Wakfu wa Mo Dewji waunga mkono juhudi za Rais Samia kuwapatia wananchi maji safi na salama

NA GODFREY NNKO

WAKFU wa Mo Dewji (Mo Dewji Foundation) umeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan za kumtua mama ndoo kichwani kwa kuhakikisha inatekeleza miradi mbalimbali ya maji mkoani Singida.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa fupi iliyotolewa leo Januari 25, 2022 na Mohammed Dewji maarufu kama Mo Dewji ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara wanaofahamika ndani na nje ya Tanzania.

Mo Dewji ambaye ametambuliwa kuwa miongoni mwa mabilionea wa umri mdogo zaidi Afrika. Pia ni mfanyabiashara na mwanasiasa ambaye amewekeza katika soka na pia katika shughuli za hisani ikiwemo kutoa sehemu ya utajiri wake kwa ajili ya kusaidia wenye uhitaji. 

"Leo, timu ya Taasisi ya Mo Dewji imerudi Singida kutengeneza na kuendeleza visima, na kuhakikisha maji salama yanaendelea kuwa rahisi mkoani Singida. Mwaka 2008, nilijenga visima vya maji salama kwa maelfu ya watu mkoani Singida, na kuboresha njia ya maji safi kutoka asilimia 23 mpaka asilimia 75,"amebainisha Mo Dewji.

Mo Dewji amefafanua kuwa, juhudi hizo anazifanya ikiwa ni kuwezesha juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwani karibu ya nusu ya Watanzania hawana njia ya kupata maji safi na salama ya kunywa.
Mwishoni mwa mwaka jana, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa alisema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inapatikana katika kila kijiji ikiwa ni utekelezaji wa kampeni yake ya kumtua mama ndoo kichwani, hivyo ni lazima kuchukua hatua ya kuhakikisha pale ambako hakuna maji safi na salama yanapatikana.

Kufuatia dhamira hiyo, Waziri Mkuu aliiagiza RUWASA akiwa Wilaya ya Kilwa, kufanya utafiti wa kina wa maeneo ambayo yatawezesha upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote yenye changamoto ya upatikanaji wa maji.

Aliyasema hayo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa vijiji vya Nasaya, Chumo na Kipatimu akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Lindi.

“Utafiti lazima ufanyike ili tujue wapi tunapa maji, Rais Samia anatoa pesa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, piteni mpime maeneo yote mtafute vyanzo na mtuambie maji yako kiasi gani, mitambo na wataalam tunao,"alisema Waziri Mkuu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news