Benki Kuu yashirikisha wananchi mbinu za kuwashinda matapeli wizi wa fedha

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha hatoi na hashirikishi taarifa zake za benki zikiwemo za simu za mkononi kwa mtu yoyote kwa kuwa, kufanya hivyo atakuwa salama zaidi dhidi ya mbinu zinazotumika na matapeli.
Afisa Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa, Bw. Fabian Kasole ameyasema hayo leo Februari 16, 2022 katika mafunzo ya waandishi wa habari za uchumi na biashara yanayoendelea katika Ukumbi wa Benki Kuu tawi la Mbeya.

Leo ni siku ya tatu ya mwendelezo wa mafunzo hayo ya siku tano ambayo yanaratibiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Katika mafunzo hayo, Bw. Kasole amewasilisha mada ya Maendeleo ya Mradi wa Malipo ya Papo kwa Papo Tanzania (TIPS), Wajibu wa Benki Kuu katika usimamizi wa kampuni za simu za mkononi (MNOs) zinazotoa huduma za kifedha.

Sambamba na hatua zinazochukuliwa kukabili matapeli katika huduma mbalimbali za kifedha nchini ambapo, Bw. Kasole amesema kuwa,kuna mbinu mbalimbali za utapeli, lakini utapeli ulio mkubwa kwa sasa ni ule wa ushawishi au ulaghai wa watu (social engineering).

"Walaghai hutumia mbinu mbalimbali kuhadaa watu kwa lengo la kushawishi mhusika kuwashirikisha taarifa zake za benki au kuhamisha fedha.

"Ulaghai hufanyika kwa kupitia simu, ujumbe mfupi au barua pepe na hata wakati mwingine ana kwa ana, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuchukua tahadhari na kutokubali kutoa taarifa zake kwa mtu yeyote zinazohusiana na benki au simu.
"Inapotokea umepoteza simu yako na ilikuwa na taarifa zako zote ikiwemo mifumo ya benki na miamala mingine, kwanza unapaswa kutoa taarifa mara moja kwa watoa huduma mfano benki na kampuni ya simu ili waweze kuzuia kwa muda huduma zako zote. Hatua hiyo, itasaidia pale mhalifu anapotaka kufanya alichokusudia baada ya kuiba simu yako kisifanikiwe, baada ya kuripoti huko na hatua kuchukuliwa, utapaswa kwenda jeshi la polisi kutoa taarifa kwa ajili ya hatua itakayofuata,"amefafanua Bw.Kasole.

BoT inachukua hatua gani?

Bw. Kasole amesema kuwa, Benki Kuu ya Tanzania inachukua hatua mbalimbali za kuhakikisha vitendo vya kitapeli vinafikia kikomo nchini.

Amesema, miongoni mwa hatua ni kutoa elimu kwa umma ikiwemo kuweka kanuni za kumlinda mlaji wa huduma za fedha (Financial Consumer Protection Regulations, 2015).

"Kanuni zinazitaka taasisi zote zinazotoa huduma za fedha na zinazosimamiwa na Benki Kuu kuwa na mpango wa elimu ya fedha kwa wateja wao na kanuni zimeweka mambo ya kuzingatiwa katika utoaji wa elimu,"amesema Bw.Kasole.

Amesema, Benki Kuu imekuwa ikitoa elimu kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na matumizi ya ujumbe wa simu za kiganjani,kuwataka watumiaji wa huduma za fedha kutunza taarifa zao za siri.

"Pia kutotekeleza maelekezo juu ya matumizi ya huduma za fedha bila kujiridhisha na kutofanya miamala ya fedha na watu wasiowajua. Benki Kuu pia inawataka watoa huduma za fedha kuwa na mipango na kutoa elimu kwa watumiaji wote wa huduma za fedha,"ameongeza Bw.Kasole.

Bw.Kasole anasema kuwa, pia kuna hatua za kwa pamoja za Benki Kuu na Mamlaka ya Mawasiliano kupitia usajili wa namba za simu.

"Kupitia TCRA na Benki Kuu, Serikali iliagiza makampuni ya simu na watoa huduma fedha kidigitali ikiwemo kupitia upya usajili wa namba za simu ili kuhakikisha kila namba imesajiliwa kwa namba ya kitambulisho cha taifa (NIDA) na kwa kupitia alama za vidole (biometric registration), lengo likiwa ni kuhakikisha kila mmiliki anatambulika rasmi.Kupitia zoezi hili, idadi ya matapeli kwa sasa imepungua,"amesema Bw.Kasole.

