Upepo mkali waezua nyumba,madarasa

NA MWANDISHI MAALUM

UPEPO mkali umeezua paa za nyumba 21, madarasa ya shule ya msingi na ofisi moja katika kijji cha Kalengakelo, tarafa ya Mlimba, mkoani Morogoro.

Akizungumza na Habarileo jana, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hanji Godigodi alisema hakuna madhara ya kibinadamu yaliyojitokea kutokana na upepo huo.

“Ulitokea upepo mkali juzi na kuezua paa za nyumba 21, vyumba vitatu vya madarasa ya Shule ya Msingi Kalengakelo na ofisi moja, lakini hapakuwa na madhara yoyote ya kibinadamu na hapakuwa na mvua bali ni upepo mkali tu, “ alisema Godigodi.

Alisema kutokana na tukio hilo, wakazi walioathirika na upepo huo walihifadhiwa na majirani na ndugu zao na kwamba baadhi waliezeka nyumba zao na kurejea katika makazi hayo.

Kuhusu vyumba vya madarasa matatu na ofisi zilizoezuliwa, alisema ametuma timu ya waaalamu kwenda kufanya tathimini na itarejesha majibu leo ili ifanyiwe kazi mara moja.

“ Leo (jana) nimeagiza wataalamu kwenda kufanya tathimini na kesho (leo) itatoa majibu ili kuangalia gharama za kurejesha upya miundombinu ya madarasa hayo ili zitakapofunguliwa shule wanafunzi waingie madarasani kuendelea na masomo yao,” alisema Godigodi.

Kwa mujibu wa Kaimu Ofisa Tarafa ya Mlimba, Acley Mhenga, tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 12:00 jioni na kwamba baadhi ya watu walijeruhiwa baada ya kuangukiwa na matofali ya nyumba zao lakini wanaendelea vyema.

Post a Comment

0 Comments