Zanzibar iliyojaa neema chini ya Rais Dkt.Mwinyi yawavutia wengi, Ujerumani yarejea

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amepongeza hatua za Serikali ya Ujerumani za kujesha uhusiano na ushirikiano wa kimaendeleo kati yake na Zanzibar.

Mheshimiwa Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Januari 26,2022 katika salamu zake za shukurani kwa Serikali ya Ujerumani kwa hatua yake ya kurejesha uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar wa muda mrefu ambao utakuwa wa kimaendeleo, uhusiano ambao ulisitishwa na nchi hiyo ya Ujerumani tangu mwaka 2015.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akipiga makofi baada ya kuzindua Taasisi ya Maendeleo ya Ujerumani na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Mhe.Regine Hess, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said na kulia kwa Balozi ni Dkt.Katrin Bornemann. (Picha na Ikulu).

Amesema kuwa, kurejesha ushirikiano na uhusiano kati ya Zanzibar na Ujerumani kutaimarisha maendeleo hapa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo ni mdau mkubwa wa maendeleo ya Zanzibar katika visiwa vyake vyote vya Unguja na Pemba.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza katika hafla ya uhuwishaji wa uhusiano baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Ujerumani pamoja na Uzinduzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Ujerumani, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.
Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Mhe.Regine Hess wa kwanza kulia akimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akizungumza wakati wa uhuwishaji wa uhusiano baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Ujerumani na Uzinduzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Ujerumani akiwa na maofisa Ubalozi.
 
Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, Ujerumani ina historia kubwa ya kuunga mkono maendeleo ya Zanzibar na pia, ni nchi ambayo ilianzisha uhusiano wake na kusaidia Zanzibar tokea mwaka 1965 ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za makazi, maarufu nyumba za Mjerumani zilipo Kikwajuni Mjini Zanzibar, nyumba za maendeleo za Bambi, kusaidia maendeleo ya Mji Mkongwe Zanzibar pamoja na kusaidia huduma mbalimbali za kijamii. 

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, kurejesha uhusiano huo wa maendeleo haupo kimaneno badala yake uko kivitendo kwani tayari Ujerumani imeshakusudia kusaidia kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo miradi kadhaa ya maendeleo kama vile miradi ya maji, afya, michezo pamoja na kuunga mkono Dira ya Uchumi wa Buluu.
Kwa upande wa Sekta ya Afya, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, Ujerumani imekusudia kuiunga mkono Zanzibar katika kutoa huduma za bima ya afya kwa wote ambapo utaratibu maalum utawekwa. 

Pia, kwa upande wa maji, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa hatua ya nchi hiyo kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu, kuchimba visima vipya, vyanzo vipya vya maji pamoja na vifaa kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa huduma hiyo kutokana na kuwepo changamoto katika upatikanaji wake. 

Kwa vile Ujerumani imeahidi kuisaida Zanzibar katika sekta ya michezo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, hatua hiyo itasaidia kukuza michezo hasa ikifahamika kwamba michezo ni ajira, afya na pia, michezo huondoa vitendo viovu kwa vijana sambamba na kueleza hatua za kuwepo uongozi makini kwenye sekta hiyo.
Mabalozi wadogo wanaowakilisha nchi zao wanaofanyika kazi Zanzibar wakifuatilia hafla ya uhuwishaji wa uhusiano baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Ujerumani pamoja na Uzinduzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Ujerumani, wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia katika hafla hiyo.
 
Katika maelezo yake Rais Dkt.Mwinyi ametoa shukurani kwa Serikali ya Ujerumani pamoja na Ubalozi wa Ujerumani kwa hatua yake hiyo ya kurejesha upya uhusiano na ushirikiano na Zanzibar, hali ambayo itaweza kusaidia katika mpango wa miaka mitano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Ameeleza kwamba hatua ya Ujerumaini kujitokeza hadharani na kuahidi kurejesha uhusiano na ushirikiano na Zanzibar ni jambo la kupongezwa na kuungwa mkono kwani Zanzibar bado inahitaji wadau wa maendeleo zikiwemo nchi kama Ujerumani pamoja na washirika wengine zikiwemo sekta binafsi. 

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Jamal Kassim kwa upande wake alitoa shukurani kwa Ubalozi wa Ujerumani kwa jinsi ulivyoonesha ushirikiano na hatimae kurejesha uhusiano wake kwa vitendo. 

Mapema Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Regine Hess alieleza kufarijika kwake na hatua hiyo na kusisitiza kwamba nchi yake inaimani kubwa na uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi pamoja na serikali yake anayoiongoza ya Umoja wa Kitaifa hatua ambayo imepelelea Zanzibar kuendelea kuwa na amani na utulivu mkubwa.
Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Mhe. Balozi Regine Hess akizungumza wakati wa hafla ya uhuwishaji wa uhusiano baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Ujerumani pamoja na Uzinduzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Ujerumani.Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama Zanzibar wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza katika hafla ya uhuwishaji wa uhusiano baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ya Ujerumani, pamoja na Uzinduzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Ujerumani.

Ameahidi kwamba miradi yote iliyoahidiwa na Ujerumani itatekelezwa ipasavyo kwani nchi hiyo ina historia kubwa ya kuisadia Zanzibar katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Nao viongozi wandamizi wa Ubalozi wa Ujerumani walieleza azma ya nchi hiyo ya kurejesha uhusiano na ushirikiano na Zanzibar pamoja na kueleza mikakati iliyowekwa na Ujerumani katika kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo maji, afya, michezo, elimu, kuwawezesha wananchi kiuchumi pamoja na kuiunga mkono Dira ya Uchumi wa Buluu. 

Rais Dkt.Mwinyi pamoja na Balozi Regine Hess walifungua pazia maalum kuonesha ishara ya uzinduzi wa kurejesha ushirikiano na uhusiano huo wa kimaendeleo kati ya Ujerumani na Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news