Zanzibar sasa ni mwendo wa uwekezaji tu, Serikali yaweka mazingira bora na rafiki

NA RAJAB MKASABA 

KUFUNGULIWA kwa hoteli mpya ya kitalii yenye hadhi ya Nyota Tano ijulikanayo kwa jina la Marijani Resort and SPA hapa Zanzibar ni miongoni mwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kuimarisha sekta ya utalii hapa nchini, juhudi ambazo zimeweza kuungwa mkono na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwinyi (kushoto) wakifuatana na Mwekezaji Rahim Balu (katikati) pamoja na kupata maelezo wakati alipotembelea sehemu mbalimbali mara baada ya ufunguzi wa Hoteli ya Marijani Resort &Spa ikiwa ni katika shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar hafla iliyofanyika Januari 6,2022 Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja, kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Kazi,Uchumi na Uwekezaji, Mhe.Mudrik Ramadhan Soraga. (Picha na Ikulu). 

Marijani Resort and SPA inamilikiwa na Kampuni ya Z.K. VENTURE pamoja na wanahisa wake ambao ni Kampuni ya Avenes Limited, Harwood Limited na Amcop Investment Limited zote kutoka nchini Mauritius kwa kushirikiana na mwekezaji mzalendo Rahim Baloo, ambapo uzinduzi wake ni miongoni mwa shughuli zilizopangwa kufanyika katika shamrashamra za sherehe za maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. 

“Nachukua fursa hii kutoa shukurani maalum kwa Mwekezaji wetu ndugu Rahim Baloo na wamiliki wenzake kutoka Visiwa vya Mauritius kwa kuichagua Zanzibar kuwa sehemu ya kuwekeza mradi wao huu wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 10.5 ikiwa ni ongezeko la asilimia 147 ya mtaji wa makisio ya awali wa Dola za Kimarekani Milioni 4.25. 

“Nawahakikishia kwamba, uamuzi waliouchukua wa kuwekeza hapa Zanzibar ni sahihi na mitaji pamoja na amana zao zipo salama, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, itafanya kila linalohitajika katika kuhakikisha kwamba, wawekezaji wetu hawa wanayafikia matarajio yao kwa faida ya pande zote mbili,”amesema Dkt. Mwinyi katika hotuba yake ya uzinduzi wa hoteli hiyo. 

Kumbukumbu zinaonesha kuwa, Zanzibar ina historia kubwa katika mambo mbalimbali ya kuvutia wageni na watalii kwa jumla hii ni kutokana na mazingira yake pamoja na vivutio mbalimbali vilivyopo hapa Zanzibar. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwinyi wakipata maelezo kutoka kwa Mwekezaji Rahim Balu baada ya ufunguzi wa hoteli ya Marijani Resort &Spa ikiwa ni katika shamra shamra za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar hafla iliyofanyika huko Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja. (Picha na Ikulu). 

Kama inavyofahamika kuwa kabla ya Mapinduzi sekta ya utalii haikupewa umuhimu mkubwa na iliendelezwa kwa ajili ya kunufaisha kundi la wachache hasa waliokuwa wakilimiki hoteli chache na nyumba za kulala wageni. 

Kabla ya Mapinduzi, Zanzibar ilikuwa na hoteli mbili tu za kitalii ambazo ni Zanzibar Hotel na Africa House, lakini mara baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964, Serikali ilianza kuipa sekta hii umuhimu unaostahiki kwa kufanya mageuzi ya uendeshaji katika hoteli hizo kwa lengo la kuziimarisha. 

Mipango ya Serikali ya kujenga hoteli za kisasa na kuifanya sekta ya utalii kuwa ni sehemu muhimu kwa uchumi wa Zanzibar na utamaduni wa watu wa Zanzibar ilipangwa na kuanza kutolewa mara tu baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964. 

Mnamo mwaka 1970 Serikali ilijenga hoteli mpya katika eneo la Funguni na kuitwa Hoteli ya Bwawani, Hoteli hii ilifunguliwa rasmin mnamo mwaka 1974 na ikawa ni miongoni mwa hoteli bora na kubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki. 
Sambamba na hilo, Hoteli ya Uwanja wa Amaan ambayo ilijengwa katika eneo la Uwanja wa michezo wa Amaan ambapo kwa upande wa Pemba hoteli nyingine zilijengwa katika mji wa Wete, Chake Chake na Mkoani hatua ambayo ilipelekea kuimarika sana kwa utalii baada ya kumaliza ujenzi wa hoteli hizo. 

Shirika la Utalii lililojulikana kwa jina la “Tanzania Friendship Tourist Bureau (TFTB) liliimarishwa kwa kupatiwa vifaa, nyenzo na vyombo vya usafiri kwa ajili ya kuwatembeleza watalii ambapo Shirika lilifanya juhudi za kuwasomesha wafanyakazi wake ili kuwajengea uwezo wa kusimamia mabadiliko yaliyokuwa yamepangwa katika kuendesha sekta hiyo. 

