TRA yavunja rekodi makusanyo ya kodi kipindi cha nusu mwaka

NA BWANKU M BWANKU

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema makusanyo ya kodi kwa kipindi cha nusu mwaka 2021/22 na kwa Mwezi Disemba 2021 yameendelea kuimarika zaidi ikilinganishwa na huko nyuma.

Kwa mujibu wa taarifa ya TRA iliyotolewa Januari Mosi,2021 inasema katika kipindi cha nusu mwaka 2021/22 kilichoanza Mwezi Julai 2021 hadi Disemba 2021, Mamlaka hiyo yenye dhamana ya kukusanya mapato nchini imekusanya jumla ya kiasi cha Shilingi Trilioni 11.11 ikiwa ni sawa na asilimia 98 ya lengo ya kukusanya Shilingi Trilioni 11.302.
Makusanyo hayo ni ongezeko la Shilingi Trilioni 1.87 ikilinganishwa na kiasi cha Trilioni 9.24 kilichokusanywa katika kipindi kama hicho cha nusu mwaka kwa mwaka 2020/21.

Ongezeko la Trilioni 1.87 chini ya Serikali ya Awamu 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa nusu mwaka 2021/22 ni sawa na ongezeko la ukuaji mzuri wa ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 20.2.

Aidha, kwa mwezi Desemba 2021 pekee, TRA imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 2.51 katika lengo la kukusanya Trilioni 2.29 wakivuka lengo lao walilojiwekea na hivyo kufikia asilimia 109 ya ufanisi wa lengo lao na kuvuka zaidi ya lengo lao.

Kwa mujibu wa TRA, makusanyo haya yamevuka lengo lao kwa mwezi Desemba 2021 na ndicho kiwango kikubwa zaidi na cha juu zaidi kuwahi kukusanywa kwa mwezi mmoja tu tangu Mamlaka hiyo ianzishwe na kuanza kazi rasmi mwaka 1996.

Mamlaka ya Mapato kupitia kwa Kamishna wake Mkuu, Bw.Alphayo Kidata imesema mafanikio haya makubwa kuwahi kupatikana toka mamlaka hiyo ianze imechagizwa na kusababishwa na kuimarika kwa mahusiano mazuri zaidi baina ya mamlaka na walipakodi.

Mamlaka imemtaja Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa ndiye kichocheo kikubwa sana cha mafanikio haya makubwa na rekodi mpya kubwa ya ukusanyaji wa mapato nchini kwa miongozo yake aliyoitoa kwa mamlaka kuzingatia uadilifu, weledi na uwajibikaji unaokidhi matarajio ya walipakodi na wananchi kwa ujumla.

Pamoja na mafanikio haya makubwa katika ukusanyaji wa Mapato ambao haukuwahi kutokea toka nchi ipate Uhuru na toka Mamlaka hiyo ianzishwe, Mamlaka ya Mapato imeendelea kuwakumbusha walipakodi kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kuwaasa wote wasiozingatia sheria, kanuni na taratibu za ulipaji kodi kubadilika ili kuepuka usumbufu usio wa lazima ikiwemo kuepuka riba, adhabu, kesi na mengine yanayoweza kujitokeza ambayo si mazuri kwa pande zote.

Wakati huo huo,mamlaka kupitia kwa Bwana Kidata imewakumbusha wadau wake wote kuzingatia mambo makuu sita ambayo ni kwa wauzaji wote wa bidhaa na huduma kutoa risiti zao zote za mauzo Kielektroniki ili zikasaidie ujenzi wa Taifa, wanunuzi wote kudai risiti.

Pia walipakodi kuwasilisha ritani sahihi na kulipa kodi stahiki, wazalishaji na waingizaji wa bidhaa nchini kuzingatia matumizi sahihi ya stempu za ushuru, walipakodi kulipa madeni yao ya kodi kwa wakati pamoja na wadau wote kuhudhuria mafunzo mbalimbali yanayotolewa na TRA ili kuelewa masuala mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments