Benki Kuu yatoa neno wanaohifadhi fedha nyumbani, wanaotumia sarafu ya 200/- michezo ya kubahatisha

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania imewashauri wadau mbalimbali wakiwemo wananchi kuacha tabia ya kuhifadhi fedha nyumbani, kwani kwa kufanya hivyo wanasababisha upungufu wa fedha katika mzunguko bila sababu na wakati mwingine ni hatari zaidi.

Msimamizi wa Mzunguko wa Sarafu kutoka Idara ya Sarafu chini ya Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo ya Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Ilulu Said Ilulu ameyasema hayo leo Februari 16,2022 katika siku ya tatu ya mwendelezo wa mafunzo kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara yanayofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania tawi la Mbeya.
Katika mafunzo hayo yanayoratibiwa na Benki Kuu, Bw.Ilulu alikuwa anawasilisha mada zilizoangazia kuhusu Maana ya Sera ya Sarafu Safi na nafasi ya wananchi kuifanikisha pamoja na Namna ya Kutambua alama za usalama katika fedha za Tanzania.

"Kuhifadhi fedha nyumbani kunasababisha upungufu wa fedha kwenye mzunguko na kusababisha Benki Kuu kuingia gharama zisizo na msingi za kuingiza sarafu kwenye mzunguko kinyume na malengo ya kiuchumi ya nchi. Nitoe rai kuwa, kila mmoja atumie taasisi za kifedha zikiwemo benki kwa ajili ya kuhifadhi fedha zake, kwani ni njia nzuri na salama zaidi ya kutunza fedha.

"Ukiweka fedha benki zinaingia katika mzunguko, tofauti na unavyoziweka ndani ambapo ni hatari, wakati mwingine kuna majanga ya moto au aina nyingine ambapo yakitokea ukawa umehifadhi fedha zako nyumbani ni rahisi zaidi kuzipoteza, lakini zikiwa benki zinakuwa mahali sahihi,"amefafanua Bw.Ilulu.

Wakati huo huo, Bw.Ilulu amesema,kwa wananchi ambao wapo mbali na huduma za benki ni vema wakatumia huduma jumuishi za kifedha kwa kutumia watoa huduma za simu ili kulinda usalama wao na fedha kuwa kwenye mzunguko.

Pia ametoa wito kwa wananchi kuzihifadhi fedha zikiwemo noti katika mazingira mazuri ili ziendelee kubaki na ubora wake kwa muda mrefu kwa ajili ya matumizi.
"Nichukue nafasi ii kutoa rai kwa wananchi wenzangu, tusikunje noti, tunatakiwa kuhifadhi noti zikiwa zimenyooka, tunapokunja noti zinachoka haraka,"amesema Bw.Ilulu.

Akizungumzia kuhusu utambuzi wa noti bandia, Bw. Ilulu amesema Sarafu ya Benki Kuu imetengenezwa kwa karatasi maalum na kuna alama maalum ambazo hazionekani kwa macho. Amesema, alama hizo zimewekwa katika noti zote kwa ajili ya usalama.

Michezo ya kubahatisha

Katika hatua nyingine, Bw.Ilulu amewataka waendesha michezo ya kubahatisha kwa kutumia mashine kutumia 'token' ambazo ni maalum kwa michezo hiyo badala ya kutumia sarafu za Benki Kuu kwani kufanya hivyo ni kujitafutia makubwa.

“Kutumia sarafu ya shilingi 200 badala ya token kufanya kama ndiyo sarafu ya kuchezea ni kosa linaloangukia kwenye makosa ya uhujumu uchumi, hivyo wanaofanya hivyo waache na tayari Bodi ya Michezo ya Kubahatisha wana taarifa hiyo na wanapaswa kulisimamia suala hilo,"amesema Bw. Ilulu.

Bw.Ilulu amesema kuwa, tayari Benki Kuu imewachukulia hatua watu waliobainika kufanya matumizi ya sarafu ya shilingi 200 kuigeuza kama token na hivyo kusababisha matumizi yasiyo rasmi ya sarafu hiyo na tayari hatua zimeendelea na zinaendelea kuchukuliwa kwa watu mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments