Waziri Mkuu:Vijana someni kwa bidii

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka vijana wa Kitanzania wahakikishe wanajiwekea malengo ya kusoma kwa bidii ili kupata maarifa yatakayolisaidia Taifa kupata maendeleo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ubora wa madawati wakati alipokagua ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Gehandu wilayani Mbulu, Januari 24, 2022. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere.

Pia, Waziri Mkuu amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Elimu kufanya mapitio ya sera ili kuifanya sekta hiyo kuendelea kufanya vizuri zaidi.

Ameyasema hayo leo Januari 24, 2022) alipokagua ujenzi wa madarasa ya shule za Sekondari za Gehandu na Nowu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akagua ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari ya Gehandu wilayani Mbulu akiwa katika ziara ya Mkoa wa Manyara.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali kwa upande wake imejipanga ipasavyo na itaendelea kuweka mazingira bora ya kujifunza na kufundishia ili kuwawezesha kufikia malengo yao.

Ujenzi wa madarasa unatokana na fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19. “Vijana someni kwa bidii hadi mfike chuo kikuu.”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizama madawati wakati alipokagua ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Nowu wilayani Mbulu, Januari 24, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Pia, Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote ziweke mpango wa ujenzi wa mabweni kupitia mapato yao ya ndani ili wanafunzi wakae shuleni na kupata muda wa kutosha wa kujisomea.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewakumbusha watumishi wa umma kutambua kuwa wanajukumu kubwa la kuwatumikia Watanzania na kutekeleza maelekezo ya ilani ya uchaguzi ya CCM.

Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Gehandu, Mwalimu Gadiel Bei alimshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kutoa fedha za ujenzi wa vyumba hivyo viwili vya madarasa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Gehandu wilayani Mbulu akiwa katika ziara ya Mkoa wa Manyara.

Alisema mbali na madarasa hayo pia wamejenga madarasa mengine matano kati yake mawili yametokana na fedha za ruzuku ya EP4R na matatu ni nguvu za wananchi na Halmashauri.

Mwalimu Bei alisema kukamilika kwa madarasa hayo kutaiwezesha shule hiyo yenye wanafunzi 945 wa kidato cha kwanza hadi cha sita kuongeza tahasusi nyingine ya kidato cha tano kuanzia mwezi Julai 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news