Bhoke:Uzazi wa mpango umenipa tumaini jipya la kuishi maisha bora

NA GODFREY NNKO

WANANDOA wameshauriwa kutoa kipaumbele katika masuala ya uzazi wa mpango kwa kuwa, hiyo ni njia nzuri inayomuwezesha mama na mtoto kuwa na afya bora.
Uhusiano mwema baina ya wanawake, wanaume katika familia ni jambo la faraja ambalo linawapa nafasi wapendanao kufanya uamuzi sahihi kwa mustakabali wa familia yao hususani matumizi ya huduma za uzazi wa mpango. (Picha na Maktaba ya TMEPiD).

Sambamba na kuwapa nafasi wanandoa hao kushiriki kikamilifu katika kuwahudumia watoto wao kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali ya msingi na kushiriki shughuli za maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa Februari 6, 2022 na Bhoke Chacha mkazi wa Tambani wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani wakati akizungumza na DIRAMAKINI BLOG.

Amesema, moja wapo ya siri ya mafanikio yake ni pamoja na kukubaliana kwa pamoja yeye na mumewe kuwa, ili waweze kuwa na familia bora ikiwemo kushiriki shughuli za maendeleo wanapaswa kuridhia kwa pamoja kuhusu aina ya uzazi wa mpango unaowafaa.

"Ninamshukuru sana mume wangu (Chacha), nilipomueleza kuhusu umuhimu wa uzazi wa mpango hakuniwekea kipingamizi,kwa pamoja tulifunga safari hadi Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, tulipokelewa kwa ukarimu na tukapewa huduma na wahudumu wa pale.

"Walitueleza aina nyingi za uzazi wa mpango, walitupa nafasi ya kufanya uamuzi, mume wangu (Chacha) na mimi tulishauriana na tukaridhia nitumie njia ya kipandikizi. Tangu nitumie hiyo njia, huu ni mwaka wa pili na nusu...ninajisikia furaha na kama unavyoona watoto wangu wanafuraha pia. Uzazi wa mpango umenipa tumaini jipya la kuishi. Nilihisi kifo awali, lakini sasa nahisi kuwa na nguvu.

"Ninaamini baada ya miaka mitano ya hiki kipandikizi, tutaamua kufanya maamuzi na Baba watoto wangu, kama tuzae au tuongeze muda. Sijutii kuchukua uamuzi huu, kwani licha ya kipato kidogo ambacho mzee anakipata katika biashara ya kuuza mayai na mimi hapa gengeni, tukichanganya tunaweza kumudu maisha yetu, kwa sababu tumejiwekea malengo,"anasema Bi.Bhoke ambaye ni mama mwenye watoto watatu, mmoja wa kike na wengine wa kiume.

Kwa upande wake mumewe, aliyejitambulisha kwa jina la Chacha amesema kuwa, waliamua kuchukua uamuzi huo wa uzazi wa mpango baada ya kubaini kuwa,uzao wao ulikuwa wa haraka.

"Hawa watoto wa kwanza, tuliwapata ndani ya miaka miwili, niliumia sana kwa sababu nilihisi kama nimemuonea mke wangu, sikumpa nafasi ya kupumzika na kumlea mtoto wetu wa kwanza, afya yake ilidhoofika, lakini ninamshukuru Mungu alitupigania na kumuwezesha kuyamudu mapito hayo, ndiyo maana baada ya kupata mtoto wa tatu, tuliamua kuzingatia maelezo ya wataalamu wa afya,"amesema Chacha.

Chacha amesema, awali alikuwa hatambui umuhimu wa uzazi wa mpango kwa sababu walipotokea mkoani Mara, familia nyingi hazitoi kipaumbele kuhusu masuala ya uzazi wa mpango. Lakini, baada ya changamoto aliyoipitia ameona uzazi wa mpango ni miongoni mwa njia nzuri katika kujenga familia bora na uchumi imara.

Njia anayotumia Bhoke ni kati ya njia za muda mrefu ambayo unaweza kuirudia kadri ya hitaji lako, wataalamu wa afya wanaeleza kuwa, ukitumia njia hii unaweza kupata ujauzito mara utakapoacha kuzitumia. 

Hii ni njia nzuri ikiwa unataka kusubiri zaidi ya miaka miwili kabla ya kupata mtoto mwingine.Vipandikizi, hiki ni kijiti cha plastiki anachowekewa mwanamke chini ya ngozi kwenye mkono wake na kinaweza kuwa kimoja au viwili. 