Wakati huo huo amesema kuwa,ili kudhibiti hali hiyo Serikali imeanzisha namba moja ya watoa huduma kuwasiliana na wateja wao.

"Yaani namba 100 ili kudhibiti namba za simu za matepeli kuwapigia wateja wa huduma za kifedha. Pia Serikali imeanzisha namba maalumu, ambayo ni 15040 ili kutuma taarifa za jumbe za utapeli na namba husika.

"Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma juu ya huduma hii na kuwataka kutozingatia ujumbe au mawasiliano yoyote nje ya namba 100 kuhusu huduma za kifedha,"amesema Bw.Kasole.

Hatua za kujikinga

Bw. Kasole anasema kuwa, ili kuweza kukabiliana na hali hiyo kila mmoja anapaswa kutafakari kabla ya kuchukua hatua.

Amesema, pia unapaswa kuepuka kutekeleza maelekezo ya mtu usiyemjua bila kutafakari au kupata uhakika au uhalisia wa kile unachoelezwa.

"Mhalifu atajaribu kukuhimiza kuchukua hatua kwa kukujengea hisia ya uharaka au kukufanya uamini udharura wa malipo, jihadhari na hisia, wakati mwingine mhalifu anaweza kukutengeneza mazingira ya hisia na kutokukupa nafasi ya kumuuliza maswali au kudadisi kutakapokuwezesha kujiridhisha.
"Hakikisha unatunza namba yako ya siri, kumbuka hakuna siri zaidi ya mtu mmoja. Vivyo hivyo, unapaswa kuangalia ni nani unayezungumza naye kwani tapeli anaweza kuiga wenzako, washirika, wasambazaji au marafiki. Ni vyema kuwasiliana na mhusika mwenyewe kwa kutumia mawasiliano uliyo na imani nayo.

"Usitoe taarifa zako,ikiwa humjui unayezungumza naye, usijibu maswali mengi. Kumbuka kila taarifa unayowapatia inaweza kuwasaidia kukusanya taarifa zako zinazoweza kuwasaidia kutekeleza azima yao. Ni vyema kuwa mwangalifu na usiogope kukata simu. Ikiwa unashuku au unahisi mawasiliano yanaviashiria vya utapeli au kujua taarifa zako binafsi, kata simu.

"Vivyo hivyo, linda simu yako au kadi yako ya benki na usimpe mtu yeyote simu yako au kadi yako kwa kuwa anaweza kuvitumia katika kufanikisha azima yake. Na hakikisha unatoa taarifa kwa wakati pale unapokutana na utapeli au upotevu wa kifaa chenye uwezo wa kuwasiliana na akaunti zako za fedha.

"Kumbuka kila wakati kwamba wahalifu wakati mwingine wanaweza kuwa tayari wanajua jina, anuani au msimbo wa aina ya akaunti yako, hii inamaanisha kuwa wamefanya utafiti wao,"amefafanua Bw. Kasole.

Kuhusu kurugenzi

Afisa huyo Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa, Bw. Fabian Kasole anasema kuwa, Sheria ya Benki Kuu 2006, Ibara ya 6 (BoT ACT 2006 sec 6) na Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa mwaka 2015 zinasisitiza kuhusu kuendeleza na kuhakikisha usalama na udhibiti wa mifumo ya malipo ya Taifa.

Sambamba na vyombo vyote vinavyojishughulisha na mifumo ya malipo nchini yakiwemo mashirika yote ya kifedha, kama benki, vyombo mbalimbali vya fedha wakiwemo watoa huduma za mifumo ya malipo, kama kampuni za simu, kampuni za kadi za malipo na nyinginezo.

Bw. Kasole anafafanua kuwa,majukumu waliyonayo katika kurugenzi hiyo ni usimamizi wa mifumo ya malipo nchini ambao umegawanyika katika maeneo makubwa mawili.

Mosi, Bw.Kasole amesema ni kusimamia mifumo ya malipo ya nchi inayoendeshwa na taasisi za fedha na zisizo za fedha mfano kampuni za simu na kampuni za teknolojia katika sekta ya fedha (fintech).

