Wafunguka kuhusu mikopo inayochukuliwa na Serikali kutekeleza miradi ya kimkakati, maendeleo ya wananchi

NA GODFREY NNKO 

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga amesema kuwa,mikopo mingi inayochukuliwa na Serikali ni ile yenye umuhimu katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na maendeleo ya wananchi.

"Hakuna uamuzi wa kuchukua mkopo ambao haufuati taratibu za sheria ya mikopo,dhamana na misaada ambayo ni Sura ya 134 ya Sheria ya nchi,mikopo mingi inayochukuliwa na Serikali ni ile yenye umuhimu katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na maendeleo ya wananchi,"amebainisha.
Prof.Luoga ameyasema hayo Januari 2,2022 kupitia mjadala wa Kitaifa juu ya umuhimu na usimamizi mzuri wa mikopo katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na maendeleo ya wananchi.
Mjadala huo uliandaliwa kwa njia ya Zoom na kuratibiwa na Watch Tanzania kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) huku wabobezi wa uchumi na wachambuzi kutoka ndani na nje ya Tanzania wakiwasilisha hoja nzito.
"Tunaposema deni la taifa ni himilivu ni uwezo wa nchi kurejesha deni lote lililokopwa ndani ya miaka 20 bila kuathiri ukuaji wa uchumi na uwezo wa serikali kugharamia shughuli za kijamii,"amesema Gavana Prof.Luoga.
 
Profesa Luoga amesema kuwa, nchi kama Tanzania inaonekana ulimwengu mzima na taasisi mbalimbali za Dunia zinaifanyia tathimini mara kwa mara.🔴 LIVE: Watch Tanzania inakuunganisha katika mjadala wa Kitaifa juu ya Umuhimu na usimamizi mzuri wa mikopo katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na maendeleo ya wananchi

"Hivyo inaonesha mwenendo wake ni mzuri na ni rahisi kukopeshwa na kurudisha kwa wakati na ukopaji wote sharti upitishwe na Bunge wakati wa kujadili mapendekezo ya bajeti ya Serikali kila mwaka,"amesema Profesa Luoga.

Kwa upande wake, Mhadhiri na Mtafiti wa Masuala ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Semboja H.Hatibu amesema kuwa,maana ya neno kukopa isiwe inatumika kupotosha kwa kuwa mikopo ina tija kubwa katika miradi ya kimkakati na maendeleo ya wananchi.

""Neno kukopa halina tafsiri kwamba unachukua kitu ambacho huna uhakika kwamba kesho utarudisha hapana, kuchukua fedha kwenye jamii nyingine na kuwekeza kwako sio tatizo ndio maana nchi kubwa sana kama Marekani, China na Japan zinachukua fedha kwenye taasisi kubwa kama World Bank (Benki ya Dunia) kwa ajili ya maendeleo ya nchi zao,"amefafanua.

Semboja ametumia mjadala huo kueleza kuwa, Tanzania inakopesheka kwa sababu ina rasilimali nyingi ambazo tutazifanyia kazi, "hivyo matokeo yake tunaweza kulipa madeni yote tunayodaiwa kwa wakati,"ameongeza Mhadhiri na Mtafiti huyo.

Naye mchambuzi wa masuala ya fedha, masoko na mitaji nchini Marekani, John Mashaka anasema kuwa,moja ya nchi ambayo ina uchumi wa kipekee ni Singapore na Tanzania inaweza kufikia hatua hiyo.

"Singapore ni moja ya nchi ambayo ni economic miracle, hii imetokana na sera bora za uchumi walizonazo, miaka ya 1967 ilikuwa ni nchi masikini sana kutokana na kutokuwa na rasilimali, lakini leo hii kipato cha wastani kwa mtu anayefanya kazi ni shilingi milioni 152,"amesema huku akiashiria kuwa, kwa mazingira yaliyopo hapa Tanzania uwezekano wa kufikia huko upo wazi.

Pia amesema, Tanzania ni kati ya nchi chache duniani ambazo zimejaliwa kuwa na rasilimali na maeneo mengi ya uwekezaji ambayo yanampa faraja mtu yeyote ambaye anataka kuwekeza mtaji wake.

"Mfano, Ethiopia sasa hivi ukiwa unafanya biashara ni ngumu sana kurudisha fedha zako nje, lakini Tanzania ni rahisi sana kuwekeza nchini na kurudisha fedha nje, hii imetokakana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini Tanzania, hivyo hilo ni jambo la kujivunia na kusonga mbele,"amesema.

Wakati huo huo,Afisa Mkuu wa Fedha katika Serikali ya Jimbo la Connectcut nchini Marekani ambaye ni Diaspora, Lunda P.Asmani amesema,mataifa mengi duniani huwa yanakopa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Asmani amesema, hata Marekani ambalo ni Taifa kubwa duniani na lenye nguvu kiuchumi pia huwa inakopa ingawa wao tofauti ipo kwenye matumizi.

"Nchi kama Marekani haina tofauti na nchi zingine kama Tanzania katika ukopaji, utofauti upo katika matumizi ya mkopo huo.

"Kwa nchi zinazoendelea (kama Tanzania) huwa zinakopa kwa ajili ya miradi endelevu au ile ya kimkakati, lakini nchi kama Marekani huwa inakopa kwa ajili ya usawa wa vizazi,"amesema Asmani.

Dkt.Joseph L.Masawe ambaye ni mtumishi wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) amesema, Serikali iliamua kujiunga na mashirika ya Kimataifa na taasisi mbalimbali za kifedha kwa kuwa, inatambua umuhimu wake katika kuiwezesha kufikia malengo yake hususani miradi mikubwa ya maendeleo.

"Tanzania tulijiunga na vyombo hivi vya World Bank (Benki ya Dunia), IMF (Shirika la Fedha la Kimataifa) na African Development Bank (Benki ya Maendeleo Afrika) mnamo Septemba 10, mwaka 1962 na tulifanya hivyo kwa sababu tulielewa maana yake,"amesema.

Naye Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Dkt.Abdula H.Makame amesema,kukopa si jambo la ajabu kabisa, kwani nchi yeyote kabla haijakopa lazima ifanye mipango yake ni kwa namna gani inakopa na kurejesha.

"Katika nchi za Afrika Mashariki nchi zote zinakopa na kulipa kwa wakati, hivyo tupuuzie maneno mitandaoni yanayosemwa kuhusu masharti na mikopo hii haina ukweli wa aina yoyote,Tanzania iliweza kuridhia Itifaki ya Umoja wa Fedha na miongoni mambo tuliyokubaliana ni kuwa na vigezo vya uwiano wa uchumi mpana,Tanzania mapaka sasa kwa jinsi Benki ya Dunia inavyosimamia uchumi wetu, sisi ndio vinara wa kukidhi vigezo,"amesema Mbunge huyo.

Wakati huo huo, Waziri wa katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa,Tanzania tunakopesheka kwa sababu tuna uwezo wa kukopa na uchumi wetu umekuwa ni imara ndio maana tumeingia kwenye uchumi wa kati na kuzidi nchi nyingi Afrika.

"Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina jukumu kubwa sana la kuhakikisha inapitia upya na kufanya kitu kinaitwa vetting na kutoa legal opinion, hivyo mkataba wowote hauwezi kusainiwa bila kupitiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.Kwenye masharti ya dhamana ni lazima masharti yawe hayagusi au kuweka rehani rasilimali yeyote muhimu ya nchi hii, ikiwa ni pamoja na madini,"amefafanua Profesa Kabudi.

 
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Moremi A.Marwa amesema kuwa,ukubwa wa soko kwenye upande wa hisa umeongezeka karibu asilimia 4.5 kutoka karibu trilioni 15.4 mpaka 15.8.

Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema kuwa, hilo ni ongezeko la karibu shilingi bilioni 500 katika kipindi cha miezi tisa, jambo ambalo linadhirisha kuwa mambo yapo vizuri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news