mgumu miaka yote. 

Olengurumwa amesema, miaka ya nyuma wapo waliowahi kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kughushi.  

"Wengine wamewahi kutumiwa na kufunguliwa mashataka ya kughushi kwa kutuhumiwa kwa kosa la ujasusi (espionage) pamoja na makosa ya uchochezi. 

"Pamoja na vitisho vyote hivi bado watetezi wa haki za binadamu na haki za wafugaji Arusha na Ngorongoro waliendelea kuwa karibu na wananchi.Aidha, tumesikitishwa na hali inayoendelea kwa sasa ambapo mgogoro huu wa sasa unaonekana kukosa ukaribu wa mashirka ya haki za binadmu, vyombo vya habari vya ndani pamoja na wadau wa maendeleo. 

"Pia tunasikitishwa zaidi kuona viongozi wa juu wa Serikali wamekua kimya kufanya jitihada za kuwasikiliza wananchi wa Ngorongoro na hivyo kufanya wanachi hao waishi maisha ya hofu muda wote huu,"amefafanua kwa kina Olengurumwa.

Wito

Olengurumwa amesema kuwa,Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) unatoa wito kwa Serikali na idara zake kwa kuikumbusha Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kuwa inasimamia na kutekeleza kwa vitendo misingi ya haki za binadamu kama inavyotambuliwa na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeisaini na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Vyombo vya usalama vitambue kuwa haki ya kujieleza na kukusanyika inatambuliwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo wanawajibika kulinda haki hizo pale wananchi wanapokutana kujadili kuhusu namna ya kuutatua mgogoro wa ardhi Ngorongoro ili malalamiko yao yafike kwa viongozi wa juu wa nchi. 

"Wananchi wote ambao wameitwa polisi kutokana na mikutano ya wananchi waachwe wawe huru. Pia tunamuomba Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan awape nafasi na kuwasikiliza wananchi wa Ngorongoro ili kusikia hoja zao na hatimaye azifanyie kazi ili kumaliza mgogoro huu wa muda mrefu,"amesema.

Vilevile amesema, Serikali isitishe mpango wake wa kuchukua ardhi za vijiji na badala yake ikae na wananchi na kutafuta suluhu itakayokubaliwa na pande zote. 

Amesema, uhamisho wa wananchi utakapofanywa ufanywe kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi yetu na mikataba ya kimataifa.

"Tunapendekeza migogoro hii baina ya wananchi wa Wilaya Ngorongoro na wahifadhi ufanyiwe usuluishi wa kudumu. Tunapendekeza apatikane Msuluhishi ambaye hana maslahi na pande zote mbili au Msuluhishi Mkuu awe ni Mheshimiwa Rais Samia kwa kuwa yeye ana maslahi pande zote mbili (kwa wananchi ni wapiga kura na wananchi wake na pia Taasisi za Uhifadhi zipo chini yake),"amesema.

Mbali na hayo, mtandao huo umetoa wito kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kuiomba kufanya uchunguzi kuhusu malalamiko ya wananchi na kuchukua hatua stahiki ili kuzuia ukiukwaji wa haki za binadamu wilayani Ngorongoro.

Amesema, tume iendelee kuisisitiza Serikali kuhusu utekelezwaji wa maamuzi ya Mahakama yaliyotolewa miaka ya nyuma kuhusu haki za wananchi kumiliki ardhi yao. 

"Itakumbukwa kuwa mwaka 2018, katika kesi ya Kijiji cha Ololosokwan na wengine watatu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mahakama ya Afrika Mashariki iliweka zuio dhidi ya serikali ya Tanzania kutowahamisha wananchi, kutoharibu mali, kukamata au kuwasumbua wananchi katika eneo la Ngorongoro hadi maamuzi ya mahakama yatakapotolewa.

Pia mtandao huo umetoa wito kwa Watetezi wa Haki za Binadamu/Asasi za Kiraia na Vyombo vya habari na wale wenye majukumu ya kutetea haki za wafugaji waendelee kutetea haki za wananchi huko Ngorongoro na maeneo mengine ya nchi bila hofu kwa kufuata taratibu za kisheria kwa kuwa haya ni majukumu yao kikatiba na kisheria.

"Wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania waliopo Ngorongoro na Arusha wanaombwa kuendelea kufuatilia kwa ukaribu suala hili la mgogoro wa ardhi Ngorongoro na kuripoti changamoto zote zinazotokea na pia kufanya jitihada za kuwakutanisha wananchi na viongozi wa nchi kwa ajili ya mazungumzo kama walivyokuwa wanafanya miaka yote.

"Vyombo vya habari vifuatilie kwa ukaribu maendeleo ya hali ya haki za binadamu na utatuzi wa mgogoro wa ardhi Ngorongoro na kuripoti taarifa hizi bila upendeleo wowote na kufuata misingi ya taaluma yao. Washirika kimataifa na wadau wa maendeleo wanaombwa kuendelea kuwasaidia Watetezi wa Haki za Binadamu na Serikali kutafuta njia bora na ya kudumu ya kutatua migogoro hii kwa maslahi ya pande zote mbili zinazovutana,"amesema.

Pia Olengurumwa amesema, wanapaswa kuendelea kuhimiza majadiliano kati ya Serikali na wananchi ili mgogoro huu ufikie suluhu ya kudumu kama walivyokuwa wanafanya miaka ya nyuma.

"Wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro wanaombwa kuendelea kutumia haki yao ya kikatiba ya kutoa maoni yao kwa serikali ili yaweze kufanyiwa kazi bila hofu na kufuata sheria za nchi.

"Kuendelea kushirikiana na Watetezi wa Haki za Binadamu na Idara za Serikali katika kutatua changamoto zilizopo na hatimaye kupata suluhu ya kudumu. Pia kuwa tayari kukaa mezani kujadili suluhu ya kudumu kwa manufaa ya pande zote mbili, yaani haki za wananchi pamoja na shughuli za uhifadhi kwa maslahi ya Taifa,"amefafanua kwa kina Olengurumwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news