TPDC yaweka wazi tija na ufafanuzi kuhusu Mshauri Elekezi mradi wa LNG

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetoa ufafanuzi wa kina kuhusu upatikanaji wa Mshauri Elekezi (Transaction Advisor) wa Serikali katika Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (Liquefied Natural Gas (LNG Project).

Ni kupitia taarifa iliyotolewa Januari 26, 2022 na Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Januari 25, 2022, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Baker Botts (UK) LLP walisaini Mkataba wa Huduma ya Ushauri wa Kitaalam na kampuni hiyo ili kushirikiana na Serikali katika majadiliano ya kutekeleza Mradi wa LNG.

"Mchakato wa kumpata Mshauri Elekezi ulianza tarehe 12 Aprili 2018 ambapo TPDC ilitoa tangazo katika magazeti na tovuti mbalimbali kwa ajili ya kualika kampuni mbalimbali kuonesha nia ya kutekelea jukumu hilo kwa Serikali.

"Tangazo hilo lilichapishwa katika Gazeti la Dailynews la tarehe 12 Aprili 2018 pamoja na kuwekwa katika tovuti za TPDC, UNDP na AfDB. Hadi kufikia tarehe 4 Mei 2018, kampuni 64 ziliwasilisha nia ya kushiriki katika zabuni tajwa,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo kutoka TPDC imebainisha kuwa, tathimini ya maombi yote ilifanyika kwa mujibu wa Sheria za Manunuzi ya Mwaka 2011 ambapo kampuni tatu kati ya 64 zilifanikiwa kutimiza vigezo vyote vilivyotumika katika tathimini na hivyo kuendelea na hatua zinazofuata, amabyo ilihusisha ufunguzi wa mapendekezo ya kifedha (financial proposal).

"Hata hivyo, mchakato wa zabuni ulisimama kutokana na kusimamishwa kwa majadiliano baina ya Serikali na wawekezaji.

"Mwezi Novemba 2021, Serikali na wawekezaji walikubaliana kuendeleza majadiliano, Hivyo, TPDC ilihuisha mchakato wa kumpata Mshauri Elekezi baada ya kushauriana na taasisi mbalimbali zinazosimamia manunuzi ya umma na mikataba. Mchakato huu ulikamilika na kupelekea TPDC na Mzabuni aliyeshinda kusaini Mkataba tarehe 25 Januari, 2022.
"Ikumbukwe kuwa, Mradi wa LNG, ni mradi mkubwa na wa kwanza kutekelezwa hapa nchini. Mradi huu unahusisha kuvuna gesi asilia kutoka kwenye kina kirefu cha bahari, takribani kilomita 200 mpaka ufukwe wa Bahari ya Hindi katika eneo la Likong'o, Lindi kwa ajili ya kuichakata na kuisindika ili kuisafirisha kwenye masoko ya Kimataifa na gesi nyingine kutumika kwa ajili ya mahitaji ya ndani na ya kikanda,"imeeleza.

Kwa mujibu wa TPDC, mradi huo unatarajiwa kuwa na gharama ya takribani shilingi trilioni 70. "Kutokana na ukubwa na upekee wa mradi huu, Serikali iliona umuhimu wa kushirikiana na Mshauri Elekezi mwenye uzoefu wa utekelezaji wa miradi ya aina hii duniani ili kushauri kuhusu masuala ya kiufundi, kiuchumi, kifedha na kisheria.

"Serikali ina lengo la kumtumia Mshauri Elekezi kwa ajili ya kupata ushauri stahiki hususani katika masuala ya teknolojia, kifedha na masoko ya Kimataifa ili kuuza gesi iliyogundulika katika misingi ya ushindani na kulinda maslahi ya Taifa,"imefafanua taarifa hiyo.

Pia TPDC wamefafanua kuwa, Kampuni ya Baker Botts (UK) LLP ni moja ya kampuni kubwa duniani yenye uzoefu wa Kimataifa wa kutoa ushauri wa kitaalam kwenye miradi ya aina hiyo.

"Kampuni itashirikiana na kampuni nyingine za Kimataifa zenye ubobezi wa masuala ya teknolojia, kifedha na masoko.

"Vilevile, kampuni hiyo itafanya kazi na Kampuni ya Kitanzania ya Apex Attorneys Advocates. Pia kampuni hiyo itatoa mafunzo kwa Watanzania katika mada mbalimbali kuhusu mradi ili kuwajengea uwezo wakati wa utekelezaji wa mradi,"imebainisha kwa kina taarifa kutoka Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano TPDC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news