Kutokana na kuanguka kwa bei ya zao la karafuu katika miaka ya themanini na kudumu hadi mwanzoni mwa 2010, Serikali iliongeza nguvu za kuimarisha sekta ya utalii ili kupunguza utegemezi wa zao hilo sambamba na athari za kiuchumi zilizosababishwa na kuanguka kwa bei la zao hilo. 

Baada ya mabadiliko na juhudi hizo kubwa kwenye sekta ya utalii, idadi ya watalii ilianza kuongezeka mwaka hadi mwaka kutoka wastani wa watalii 10,000 kutoka miaka ya sabini hadi kufikia watalii 29,211 mwaka 1986. 

Mipango ya kuendeleza utalii ilianza mnamo miaka ya mwisho ya 1980 na juhudi hizo ziliendelezwa hatua kwa hatua na kuanzia mwaka 1987 hadi 1993 kulikuwa na miradi 111 tu ya uwekezaji wa hoteli na nyumba za kulala wageni. 

Mafanikio makubwa yamepatikana katika kipindi hicho na hadi mwaka 2018 tayati zilikuwepo nyumba za kulaza wageni 548 zikiwa na takribani vyumba 10,679 katika madaraja mbalimbali. 

Kwa kuimarisha sekta ya utalii, Serikali ilitunga Sheria Namba.9 ya kuimarisha utalii, mwaka 1996 yenye lengo la kukuza ujenzi wa Hoteli za kisasa ambayo iliipa nguvu Kamisheni ya Utalii iliyoanzishwa mnamo mwaka 1992 kwa lengo la kusimamia sekta ya utalii hapa nchini. 

Mabadiliko ya Sheria ya Utalii Namba 6 ya mwaka 2009 ambayo imefuta Sheria Namba, 9 ya 1996 imefanyiwa marekebisho na sasa Sheria mpya Namba 7 ya mwaka 2012 inatumika hatua ambayo inapelekea Sheria hiyo kwenda sambamba na dhana ya Utalii kwa wote. 
Juhudi zote hizo zimekuwa chachu ya kuvutia watalii na wawekezaji ambao wako tayari kutumia kiwango kikubwa cha rasilimali zao kwa kujenga hoteli za kisasa zinazokidhi mahitaji ya wageni wa aina na daraja zote. 

Kufunguliwa kwa hoteli hii ni ushahidi tosha wa mikakati ya kiuwekezaji inayolenga kuhamasisha uwekezaji wa mitaji mikubwa kwa kuruhusu kuwekeza miradi ya hoteli ya kiwango cha juu kwa hapa Zanzibar. 

Kwa lengo la kuimarisha uwekezaji, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imekuwa ikipanga na kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya kuimarisha mazingira ya uwekezaji Zanzibar. 

Serikali imeelekeza juhudi kubwa katika kuimarisha miudombinu muhimu kwa maendeleo ya sekta ya utalii, ambapo imeimarisha viwanja vya ndege na bandari kwa lengo la kuimarisha sekta ya usafirishaji ambayo ndio msingi wa sekta ya utalii. 

Hivi karibuni Serikali imesaini mkataba na Kampuni ya DNATA ya Dubai kwa ajili ya kuimarisha huduma za ndege na abiria kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume. 

Aidha, Serikali kupitia Mamlaka ya viwanja vya ndege imesaini mkataba na Kampuni ya Emirates Leisure Retail ya Dubai kwa kutoa huduma za maduka na migahawa katika uwanja huo pamoja na Kampuni ya SEGAP ili kusaidia shughuli za uendeshaji ambapo hivi sasa mazungumzo yanaendelea na kampuni mbalimbali kwa ajili ya kukiimarisha Uwanja wa Ndege wa Pemba. 

Juhudi za kuimarisha uwanja huo zimelenga katika utekelezaji wa dhamira ya kukifanya Kisiwa cha Pemba kuwa eneo maalum la Kimkakati la uwekezaji. 

Kuwepo kwa hoteli hii kutainua daraja la utalii Zanzibar kwa kuwa na watalii wa daraja la juu pamoja na kupanua soko la utalii kwa nchi za Ghuba na Mashariki ya Mbali sambamba na kustawisha sekta nyingine kama vile kilimo, uvuvi na biashara. 
Kwa hapa Zanzibar takwimu za uwekezaji zinaonesha kuwa sekta ndogo ya Hoteli na migahawa imeweza kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka nje kuliko sekta nyingine. 

Hii imetokana na juhudi za pamoja baina ya sekta binafsi na Serikali katika kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji hapa Zanzibar. 

Juhudi za pamoja na kuwepo kwa hali ya amani na utulivu ni mambo ambayo yanaendelea kuwavutia sana wawekezaji kuja kuwekeza Zanzibar. 

Ndio maana wawekezaji wengi wameonesha hamu kubwa ya kuja kuwekeza katika visiwa vidogo vidogo ambavyo Serikali imeamua kuvitangaza kwa wawekezaji wenye lengo la kuwekeza kwenye miradi ya hadhi ya juu. 

Tayari wawekezaji wamejitokeza kwenye visiwa 10 vilivyotangazwa kuvikodisha ambapo kwa pamoja kuna kila sababu ya kudumisha ushirikiano uliopo pamoja na hali ya amani na utulivu. 

Kutokana na umuhimu sambamba na azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi, Taasisi inayosimamia Uwekezaji hapa Zanzibar (ZIPA) iliyo chini ya Wizara ya Fedha, inaendelea kuwa mstari wa mbele kushauri na kusimamia utekelezaji wa Sera ya Uwekezaji kwa kutambua kuwa uwekezaji wa mitaji binafsi hapa nchini unachangia ongezeko la ajira, mapato ya Serikali, uwepo wa teknolojia za kisasa na utaalam. 

Lakini kubwa zaidi ni kuhakikisha kuwa uwekezaji unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuinua maisha ya wananchi wa Zanzibar sambamba na kupunguza umaskini hapa nchini. 

Imeelezwa kwamba pato lililopatikana kutoka sekta ya utalii limekuwa likiongezeka kwa kiasi kikubwa kila mwaka ambapo kwa mfano pato hilo liliongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 157.1 mwaka 2011 hadi kufikia Dola za Kimarekani milioni 269.3 katika mwaka 2014 na katika mwaka 2017 lilifikia Dola za Kimarekani milioni 489. 

Mafanikio yote hayo yanakuja kwa kuwepo kwa utulivu mkubwa hapa Zanzibar ukiwemo utulivu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii pamoja na Serikali kufanya mapitio ya Sera na kufanya marekebisho ya Sheria mbalimbali zikiwemo za Biashara, Kodi, Uwekezaji, Ardhi, na nyinginezo ambazo zote zimejaribu kuweka mazingira bora ya uwekezaji hapa Zanzibar. 

Kwa lengo la kuimarisha usalama wa watalii wanaoingia nchini, Serikali imeanzisha Kikosi maalum cha Askari wa Utalii ambacho Rais Dkt. Mwinyi alikizindua rasmi tarehe 19 Novemba, 2021 kwani kulinda na kuendeleza usalama wa raia na wageni ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane. 

“Nawahimiza wafanyakazi wote wanaotoa huduma kwa wawekezaji na wageni wahakikishe wanatoa huduma zinazokidhi viwango na matarajio ya watalii na kwa misingi ya uzalendo na uadilifu. Kila mmoja atekeleze majukumu yake akijua kwamba, utalii ndio muhimili mkuu wa uchumi wetu”. 

“Kwa hivyo, mafanikio tunayoyapata ndio msingi wa kukuza Pato la Taifa, uingizaji wa fedha za Kigeni pamoja na kuimarisha ajira bado ntuna nafasi ya kuongeza ukusanyaji wa mapato,” alisisitiza Rais Dkt. Miwnyi katika uzinduzi wa Hoteli hiyo. 

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwamba bado wajasiriamali hawajaunganishwa vizuri na sekta ya utalii, kwani kwenye eneo hilo kuna fursa nyingi za wajasiriamali wanaozalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo za utamaduni, kunufaika na soko linaloendelea kukua kwa kuuza bidhaa zao katika hoteli za kitalii. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwinyi (kushoto) wakifuatana na Mwekezaji Rahim Balu (katikati) pamoja na viongozi wengine wakifuatana kabla ya kuagana baada ya kumalizika kwa hafla ya ufunguzi wa hoteli ya Marijani Resort &Spa ikiwa ni katika shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar katika Kijiji cha Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja leo.(Picha na Ikulu). 

Aliwakumbusha wawekezaji kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa makubaliano yaliyomo kwenye mikataba yao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatii sheria za nchi, hasa katika ulipaji wa kodi na tozo mbali mbali wanazopaswa kulipa wakiwa nchini, watii sheria na miongozo ya sheria inayohusu ajira na maslahi ya wafanyakazi. 

Rais Dkt. Mwinyi alitoa pongezi kwa maalum kwa wawekezaji wa hoteli hiyo kwa namna wanavyoshirikiana na wananchi wa kijiji hicho cha Pwani Mchangani katika kuliendeleza zao la mwani na kuwataka wananchi nao kuendelea kuishi vizuri na wawekezaji wote waliopo kijiji hicho na Zanzibar kwa jumla. 

Post a Comment

0 Comments