Waziri Mhagama atoa maelekezo kwa watumishi wa wizara yake

NA DOREEN ALOYCE

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amewataka watumishi wa wizara hiyo kuendelea kusimamia majukumu yao kwa ufanisi, kutekeza zile programu walizonazo kwa Kila idara pamoja na kutumia maarifa waliyonayo katika kuleta mafanikio.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dodoma wakati alipokuwa kwenye kikao na wafanyakazi wa ofisi hiyo pamoja na taasisi zake waliopo Dodoma kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yakiwemo mafanikio yaliyojitokeza katika kipindi cha mwaka 2021.

Aidha, Mhagama amesema kuwa katika kufanikisha kusudi la Serikali wafanyakazi hao wanapaswa kudumisha mshikamano,uwajibikaji wa pamoja katika kutekeleza majukumu,uaminifu huku wakitumia hekima na busara kwenye utendaji kazi wao.

"Pia niwatake kuendelea kupambana na rushwa na vitendo ambavyo haviendani na utumishi wa umma badala yake mtumie busara,hekima katika ufanisi wa kazi huku mkiwa wawazi kutafuta haki zenu kusiko kuwa na malalamishi ambayo hayana tija,"amesema Waziri Mhagama.
Amesema kuwa, wizara imeweza kufanikiwa mambo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vyuo sita vya watu wenye ulemevu ambavyo vitasaidia kuweza kuboresha ujuzi na kuboresha maisha yao ya kila siku huku Serikali ikitenga Bilioni tisa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la msajili wa vyama vya siasa.

"Pia tumepokea fedha Bilioni 2.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Tume ya Usuluhishi na Usimamizi, kituo chenye sura ya kimataifa niwatake mtakaosimamia ujenzi huo kuwa makini ili jengo liwe imara na ubora wa hali ya juu.

"Na tumepokea Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda kipya cha kisasa cha kupiga chapa ambacho kitakidhi vigezo na kusaidia Serikali kufanya kazi kwa viwango vya juu," amesema Mhagama.
Kwa upande wake Katibu wa wizara hiyo,Tixon Nzunda amesema kuwa,kutokana na maelekezo ya waziri kupitia ofisi yake watayafanyia kazi huku akiwataka watumishi kuonyesha umoja na mshikamano ili waweze kutimiza malengo yao.

"Tumefaanya maboresho mbalimbali sekta ya hifadhi za jamii na uwekeji wa mifumo ambayo itarahisisha wanachama kupata huduma kwa urahisi bila ubaguzi wowote kwani wote ni ofisi moja,"amesema Tixon.

Awali wakitoa kero zao mbele ya Waziri Mhagama wajumbe wa kikao hicho wamesema Serikali kupitia ofsi yake wanapaswa kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi na kuweka mazingira rafiki ya kutatua changamoto zao.
Pia wamemuomba kuwepo mafunzo maalumu ya kuwaandaa watumishi kabla ya kustaafu ambayo yatawasaidia kukabiliana na maisha wanapostaafu kwani wengi wao huwa wanakumbana na changamoto wanapomaliza muda wao wa kazi kwa kukosa elimu hiyo.

Hata hivyo, wameiomba Serikali kupitia Ofsi ya Waziri Mkuu kushughulikia walemavu wapatiwe viwanja kwa riba nafuu kwa ajili ya kuweka makazi yao ambayo wataweza kulipa taratibu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news