Hivi huzuia mwanamke asipate ujauzito kwa muda kati ya miaka mitatu hadi mitano kutegemea na aina ya vipandikizi alivyotumia.

Chacha anaongeza kuwa, alikuwa na dhana potofu kuwa, ukiwa na idadi kubwa ya watoto ndiyo watakuja kuwa mkombozi katika maisha yake siku za usoni, lakini baada ya kupata ufahamu ametambua kuwa, idadi hiyo ya watoto isipokuwa katika mpangilio, ikapata elimu na mahitaji au kuendelezwa kwa namna yoyote ile haitakuwa na tija badala yake inaweza kuwa mzigo katika familia.

"Kwa maana hiyo, nimetambua kuwa suala la uzazi wa mpango wakati mwingine halipaswi kuwa hiyari, bali liwekewe muongozo ili tuwe na familia ambazo zinaweza kukabiliana na maisha siku za usoni na kuwa na tija katika kuendeleza gurudumu la maendeleo kwa Taifa na si kuwa tegemezi,"amesema Chacha.

Umuhimu

Meneja wa Utetezi wa Shirika la Tanzania Communication and Development Centre (TCDC), James Mlali anasema, huduma za uzazi wa mpango ni muhimu zaidi katika kuboresha afya ya mama, afya ya mtoto ikiwemo kuleta maendeleo kwa ujumla kwa kusaidia Serikali kupanga bajeti ambayo inaweza kutosheleza.

Anasema,juhudi zinapaswa kufanywa ili kuongeza huduma hizo nchini kuanzia maeneo yote ya vijijini na mijini pamoja na kuruhusu sekta binafsi kushiriki katika kutoa huduma jumuishi ya soko.

Mlali ameyasema hayo hivi karibuni katika semina juu ya Mbinu Jumuishi za Soko la Huduma za Uzazi wa Mpango zinazoweza kupatikana kwa urahisi kwa kila anayehitaji na kuwa endelevu kuliko ilivyo sasa.

Semina hiyo iliandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ambayo imejikita katika kukuza ushiriki wa wanaume katika Afya na Haki za Ujinsia na Uzazi, Afya ya Mama na Mtoto pamoja na Kukuza usawa wa Kijinsia katika Shughuli za Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi la Tanzania Men as Equal Partners in Development (TMEPiD) na kufadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshugulikia Idadi ya Watu (UNFPA) pamoja na wengine katika utetezi wa uzazi afua za uzazi wa mpango nchini.

"Ili tuweze kupiga hatua katika huduma za uzazi wa mpango nchini, kwani tunapaswa kufanya kazi kubwa kulingana na taarifa rasmi za afya na idadi ya watu za mwaka 2015 hadi 2016 ya Tanzania Demographic and Health Survey, tunaona kuwa watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango walifikia asilimia 32 katika kila asilimia 100, ambacho ni kiwango kidogo, hawajafikia hata theluthi,"amesema Mlali.

Amesema, matumizi ya kila mwaka yanaonesha kuwa, kufikia mwaka 2020 idadi hiyo ilikuwa imefikia asilimia 41 ambapo malengo yake ni kuhakikisha watumiaji hao wanafikia asilimia 47 mwaka 2023.

Mlali anasema, ili kuweza kufikia asilimia 47 jitihada zinahitajika kwa Serikali kufanya kazi zaidi kwa kushirikisha wadau ili watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango waweze kuongezeka nchini ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma kila sehemu ambapo huduma hizo zinaweza kukaa ikiwemo Famasi na Maduka ya Dawa Muhimu kama iliyo kwa kwa huduma za mipira ya kike na kiume (kondomu).

"Lengo sio kuwa na idadi kubwa ya watumiaji, bali ni kufanya kuongezeka kwa huduma za uzazi wa mpango ili kurahisisha watu kuzifikia na kuweza kutoa mchango mkubwa sana katika afya ya mama, afya ya mtoto na maendeleo kwa ujumla,"amesema Mlali.

Amesema kuwa, kutokana na huduma hizo kupatikana kidogo karibu ya mimba zote zinazotungwa baadhi ya mimba ambazo hazikutarajiwa kuwa wanapanga kuwa wazae, wengine wana mtoto mdogo, wengine umri umeenda sana, hana malengo ya kuzaa, lakini baada ya kushiriki tendo wanajikuta wamepata mtoto.

"Tafiti ulimwengunj zinaonesha kuwa, matumizi ya huduma za uzazi wa mpango zikifanyika vizuri, vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi vinaweza kupungua kwa asilimia 44,na vifo vya watoto vinaweza kupungua kwa asilimia 35.

"Taifa linahitaji nguvu kazi kubwa, linahitaji wanawake wenye afya njema, linahitaji watoto wakue vizuri, wasikatishwe au maisha yao yasikatishwe, katika umri mdogo waweze kukuwa ili waweze kuwa sehemu ya nguvu kazi ya Taifa,"amefafanua Mlali.

Amesema, huduma za uzazi wa mpango zina mchango mkubwa katika maendeleo kwa sababu ndizo ambazo zinasaidia familia, au watu binafsi kuamua idadi ya watoto ambao wanataka kuzaa, wawazae kwa wakati gani, wawaachanishe kwa umri gani kati ya mtoto na mtoto na hizo ndiyo kanuni bora kwa ajili ya afya mama na mtoto kwa maendeleo ya nchi.

Mlali anasema kuwa, Serikali inapaswa kuelekeza bajeti ya kutosha kwenye masuala yahusuyo uzazi wa mpango na inapaswa kupewa kipaumbele kikubwa, pia jamii ambazo zina fikira potofu kuhusu uzazi wa mpango zinapaswa kuachana nazo.

TMEPiD

Dkt.Cuthbert Maendaenda ambaye ni Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Tanzania Men as Equal Partners in Development (TMEPiD), ushirikiano wa pamoja baina ya wananchi, Serikali na taasisi binafsi utasaidia kuwezesha huduma za uzazi wa mpango kupatikana kwa urahisi na kwa haraka popote pale vijijini na mijini.

"Taasisi yetu inahusika na utetezi na kuimarisha elimu afya ya uzazi katika jamii hasa ikiwalenga wanaume, kwa nini tunawalenga wanaume? Kwa sababu mbalimbali za kijamii, walikuwa ni kundi ambalo limewekwa pembeni. 

"Ukizungumzia mambo ya uzazi wa mpango zinawalenga wanawake, njia za uzazi wa mpango nyingi zinawalenga wanawake, huduma zinazotolewa mahali zinawalenga mama na mtoto, hivyo wanaume walikuwa wanakaa pembeni.Tukiangalia kimila, wanaume ndiyo wafanya maamuzi,kama ni mzazi mtoto apatikane lini, wapatikane watoto wangapi, maamuzi mara nyingi yanategemea wanaume, mila zimewapa hiyo nguvu au upendeleo.

"Kwa hiyo, kwa sasa tumejikita katika kujiimarisha kwenye utetezi wa afya ya uzazi wa mpango, tukisaidiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu hapa Tanzania, na kwa sababu tayari Serikali imekwishajiwekea malengo, Malengo ya Uzazi wa Mpango 2030, Serikali imepania kupanua matumizi ya huduma za uzazi wa mpango. 

"Na kupanua wigo wa wananchi kuweza kupata huduma za uzazi wa mpango, sasa katika kufanya hivyo, tukajikuta miaka mingi mtu akitaka kupata huduma ya uzazi wa mpango alipaswa kwenda kiliniki, usipokwenda kiliniki hauwezi kupata huduma,lakini pia kuna watu wengine wanapata shida ya kupata huduma, ukienda kiliniki au zahanati huduma hamna, kwenye jamii zingine ambapo vijana ambao ndiyo wapo kwa wingi zaidi, suala la uhusiano wamekuwa wakishindwa kufikia hizo huduma kwa sababu ya hofu ya wazazi wao, ndugu zao kwa sababu zinatolewa na watu wazima.

"Kwa hiyo kuna kundi kubwa sana, la Watanzania wanapotaka kuifikia huduma ya uzazi wa mpango wanashindwa kuifikia. 

"Kwa sasa tumekuja na Approach ya Total Market, katika hili tunachotaka ni huduma ya uzazi wa mpango zipatikane kila mahali, na kupitia wadau mbalimbali na si kwenda kliniki, tukiangalia huko miaka ya nyuma hata kupata huduma ya baba, mpira wa kiume au kondomu ilikuwa lazima uende kliniki, lakini kwa sasa ukitaka kondomu inapatikana kila mahali ikiwemo katika maduka ya rejareja.

"Kwa hiyo mtu hawezi kuacha kutumia kondomu, kwa sababu inapatikana kila mahali, na kwa sababu tunataka huduma nyingine zipatikane kila mahali za uzazi wa mpango ikiwemo katika famasi na maeneo mengine ili ziweze kupatikana kwa wingi hususani mashirika yanayotoa huduma hizo. Kwa hiyo mtu hawezi kuacha kutumia kondomu,"amesema Dkt.Maendaenda.

