Waziri Biteko akemea migogoro maeneo ya wachimbaji

NA TITO MSELEM-WM

WAZIRI wa Madini, Dkt. Doto Biteko amewataka wachimbaji wa madini wa vijiji vya Lubungo Kata ya Mikese na Maseyu Kata ya Dwata Wilaya ya Morogoro kuachana na migogoro katika maeneo yao ya uchimbaji na badala yake washirikiane katika shughuli zao cha uchimbaji madini.
Dkt. Biteko ametoa kauli hiyo alipotembelea vijiji hivyo vyenye shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu ambapo amesema migogoro baina ya wawekezaji wa madini na wachimbaji wadogo mkoani Morogoro inatakiwa kuisha kwa wao wenyewe kushirikiana kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo na kueleza kuwa migogoro hiyo hailipi na badala yake inazidi kuwarudisha nyuma na kukimbiza maendeleo kwenye maeneo yao.

Aidha, Dkt. Biteko amesema, mapinduzi katika Sekta ya Madini yameongezeka katika kipindi cha uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambapo mapato yatokanayo na madini yameongezeka.
Sambamba na hayo, Dkt. Biteko amesema,kwa sasa wawekezaji kutoka nje wanakuja kwa wingi kutokana na kufunguliwa kwa milango ya nchi ambapo hivi karibuni nchi ilishuhudiwa kusainiwa kwa mikataba mikubwa ya uchimbaji madini.

Pia, Dkt. Biteko amewataka wachimbaji wa madini nchini wamuunge mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na namna alivyoweza kufanya ushawishi wa kuwaleta wawekezaji baada ya kwenda nje ya nchi na kufanya mazungumzo na viongozi wenzake.
“Mimi na wenzangu kutoka Wizara ya Madini tunaona, juzi juzi tumesaini mikataba mingi ya uchimbaji mkubwa wa madini ambayo haijawahi kutokea ila katika kipindi cha Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan imetokea,”amesema Dkt. Biteko.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Biteko amesema, kwa sasa Serikali inafanya juhudi za makusudi kuhakikisha watanzania wanashiriki kikamilifu katika uchumi wa madini na kuzifungamanisha sekta zingine katika fursa zilizopo kwenye sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando amempongeza Dkt. Biteko kwa kutembelea wilaya hiyo na kumuahidi kuyafanyia kazi maagizo yake yote atakayoyatoa.
Msando amesema, uongozi wa wilaya yake utasimamia Sekta ya Madini kikamilifu pamoja na kutatua kero zitokanazo na sekta hiyo sanjari na kuboresha maisha ya wananchi wa eneo hilo ambao licha ya madini kuwepo katika maeneo yao, lakini bado wanaishi katika nyumba za matope na majani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news