Pili, anasema ni kuendesha mifumo ya malipo kwa ajili ya kuleta ufanisi na usalama wa malipo nchini.

Wakati huo huo anasema kuwa, kurugenzi hiyo ina jukumu la kuhakikisha uwepo wa mifumo ya malipo nchini inayoaminika, salama, yenye gharama nafuu, iliyounganishwa na inayokubalika kisheria mahali popote nchini ili kukidhi mahitaji ya kiuchumi.

"Ikiwemo kupunguza vihatarishi vinavyoweza kujitokeza katika kufanya malipo kwa miamala na kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kisasa iliyo na ubora na inayokidhi matakwa ya watumiaji. Sambamba na kuandaa na kupendekeza mazingira bora ya kisheria na kitaasisi yatakayowezesha mifumo ya malipo kustawi nchini na kuhakikisha watumiaji wanalindwa vyema kadiri teknolojia na mifumo ya malipo inavyobadilika,"amefafanua Bw.Kasole.

Ametaja majukumu mengine kuwa ni kudhibiti ucheleweshaji wa malipo kwa walengwa (float), kuimarisha mzunguko wa kifedha ili kukuza uchumi (financial deepening in the economy) na kufikisha huduma za kifedha kwa wananchi wahitaji wote (Financial Inclusion).

"Bila kusahau jukumu la kutoa kwa uhakika na ufasaha taarifa muhimu za kifedha na mtiririko mzima wa mwenendo wa malipo kwa wadau wote nchini ili kuboresha majukumu ya Benki Kuu ya kusimamia sera za kiuchumi za nchi,"anafafanua.

Mifumo ya malipo

Bw.Kasole akizungumzia kuhusiana na mifumo ya malipo amesema kuwa, imegawanyika katika makundi makuu mawili likiwemo la mifumo ya malipo yenye thamani ndogo.
Amesema, hii ni mifumo ya uhahulishaji fedha ambayo kwa kawaida hushughulikia kiasi kikubwa cha malipo
ya thamani ndogo.

"Ni malipo ya kila siku kati ya watu binafsi, makampuni, mashirika ya serikali kwa miamala au malipo ya thamani ndogo na kwa kawaida hayana asili ya uharaka,"amesema Bw.Kasole.

Pia ametaja mifumo mingine kuwa ni ya malipo yenye thamani kubwa ambayo inahusika katika uhahulishaji fedha ambayo kwa kawaida hushughulikia kiasi kikubwa cha malipo yenye thamani kubwa.

"Ni malipo ya kila siku kati ya taasisi na hata watu binafsi (watu binafsi, makampuni, benki, mashirika na taasisi za serikali), haya ni malipo yenye asili ya thamani kubwa na kwa kawaida ni ya haraka na huzingatia muda,"anasema Bw.Kasole.

Kuhusu TIPS

Bw.Kasole akizungumzia maendeleo ya Mradi wa Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Hapo (TIPS) anasema kuwa,Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika mwaka wa fedha 2020/2021 iliazimia kutekeleza mfumo wa malipo ya reja reja
(Retail Payments System).

Anasema, huu ni mfumo wa malipo unaolenga kuongeza ufanisi kwa kuwaunganisha watoa huduma za kifedha wa kidijitali (FSPs) na kufanya huduma jumuishi za fedha kuwa rahisi.

"Mfumo huu unaitwa ‘Tanzania Instant Payments System (TIPS). Awamu ya kwanza ya utekelezaji ilianza mwezi Septemba mwaka 2020 na kukamilika mwezi Julai mwaka 2021.Mwezi Agosti 2021, mfumo ulianza kutumika kwa watoa huduma za kifedha wa kielektroniki (FSPs) wachache (pilot FSPs), ambapo zoezi litakamilika mwezi Februari 2022,"amesema Bw.Kasole.

Amebainisha kuwa, awamu ya pili ya utekelezaji itaanza mwezi Machi, 2022 ambapo watoa huduma wengine watajumuishwa kwenye mfumo ikiwa ni pamoja na kuongeza huduma nyingine.

"Hivyo, Benki Kuu itaendelea kuboresha mifumo ya malipo yote kwa ujumla ili kuongeza ufanisi,usalama,njia mbalimbali za mifumo ya malipo ili kupunguza matumizi ya fedha taslimu,"anasema Bw.Kasole.

Post a Comment

0 Comments