Amesema, tukifanya hivyo Taifa litapata faida nyingi kupitia upangaji salama wa uzazi wa mpango na hakutakuwa na kisingizio cha mtu kushindwa kuitumia huduma hiyo.

"Na kwa sababu hiyo tunataka huduma za uzazi wa mpango zipatikane kila mahali wakati wowote, kwa mfano katika maduka ya kutolea huduma za dawa kwa kuwapa mafunzo,mashirika kama TMARK ambao wapo mitaani, kwa hiyo, mwanamke au mwanaume akitaka huduma asilazimishwe, kama tumeweza kuzileta kondomu zikajaa, basi itafutwe njia nyingine ya kuhakikisha huduma zingine za uzazi wa mpango zinasambaa kila mahali.

"Lazima tutoe mafunzo, na kuhakikisha vikwazo vya kisera vinapatiwa ufumbuzi, kwa mfano duka la dawa muhimu haliwezi kutoa baadhi ya dawa za kuzuia mimba, sasa tunataka changamoto hiyo ipatiwe ufumbuzi ili kurahisisha mama anapotaka kwenda kuchukua vidonge vikiisha aweze kuvipata kwa haraka, vivyo hivyo kuondoa visingizio vya umbali, hivyo wengine kuacha kwenda kutumia huduma ya uzazi wa mpango,"amesema.

Pia amesema kuwa, idadi kubwa ya watu wanaoishi mijini wana uwezo hivyo inawezekana wakawa wanapatiwa huduma hizo kwa kugharamia ili kipato kitakachopatikana kiweze kupeleka huduma hiyo kwa wingi huko vijijini.

"Kwa hiyo itatupa faida kubwa ya kuhakikisha kule kijijini huduma zinajaa, lakini pia tunatetea kwamba haya mashirika ya bima na wenyewe katika huduma wanazotoa wahusishe suala la uzazi wa mpango ili kama huduma hiyo inatolewa katika vituo binafsi, waweze kufanya maamuzi ya kwenda kutumia huduma anapotaka,

"Pia itaweza kusaidia kuongeza usiri, kwa mtu ambaye anataka huduma hiyo,anaweza kuipata sehemu yoyote bila kukaa foleni,kwa hiyo unajua mimi ninatumia huduma fulani unaenda kwenye duka la dawa kupata huduma, hivyo kama mwingine anatumia kitanzi badala ya kwenda kliniki na kuambiwa kuwa havipo, ataweza kwenda kununua na kuja kuwekewa katika kituo cha afya.

"Pia itatoa nafasi kwa watumiaji wa huduma ya uzazi wa mpango mfano wanaume kupata nafasi ya kukaa na wahudumu kupata ushauri kabla ya kufanya maamuzi,"amesema.

Dkt.Maendaenda amesema kuwa, pia elimu kuhusu huduma za uzazi wa mpango iendelee kutolewa katika maeneo yote nchini ili kupunguza changamoto kwa baadhi ya makundi hususani vijana.

Hali ipoje Zanzibar?

Watunga Sera Zanzibar wamejitolea kutoa sera zinazolenga kuhakikisha upatikanaji na kuimarishwa kwa uzazi wa mpango ikiwa ni pamoja na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar na Mkatakati wa Sekta ya Afya Zanzibar (III). 

Aidha, sera hizi zinaaambatana na lengo la tatu la Maendeleo Endelevu ambalo linaweka shabaha ya kupatikana kwa huduma za afya ya Uzazi ukiwemo uzazi wa mpango kufikia mwaka 2030.

Mkakati wa Tatu wa Sekta ya Afya hasa unataja kupanua mbinu za uzazi wa mpango kama mkakati wa kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto wa umri wa chini ya miaka mitano.

Pia kuongeza nafasi za kupatikana kwa mbinu za kudumu za uzazi wa mpango kutasaidia kupunguza mimba zilizo na hatari kubwa ambazo hupatikana wakati mama amefika umri wa kutopata mtoto tena.

Kwa mujibu wa Jumuiya wa Wauguzi Zanzibar (ZANA),licha ya kujitolea kote huko kuweka sera, matumizi ya mbinu za kisasa za uzazi wa mpango visiwani Zanzibar yamezidi kurudi chini ikilinganishwa na Tanzania Bara. 

