WAKAZI WA MBWERA-MBUCHI WAISHUKURU SERIKALI KWA UJENZI WA DARAJA

NA ERICK MWANAKULYA-TARURA

WAKAZI wa Tarafa ya Mbwera na Kata ya Mbuchi zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani wameishukuru Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ujenzi wa daraja la kudumu la chuma la Mbuchi na kutatuliwa kero yao ya muda mrefu katika eneo hilo.
Hayo yameelezwa na wananchi waliojitokeza kushuhudia ujenzi wa daraja hilo linalojengwa na wataalam kutoka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na Mhandisi Mshauri Mhandisi Ebenezer Mollel.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wameelezea kuwa eneo hilo ambalo ni mkondo wa bahari ya hindi pamoja na Mto Rufiji lilikuwa ni kero ya muda mrefu katika kusafirisha mazao yao kutokana na gharama za usafirishaji kuwa juu kwa kutumia mtumbwi ambapo gharama ya mtu kuvuka ni shilingi 300, pikipiki shilingi 2000 na wakati wa mavuno usafirishaji wa viroba shilingi 20,000.
Bw. Muhidini Mwinyihija, Mkazi wa Kijiji cha Mbwera ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja katika eneo hilo ambalo litakuwa mkombozi kwa wananchi wa Mberwa pamoja na Mbuchi kwani litawasaidia kuvuka kwa urahisi na kupunguza gharama za usafirishaji tofauti na hapo awali.

“Tunaishukuru sana Serikali ya Rais Samia kwa ujenzi wa daraja hili maana ndiyo kilikuwa kilio chetu cha muda mrefu kwasababu wananchi wote wa Mbwera mashamba yao yapo Mbuchi, tulikuwa tunatumia gharama kubwa sana katika kusafirisha mazao yetu kwa kutumia njia ya maji hasa katika kipindi cha mavuno na wakati mwingine mtumbwi kuzama na kupata hasara,”alisema Mkazi huyo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mbuchi, Mhe. Yusufu Mpili alisema wakazi wa Mbwera walishindwa kupata huduma za kijamii kwa urahisi kutokana na ukosefu wa kivuko ambapo ilipelekea akina mama wajawazito kushindwa kufika katika Kituo cha Afya cha Mbwera kwa ajili ya kujifungua na kuongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo litasaidia kufungua fursa za kiuchumi na upatikanaji wa huduma za kijamii kwa urahisi.

“Tumepata faraja kubwa kuona ujenzi wa daraja hili katika Kata yetu ya Mbuchi, hakika daraja hili linakwenda kutatua matatizo yote ya hapo awali ambayo yalikuwa yakitukabili na tunapata matumaini kuwa, sasa Mbwera Mashariki na Mbwera Magharibi zinakwenda kufunguka na kuwasaidia wananchi wa maeneo haya," alisema Mhe. Mpili.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani, Mhandisi Leopold Runji amesema ujenzi wa daraja la chuma la Mbuchi lenye urefu wa Mita 61 na upana wa mita 4.2 na unatarajia kukamilika hivi karibuni.
Mhandisi Runji ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo umeambatana na ufunguaji wa barabara ya Mohoro-Mbuchi-Mbwera yenye urefu wa Km 35 ambapo gharama zote ni Shilingi Bilioni 6.

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) unaendelea kufungua barabara kufika kusiko fikika katika maeneo mbalimbali nchini hasa vijijini ili kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news