Benki Kuu:Elimisheni wananchi wanaochukua mikopo kuitumia kwa malengo tarajiwa

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa rai kwa waandishi wa habari kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini kutumia nafasi zao kutoa elimu kwa wananchi wanaochukua mikopo katika benki na taasisi za fedha, kuhakikisha wanatumia fedha wanazokopa kwa malengo tarajiwa ikiwemo kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Kaimu Meneja Uhusiano kwa Umma na Itifaki wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi.Vicky Msina ametoa rai hiyo leo Februari 18, 2022 wakati akifunga mafunzo ya siku tano yaliyoandaliwa na BoT kwa waandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha.

Mafunzo hayo ambayo yameratibiwa na Benki Kuu kuanzia Februari 14 hadi leo Februari 18,2022 yamefanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu tawi la Mbeya huku yakiwakutanisha pamoja waandishi wa habari kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Dar es Salaam na Zanzibar.

"Wananchi kwa kufanya hivyo, watakakuwa wanajijengea jina zuri la kukopesheka, na hivyo kuweza kupata mikopo zaidi na pengine kwa riba nafuu zaidi.

"Pia hii itawasaidia wao katika shughuli zao za kiuchumi, kuweka vizuri mizania ya mikopo ya benki na taasisi husika na kufanya ziweze kukopesha watu wengi zaidi. Aidha, wananchi wanapaswa kukumbuka kwamba, kwa sasa taarifa zao zote za mikopo zinapatikana, hivyo wasipokuwa waaminifu, watajifungia nafasi ya kupata mikopo kwenye taasisi zingine,"amefafanua Bi.Msina.

Kaimu Meneja huyo amesema kuwa,pia ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anazingatia elimu ya utunzaji mzuri wa noti na sarafu za Tanzania ili zidumu kwa muda mrefu.

Amesema, kwa kufanya hivyo kutaisaidia kupunguza gharama kwa Serikali kuchapisha fedha zingine. "Bado kuna watu wanakunjakunja hovyo hovyo noti au kuzishika wakiwa na unyevunyevu, hali ambayo inapunguza kwa kiasi kikubwa uhai wa fedha hizo na kulazimisha Serikali kuingiza gharama za kutengeneza zingine.
"Matumaini yetu ni kwamba kupitia elimu mliyoipata, mtakuwa mabalozi wetu katika kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutunza fedha katika hali nzuri,"amesema Bi.Msina.

Pia amerejea wito wa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania wakati anafungua semina hiyo Februari 14, 2022 kuwa, ni wajibu wa wanahabari kote nchini kuhamasisha wananchi kujihusisha na shughuli za ujenzi wa taifa.

Sambamba na kutangaza kazi mbalimbali, zikiwemo za ubunifu ambazo wananchi wanafanya na kuchangia maendeleo ya taifa pamoja na fursa mbalimbali ambazo, ama zimeendelezwa kidogo au hazijaendelezwa kabisa ili kuvutia wawekezaji kuziendeleza na kwa jinsi hiyo kuchangia maendeleo ya taifa.

Wakati huo huo, Bi.Msina amesema kuwa, Idara ya Uhusiano kwa Umma na Itifaki ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) itaendelea kushirikiana kwa karibu na waandishi na vyombo vyote vya habari nchini ili waweze kuhudumia jamii kupitia kazi na taarifa mbalimbali zinazotoka Benki Kuu.

“Sisi tuko tayari wakati wote na tutaendelea kushirikiana nanyi katika kuwaunganisha na wataalamu wetu pindi mnapohitaji ufafanuzi ili muweze kupata habari sahihi mnazohitaji hususani zinazoihusu Benki Kuu ya Tanzania na sekta ya fedha kwa ujumla,"amebainisha Bi.Msina.

Pia amesema, kwa miaka tisa tangu Benki Kuu ianze kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha yamekuwepo maendeleo mazuri ya ubora wa taarifa zinazotangazwa na vyombo vya habari kuhusu benki hiyo.
“Tumekuwa tukitoa mafunzo kwenye kanda zote, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha ili hatimaye habari kuhusu Benki Kuu ya Tanzania ziweze kuwafikia wananchi kwa usahihi.Tangu kuanzishwa kwa semina hizi mwaka 2013, hadi hivi sasa, kumekuwa na maendeleo makubwa namna taarifa mbalimbali zinazotolewa na Benki Kuu zinavyotumiwa na wanahabari pamoja na vyombo vyenu vya habari.

"Uelewa miongoni mwenu umeongezeka sana na hata ushirikiano pia umekua. Haya ni manufaa makubwa ya semina hizi. Benki Kuu itaendelea kuzitumia semina kama hii kama sehemu mojawapo ya kushirikiana na wadau wake muhimu,"amesema Bi.Msina.

Pia amesema, kutokana na mada mbalimbali walizojifunza waandishi hao wa habari wanapaswa watumie uelewa huo kusaidia kufikisha ujumbe kwa wananchi ili waijue sekta ya fedha nchini inafanya nini ili waweze kuzitumia fursa mbalimbali ikiwemo kuchukua mikopo kwenye benki na taasisi za fedha ili kuboresha shughuli zao za kiuchumi
Naye Mwenyekiti wa washiriki wa mafunzo hayo ya siku tano,Bi.Docras Mtenga kwa niaba ya wenzake ameishukuru Benki Kuu ya Tanzania kwa kuendelea kuandaa mafunzo hayo kwani yamekuwa na manufaa makubwa.

“Tunaamini washiriki wamejifunza mengi na tutakwenda kutumia elimu tuliyoipata ili kuandika habari za uchumi, biashara na fedha kwa usahihi,"amesema Bi.Mtenga.
Miongoni mwa mada zilizowasilishwa na wataalamu wabobezi wa masuala ya kiuchumi kutoka Benki Kuu ya Tanzania katika mafunzo hayo ya siku tano ni pamoja na Utayarishaji na Utekelezaji wa Sera ya Fedha nchini,Maendeleo ya Mradi wa Malipo ya Papo kwa Papo Tanzania (TIPS), Wajibu wa Benki Kuu katika Usimamizi wa Kampuni za Simu za Mkononi (MNOs) zinazotoa huduma za kifedha.

Mada nyingine ni hatua zinazochukuliwa kukabili matapeli katika huduma mbalimbali za kifedha nchini,Majukumu ya Kurugenzi ya Masoko ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania,Uwekezaji kwenye Dhamana za Serikali.
Pia Maendeleo ya Mifuko ya Udhamini wa Elimu ya juu inayodhaminiwa na Benki Kuu ya Tanzania ukiwemo Mfuko wa Udhamini wa Gilman Rutihinda (The Gilman Rutihinda Trust Fund) na Mfuko wa Udhamini wa Elimu ya Juu wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na nyinginezo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news