"Matumizi ya mbinu za kisasa za uzazi wa mpango Tanzania Bara yaliongezeka karibu mara tatu kati ya mwaka 1996 na 2015 huku visiwani Zanzibar yakiongezeka kwa kiasi kidogo kwa kuongezeka kutoka asilimia nane hadi 14 wakati sawa na huo.

"Zanzibar iko nyuma katika kufikia lengo lake la Uzazi wa mpango kwa asilimia 22 kufikia mwaka huu wa 2022. Mwaka 2016, takribani mara mbili ya wanawake walioolewa hawakutimiza hitaji lao la uzazi wa mpango la kutumia mbinu za kisasa za kupanga uzazi.

"Zanzibar ina nafasi nzuri ya kupanua matumizi ya mbinu za uzazi wa mpango na kuziba pengo la kutofikiwa kwa hitaji lisilotimia na kuendelea mbele kutimiza lengo la mwaka huu wa 2022. Tofauti kubwa zipo kati ya visiwa viwili vya Zanzibar - Pemba na Unguja, huku hitaji lisilotimia la uzazi wa mpango likiwa juu hasa kisiwani Pemba. Mikoa yote ya Zanzibar isipokuwa Unguja Kusini ina mahitaji ambayo hayajatimia ya uzazi wa mpango miongoni mwa wanawake wasiotaka kupata mimba tena, mahitaji ambayo yako juu kushinda kiwango cha kitaifa cha asilimia 10 kwa wanawake wa Pemba Kusini ambao hawataki watoto tena, lakini hawatumii kikamilifu mbinu yoyote ya uzazi wa mpango. 

"Njia za kudumu na za muda mrefu za uzazi wa mpango zinaweza kuwa mbinu mwafaka kwa wanawake na wanaume ambao wamefikisha familia wanayoweza kuimudu na ambao hawataki mimba nyingine na wale ambao hawakubaliwi kushika mimba kutokana na sababu za kiafya. Hata hivyo, viwango vya juu vya mahitaji yasiyotimia ya uzazi wa mpango visiwani Zanzibar vimedhihirisha kwamba bado kuna mapengo makubwa,"imefafanua ZANA.

Jumuiya hiyo inapendekeza kuwa, kuna haja ya kuhakikisha zipatikana mbinu kamilifu za uzazi wa mpango, kwani ni muhimu katika kupunguza vifo vya kina mama na watoto visiwani Zanzibar. 

Inaeleza kuwa, matumizi ya njia za uzazi wa mpango bado yako chini, hasa mbinu za kudumu za muda mrefu za uzazi wa mpango. Njia za kudumu na za muda mrefu za uzazi wa mpango ni kama vile vipandikizi vya kuwekwa mwilini, vipandikizi vinavyowekwa ndani ya mfuko wa kizazi na kuwafunga kizazi wanawake na wanaume kunaweza kuwasaidia wanawake kupanga au kupunguza mimba wanazopata.

"Utafiti unaonesha kuwa watoto wanaozaliwa kwa mpango kwa kupishana kati ya miaka mitatu na mitano hatari ya kufariki wakiwa wadogo iko chini mno.Aidha, matumizi ya njia za kupanga uzazi yanasaidia wanawake kuanza na kukoma kuzaa wanapokuwa tayari hivyo kupunguza uwezekano wa kupata mimba zilizo na hatari kubwa.

"Ongezeko la matumizi ya njia za kudumu na za muda mrefu za uzazi wa mpango inaweza kuisaidia jamii ya Zanzibar kuwa yenye afya na kutimiza malengo yake ya maendeleo,"imefafanua jumuiya hiyo.

Pia kwa mujibu wa jumuiya hiyo,Wizara ya Afya ya Zanzibar inapaswa kuchukua hatua kuongeza upatikanaji wa matumizi ya njia za kudumu na za muda mrefu za uzazi wa mpango.

"Ni kwa kuhakikisha hospitali zote zina vifaa vya kutosha kutoa huduma na mbinu za kudumu za muda mrefu za uzazi wa mpango.Maafisa wanaotoa huduma za afya wamepewa mafunzo ya kutosha juu ya mbinu za kudumu na za muda mrefu za uzazi wa mpango na kuwa na vifaa vya kazi kuwasaidia kutoa huduma.

"Wahudumu wa afya wanapaswa kujitolea katika jamii, kwani wana uwezo wa kushajihisha na kutoa mafunzo kwa jamii juu ya njia za kudumu na za muda mrefu za uzazi wa mpango na kutoa muongozo mzuri,"imeongeza ZANA. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news