Waziri Mwingulu:Marais hawakopi ni Serikali ndio inakopa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Marais huwa hawakopi ni Serikali ndio inakopa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi huku akisisitiza kwamba Deni la Taifa ni himilivu.

Dkt.Mwigulu amesema hayo Januari 4, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza katika hafla ya kupokea Taarifa ya Mpango wa awamu ya kwanza wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya Uviko 19 Ikulu Jijini Dar es Salaam, Januari 4,2022.(PICHA NA IKULU).

"Ni jambo ambalo sio la kiungwana kukaa kusema Rais amekaa miezi tisa amekopa, Marais hawakopi ni Serikali ndio inakopa, hili sio jambo la familia ni jambo la nchi ndio maana yeye katika miezi tisa yake aliyokaa kila mwezi analipa zaidi ya Bilioni 800 kwa ajili ya madeni, madeni mengine ya Awamu zilizopita, ni madeni ya nchi na ni madeni ya Serikali, lakini sio deni la familia mojamoja.

"Sasa ukiwa unataja tu kwamba Rais wa Awamu ya Tatu alikopa akajenga Uwanja wa Ndege alipoondoka aliondoka na Uwanja wa ndege ule? Nyinyi ndiyo mliopo mtalipa deni na nyinyi ndio mnatumia Uwanja wa Ndege.

"Mheshimiwa Rais Samia wale wasiotambua kwamba unafungua uchumi ili watoto wao wapate ajira wataendelea kuelewa hayo unayoyafanya siku ukifungua uchumi biashara zikakua, watoto wao wakapata ajira, utakapoiunganisha nchi yetu ikapata fursa na uchumi ukakua watatambua kwamba hiki ulichokuwa unakifanya kina maana gani,"amesema Mheshimiwa Waziri.

Amesema, kutokana na tathimini iliyofanyika mwezi Novemba mwaka 2021 inaonyesha kuwa deni hilo ni himilivu kwa kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

“Tathimini ya uhimilivu wa deni uliofanyika Novemba kama ulivyoelekeza Rais, unaonyesha deni letu ni himilivu kwa kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

“Katika tathimini hiyo viashiria vinaunyesha kwamaba, deni la Serikali kwa uwiano wa Pato la Taifa ni asilimia 31 ambapo ukomo wa kidunia ni asilimia 55,” amesema Waziri Mwigulu.

Wakati huo huo,Waziri Wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Ummy Mwalimu amesema ujenzi wa madarasa 15,000 umekamilika kwa asilimia 95 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na maeneo machache hawajakamilisha kutokana na changamoto mbalimbali.

Miongoni mwa changamoto hizo ni upatikanaji wa malighafi ya ujenzi , uchaguzi wa maeneo ya ujenzi na hali ya hewa.

Waziri Ummy amemuhakikisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa hadi kufikia Januari 15, 2022 madarasa yatakuwa yamekamilika na wanafunzi wataanza masomo yao.

Ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO -19 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Waziri Ummy amesema, kiasi cha shilingi bilioni 240 ziliidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 12, 000 ya shule za sekondari na bilioni 60 kwa ajili ya ujenzi madarasa ya shule shikizi za msingi na shilingi bilioni 4 kwa ajili ujenzi wa mabweni 50 kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Amesema kuwa, kiasi cha shilingi bilioni 203.1 zilitolewa kwa ajili ya Sekta ya Afya na bilioni 5 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo.

Amesema, hadi kufikia Desemba 31, 2021 kwa upande wa sekta ya elimu msingi Ofisi ya Rais TAMISEMI imepokea shilingi bilioni 304 ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule za Sekondari na shule shikizi jumla 15,000 pamoja na mabweni.

Ameendelea kufafanua kuwa, ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari yatawezesha wanafunzi wote 907,803 waliofaulu mitihani ya kumaliza darasa la saba na kuingia kidato cha kwanza kuanza shule siku moja badala ya kuwa na awamu tatu kama ilivyokuwa miaka iliyopita

Waziri Ummy amesema kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI iliomba madarasa 12,000 ikiwa na makadirio kuwa watoto watafaulu kwa asilimia 90 lakini matokeo ya mitihani ufaulu ni asilimia 82 hivyo kuna madarasa ya ziada 2,292 ambayo yatasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi wa vidato vingine katika shule za sekondari.

Kuhusu ujenzi wa madarasa 3,000 ya shule shikizi, Waziri Ummy amesema serikali imewasaidia watoto wa umri mdogo kutotembea umbali mrefu, kupata elimu katika madarasa mazuri na ya kisasa badala ya madarasa ya nyasi, yaliyotengenezwa na miti na ambayo hayavutii.

“Kwa upande kwa elimu msingi tumepokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 50 katika shule za msingi zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum ambayo yatasadia kuboresha mazingira ya watoto wenye ulemavu kuweza kujifunza na kusoma katika mazingira mazuri,” amesisitiza Waziri Ummy.

Ofisi ya Rais TAMISEMI imeidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni 512 kupitia mpango wa maendeleo wa taifa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 kwa ajili ya Sekta ya Elimu, Afya na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments